May 03, 2019 22:23 UTC
  • Jumamosi, 4 Mei, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 28 Sha'aban 1440 Hijria sawa na tarehe 4 Mei 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1013 iliyopita yaani tarehe 4 Mei 1006, alizaliwa malenga na arif mkubwa wa Kiislamu wa karne ya tano Hijria Khaja Abdullah Ansari. Alizaliwa katika mji wa Herat nchini Afganistan. Alipewa lakabu ya Mzee wa Herat. Khaja Abdullah Ansari ameandika vitabu vingi vya elimu ya irfani kwa lugha za Kiarabu na Kifarsi kwa sura ya mashairi na nathari, mashuhuri zaidi vikiwa ni "Munajat Nameh", "Mahabbat Nameh" na "Zadul Arifin". Vilevile ameandika tafsiri ya Qur'ani Tukufu aliyoipa jina la "Kashful Asrar." ***

Khaja Abdullah Ansari

Miaka 810 iliyopita katika siku kama ya leo, Ibn Hajib mpokezi wa hadithi na mwanahistoria mashuhuri wa Kiislamu aliaga dunia. Alizaliwa mjini Damascus katika Syria ya leo mwaka 593 Hijria na akiwa na lengo la kustafidi na elimu ya wapokezi wa hadithi wa zama zake, alifanya safari katika miji mbalimbali na kusoma elimu ya hadithi kwa wanazuoni wakubwa wa zama hizo. Ibn Hajib alikuwa na umahiri wa aina yake katika elimu ya hadithi. ***

Ibn Hajib

Siku kama ya leo miaka 74 iliyopita, chama cha National Socialism cha Ujerumani mashuhuri kwa jina la chama cha Kinazi, kilivunjwa rasmi nchini humo. Kwa utaratibu huo kipindi cha utawala wa kidikteta, ukandamizaji na mabavu cha chama hicho ambacho kiliingia madarakani tangu mwaka 1932 nchini Ujerumani, kikafikia ukingoni. Ikumbukwe kuwa, chama cha Kinazi kiliundwa mwezi Oktoba mwaka 1920 baada ya kuongezeka harakati ya kisiasa za Munich. Hadi mwaka 1929 chama hicho kilikuwa na wanachama laki moja na 76 elfu tu lakini mwaka 1933 idadi hiyo iliongezeka na kufikia milioni mbili na kuongezeka zaidi hadi kufikia milioni sita katika miaka iliyofuata. Inaelezwa kuwa, chama hicho kilikuwa na lengo la kuyaunganisha mataifa yanayozungumza Kijerumani na kuanzisha dola moja lenye nguvu ambalo lingeweza kupanua mipaka yake. Hata hivyo baada ya kushindwa Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia chama hicho cha Nazi kilisambaratika na kutoweka. ***

Chama cha Kinazi

Katika siku kama ya leo miaka 49 iliyopita, wanafunzi wanne wa Chuo Kikuu cha serikali cha Kent katika jimbo la Ohio nchini Marekani waliuawa kwa kupigwa risasi na askari wa Gadi ya Taifa na wengine kadhaa wakajeruhiwa katika maandamano ya Wamarekani ya kupinga vita vya Vietnam. Kuanza mwaka 1969 Wamarekani hususan vijana walizidisha upinzani na maandamano ya kupinga vita na uvamizi wa nchi hiyo dhidi ya Vietnam. Maandamano hayo yalishadidi baada ya kufichuliwa habari ya mauaji ya mamia ya Wavietnam katika kijiji cha My Lai (My Lai massacre) na vilevile mwaka 1970 baada ya kuchapishwa habari ya kupanuka zaidi vita vya Vietnam na kuingia Cambodia. ***

Chuo Kikuu cha Kent

Na siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, Jospi Broz Tito, kiongozi wa Yugoslavia na mmoja wa waasisi wa Jumuiya Isiyofungamana na Siasa za Upande Wowote NAM alifariki dunia. Wakati wa kujiri Vita vya Kwanza vya Dunia mwaka 1915, Tito aliyekuwa akipigana dhidi ya Russia alitiwa mbaroni na baada ya kuachiliwa huru akiwa na Wakomonisti alipigana vita dhidi ya utawala wa Tzar. Kwa muda fulani, Tito alikuwa na nafasi muhimu kkatika Chama cha Kikomonisti cha Yugoslavia na alifungwa jela miaka 6 kwa kosa hilo. Tito aliiongoza Yugoslavia kwa muda wa miaka 35Josip Broz Tito aliaga dunia katika siku kama ya leo akiwa na umri wa miaka 88 baada ya kuugua kwa muda mrefu. ***

Josip Broz Tito