Ijumaa, tarehe 10 Mei, 2019
Leo ni Ijumaa tarehe nne Ramadhan 1440 Hijiria, sawa na tarehe 10 Mei 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 864 iliyopita alifariki dunia Muhammad Bin Muhammad, maarufu kwa jina la Ibn Khorasan, mtaalamu wa elimu ya nahau, malenga na mwandishi wa mjini Baghadad, Iraq. Ibn Khorasan alizaliwa mwaka 494 Hijiria mjini Khorasan, kaskazini mashariki mwa Iran ambapo akiwa kijana alifanya safari mjini Baghdad, Iraq kwa ajili ya kutafuta elimu. Baada ya kupiga kambi mjini hapo alipata kusoma kwa walimu wakubwa wa zama hizo. Miongoni mwa athari za msomi huyo ni pamoja na diwani ya mashairi yake yenye juzuu 10.

Siku kama ya leo sawa na tarehe nne Ramadhan mwaka 832 Ramadhan, alifariki dunia Abul-Qasim Hibatullah Ibn Ja'afar, aliyeitwa kwa lakabu ya Kadhi Said Ibn Sinai Mulk, malenga na mtaalamu wa fasihi wa nchini Misri. Abul-Qasim aliyeitwa kwa jina la babu yake Sinai Mulk alizaliwa mwaka 545 Hijiria katika familia ya Kiislamu mjini Cairo. Alijifunza Qur'ani Tukufu na elimu ya nahau mjini Cairo, huku akijifunza elimu ya hadithi na baadhi ya elimu nyingine za Kiislamu mjini Alexandria kutoka kwa walimu wakubwa wa zama zake. Akiwa kijana Ibn Sinai Mulk alikuwa na kipawa kikubwa cha kuhifadhi mashairi na kuyasoma. Ameacha athari kadhaa katika uwanja huo yakiwemo pia mashairi yanayoelezea machungu ya masaibu ya siku ya Ashura na dhulma iliyomkumba Imam Hussein (as) na watu wa familia ya Mtume (saw) katika jangwa la Karbala.

Siku kama ya leo miaka 190 iliyopita alizaliwa François-Marie Raoult, mwanakemia wa Ufaransa. Baada ya kuhitimu masomo yake katika hatua ya PHD katika Chuo Kikuu cha mjini Paris, alipanua wigo wa utafiti wake wa kielimu. Baada ya hapo alifanikiwa kuwa mmoja wa waasisi wapya wa elimu ya kemia na fizikia. François-Marie Raoult alifanikiwa pia kubuni nadharia zake katika uwanja huo.
Siku kama ya leo miaka 49 iliyopita alifariki dunia alimu mkubwa wa kidini Ayatullah Muhammad Kuhestani Behshahr. Baada ya kuhitimu masomo yake ya msingi eneo alikozaliwa, Ayatullah Kuhestani Behshahr alielekea mjini Najaf, Iraq na kushiriki darsa za wasomi wakubwa kama vile Ayatullah Mirza Naini na Sayyid Abul-Hassan Isfahani. Baada ya kupanda kielimu na kufikia hatua ya ijtihad, alirejea mjini Kuhestan na kujishughulisha na kazi ya ufundishaji na kuwaelekeza watu. Katika harakati yake hiyo alifanikiwa kujenga shule kadhaa huku akilea wanafunzi kupitia masomo ya kidini. Ayatullah Muhammad Kuhestani Behshahr alifariki duani tarehe 14 Rabiul-Awwal 1391 Hijiria kutokana na maradhi ya moyo.

Siku kama ya leo miaka 44 iliyopita, kundi linalopigania uhuru wa Sahara Magharibi liliasisi Harakati ya Kupigania Uhuru ya Polisario. Harakati hiyo ilikaribishwa na wakazi wa eneo hilo na ikaanzisha mapambano dhidi ya wakoloni wa Kihispania hadi wakoloni hao walipoondoka Sahara mwaka 1975. Hata hivyo serikali ya Uhispania ilikabidhi mamlaka ya eneo hilo kwa serikali za Morocco na Mauritania. Mauritania ililazimika kuondoka Sahara Magharibi kutokana na mapambano makali ya Polisario na hali mbaya ya ndani ya nchi hiyo. Morocco iliendelea kukabiliana na wapigania uhuru wa Polisario hadi mwaka 1991 ambapo mapigano kati ya pande hizo mbili yalisitishwa chini ya upatanishi wa Umoja wa Mataifa. Eneo hilo lingali linakaliwa na Morocco.
Na siku kama ya leo miaka 34 iliyopita utawala wa chama cha Baath wa Iraq uliwatia nguvuni watu 90 wa familia ya Ayatullah Hakim na kuwaua 6 miongoni mwao. Miaka miwili baadaye utawala wa Baath uliua watu wengine 9 katika familia ya Ayatullah Hakiim. Ayatullahil Udhmaa Hakiim alikuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa Kiislamu aliyefariki dunia mwaka 1869. Watoto wa msomi huyo na watu wengi katika familia yake walikuwa mashuhuri kwa elimu na ushawishi mkubwa katika jamii ya Iraq. Kwa sababu hiyo utawala wa Saddam Hussein ambao ulikuwa na woga kuhusu ushawishi wa familia hiyo ulianzisha vita dhidi ya viongozi wa kidini na kuwaua shahidi watu wengi wa familia ya Ayatullah Hakiim.