Jumatatu, tarehe 13 Mei 2019
Leo ni Jumatatu tarehe 7 Ramadhan 1440 Hijiria mwafaka na tarehe 13 Mei 2019 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 1430 iliyopita yaani tarehe 7 Ramadhan mwaka wa 10 tangu kubaathiwa na kupewa Utume Nabii Muhammad (saw), kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, aliaga dunia Abu Talib, ami na mtetezi mkubwa wa Mtume (saw) katika mji wa Makka. Baada ya kufariki dunia Abdul Muttalib, babu mtukufu wa Nabii Muhammad (saw), Abu Talib ndiye aliyebeba jukumu la kumlea Mtume, na akawa bega kwa bega na mwana huyo wa nduguye katika hali zote. Baada ya kupewa Utume Nabii Muhammad (saw), Abu Talib hakumwacha mkono mtukufu huyo na akasimama imara kukabiliana na washirikina wa Kikureishi. Lakini baada ya kufariki dunia Abu Talib washirikina walishadidisha maudhi na manyanyaso dhidi ya Bwana Mtume (saw), kiasi kwamba kutokana na hali ngumu mno iliyomkabili, hatimaye kwa amri ya Mwenyezi Mungu, mtukufu huyo alihama kutoka Makka kwenda Madina ambako aliasisi utawala wa kwanza wa Kiislamu.

Siku kama ya leo miaka 1239 iliyopita Ma'mun, khalifa wa utawala wa Bani Abbas alimlazimisha Imam Ridha (as) kukubali takwa lake la kuwa mrithi wa kiti cha ufalme baada yake. Ni vyema kuashiria kuwa uadui wa watawala wa kizazi cha Bani Umayyah na Bani Abbas dhidi ya Ahlul-Bayti wa Mutume (saw) ni wa muda mrefu. Vizazi hivyo viwili ni maarufu kwa dhulma, ukandamizaji na utesaji dhidi ya Ahlul-Bayti wa Mtume, ambapo havikusita hata kuwaua maimamu watoharifu wa Nyumba ya Mtume wa Allah. Baada ya Ma'mun kutwaa madaraka ya ukhalifa alihofia sana taathira chanya ya Imam Ridha (as) kwa watu na kwa kuwa alikusudia kumuweka mtukufu huyo chini ya uangalizi wake mkali, huku akijionyesha kuwa mwenye mapenzi kwa Watu wa Nyumba ya Mtume, hivyo alitoa amri ya kumuondoa Imam Ridha kutoka mjini Madina na kumpeleka Khorasan (Mash'had ya leo) na kisha akamlazimisha kukubali kuwa mrithi wa kiti cha ufalme. Siku kama ya leo, yaani tarehe 7 Ramadhan mwaka 201 Hijiria, khalifa huyo aliwasilisha mbele ya mtukufu huyo suala hilo ambapo hata hivyo alilipinga. Baada ya kulipinga, mtawala huyo dhalimu alitumia vitisho dhidi ya Imam Ridha (as) ambapo baadaye alikubali tu kwa kutikisa kichwa huku mtukufu huyo akisisitiza kuwa jambo hilo halitofikiwa. Baada ya hapo mtukufu huyo alitumia fursa hiyo kuweza kueneza mafundisho sahihi ya dini ya Uislamu suala ambalo baadaye lilimfanya Ma'mun kuchukizwa na hatua yake ya kumtoa mjini Madina na ni baada ya hapo ndipo akapanga njama ya kumuua, njama ambayo ilitekelezwa sawa na tarehe 30 Swafar mwaka 203 Hijiria.
Siku kama ya leo miaka 929 iliyopita alizaliwa Ibn Zuhra, mmoja wa wataalamu wakubwa wa elimu ya fiqhi na mtaalamu pia wa elimu ya theolojia mashuhuri wa karne ya sita Hijiria. Ibn Zuhra alizaliwa mjini Aleppo, Syria ya leo ambapo pia alitokea kuwa msomi mashuhuri wa Kiislamu. Baada ya kuhitimu masomo yake ya awali alielekea mjini Najaf, Iraq na kufanikiwa kuinukia zaidi kimasomo. Alitabahari katika masomo ya fiqhi, usulu fiqhi, theolojia na fasaha ya lugha ya Kiarabu. Ibn Zuhra alifariki dunia mwaka 585 Hijiria.
Siku kama ya leo miaka 306 iliyopita, alizaliwa mjini Paris Alexis Cloude Clairaut mwanahesabati mashuhuri wa Ufaransa. Alikuwa na hamu kubwa na somo la hesabati ambapo akiwa na umri mdogo wa miaka 18 alifanikiwa kujiunga na Chuo cha Sayansi cha Ufaransa. Clairaut alipata umashuhuri mkubwa duniani kutokana na utafiti makini aliofanya katika nyanya tofauti za sayansi. Msomi huyo aliaga dunia mwaka 1765.
Siku kama ya leo miaka 266 iliyopita, alizaliwa Lazar Carnot, mwanasiasa, jenerali na mtaalamu wa hisabati wa nchini Ufaransa. Msomi huyo anayehesabika kuwa mmoja wa waasisi wa elimu mpya ya uhandisi, alitabahari pia katika fani ya uhandisi na stratijia ya kijeshi huku akiwa mmoja wa viongozi wenye taathira wa ushindi tofauti wa wanamapinduzi wa nchi hiyo. Ni kwa ajili hiyo ndio maana akaitwa kwa lakabu ya 'roho ya kijeshi ya mapinduzi ya Ufaransa.' Baada ya ushindi wa mapinduzi ya nchi hiyo alishikilia nyadhifa mbalimbali za uongozi ikiwemo nafasi ya uanachama wa mkutano mkuu wa chama tawala na Wizara ya Vita ya Ufaransa. Lazar Carnot alifariki dunia mwaka 1823 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, alizaliwa Bi Daphne du Maurier mwandishi wa riwaya, wasifu na tamthiliya wa Kiingereza. Maurier alizaliwa katika familia ya wasanii na iliyokuwa pia na wataalamu wa fasihi. Ni kutokana na kukulia katika mazingira kama hayo, ndipo Bi Daphne du Maurier akafanikiwa kukuza kipaji chake katika uwanja wa uandishi. Miongoni mwa vitabu vyake mashuhuri ni Scapegoat na Rebecca. Mwandishi huyo aliaga dunia mwaka 1889.
Na siku kama ya leo miaka 40 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Shamsiya, mkataba wa kutoshtakiwa Wamarekani nchini Iran au Capitulation Accord ulifutwa nchini kufuatia mapambano ya wananchi Waislamu wa Iran, ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu na kuasisiwa mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini. Kwa mujibu wa mkataba huo, raia wa Marekani aliyekuwa nchini Iran alikuwa na kinga kamili ya kisheria dhidi ya kufunguliwa mashtaka. Kwa kadiri kwamba hakuna taasisi au chombo chochote cha kisheria cha Iran kilichokuwa na mamlaka ya kumfungulia mashtaka na kumuhukumu raia wa Marekani aliyekuwa akiishi Iran na kesi za raia hao wa Kimarekani zilipaswa kusikilizwa nchini kwao.