Alkhamisi, tarehe 16 Mei, 2019
Leo ni Alkhamisi tarehe 10 Ramadhan 1440 Hijria, inayosadifiana na tarehe 16 Mei 2019.
Siku kama ya leo miaka 1443 iliyopita yaani tarehe 10 Ramadhani miaka mitatu kabla ya Hijra, alifariki dunia Bi Khadija binti Khuwailid mke mtukufu wa Mtume Muhammad (saw) katika mji wa Makka. Bi Khadija ambaye alikuwa mmoja wa wanawake mashuhuri na tajiri wa Makka aliolewa na Mtume Mtukufu miaka 15 kabla ya kubaathiwa mtukufu huyo. Bi Khadija alikuwa mtu wa kwanza kuamini ujumbe wa Mtume Muhammad (saw) na alitumia uwezo na utajiri wake katika kuisaidia dini ya Kiislamu. Kuweko Bi Khadija SA pamoja na Mtume wa Uislamu kulikuwa na umuhimu mkubwa kiasi kwamba Mtume (saw) alikitaja kifo cha mkewe huyo kipenzi kuwa ni msiba mkubwa. Mtume aliutaja mwaka aliofariki dunia Bi Khadija na msaidizi wake mwingine mkubwa yaani Abu Talib kuwa mwaka wa majonzi na huzuni. Hii ni kwa sababu Abu Talib ami yake Mtume (saw) pia alifariki dunia mwaka huo huo.

Siku kama ya leo miaka 955 iliyopita aliuawa na wapinzani waziri msomi na maarufu wa silsilah ya utawala wa Seljuk, Khwaja (Khoja) Nizam al-Mulk. Alizaliwa mwaka 410 Hijiria katika mji wa Tous, kaskazini mwashariki mwa Iran ambapo alihudumu kwa kipindi cha miaka 40 katika utawala huo. Katika kipindi hicho Khwaja (Khoja) Nizam al-Mulk aliweza kuasisi shule kama vile Nidhamiyah ya mjini Baghdad na baada ya kuasisi shule hiyo alianza na kazi ya kuwafundisha elimu za fiqhi, tafiri ya Qur'ani na elimu nyingine karibu wanafunzi elfu sita. Athari maarufu ya Nizam al-Mulk ni kitabu kinachoitwa 'Siyasat Nomeh' au 'Siyarul-Muluuk' chenye vipengee 50 huku kikiwa na mada tofauti zikiwemo za Qur'ani Tukufu, riwaya na sira ya Mtume Muhammad (saw), visa vya Mitume, hekaya na historia za nchi tofauti.
Siku kama ya leo miaka 517 iliyopita, ardhi ya Honduras inayopatikana leo huko Amerika Kusini iliunganishwa na makoloni ya Muhispania. Kabla ya hapo Honduras ilikuwa kituo cha utamaduni wa kaumu ya Maya. Hata hivyo baada ya Honduras kuvamiwa na kukaliwa kwa mabavu na Uhispania, kabila hilo liliangamizwa na kupotea. Mwanzoni mwa karne ya 19 Miladia na kutokana na kuvurugika hali ya ndani ya Uhispania, Honduras kama ilivyokuwa kwa makoloni mengine, ilitumia fursa hiyo kuweza kujipatia uhuru wake.
Siku kama ya leo miaka 231 iliyopita alizaliwa mjini Hamburg Friedrich Ruckert, malenga na mtaalamu wa masuala ya mashariki ya dunia wa nchini Ujerumani. Alikuwa mtafiti mkubwa wa masuala ya mashariki, aliyefundisha katika vyuo vikuu vya Ujerumani. Alifanya juhudi ya kutafsiri mashairi kwa lugha ya Kifarsi, Kiarabu na Kichina. Kadhalika alijifunza fasihi na tamaduni za eneo hilo na kuzitumia katika kusoma mashairi. Aidha Friedrich Ruckert alikuwa mmoja wa malenga wa Kijerumani aliyefanikiwa kutarjumu diwani ya mashairi ya Hafez (malenga mkubwa wa Kiirani) katika lugha ya Kijerumani ambapo tarjama yake imechapishwa mara kadhaa nchini humo. Miongoni mwa athari ya Friedrich Ruckert ni pamoja na kitabu kinachoitwa 'Msimu wa Machipuko wa Upendo' na 'Sharqiyat.'
Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, Jeshi Jekundu la Umoja wa Kisovieti lilianza kuondoka nchini Afghanistan. Baada ya Nur Muhammad Taraki kupinduliwa, serikali ya kwanza ya kikomunsti iliyokuwa ikipata himaya ya moja kwa moja ya Urusi ya zamani ilianzishwa nchini Afghanistan. Utawala wa Taraki uliondolewa madarakani mwanzoni mwa mwaka 1979 kupitia mapinduzi mengine yaliyoongozwa na Hafidhullah Amin mmoja wa watu wake wa karibu. Lakini Warusi hawakumpenda Hafidhullah ambaye alikuwa akitaka kujikurubisha kwa Marekani na kuanzisha uhusiano kati ya Afghanistan na Mashariki na vilevile Magharibi na hivyo wakaipindua serikali yake.
Na siku kama ya leo miaka 22 iliyopita, Jenerali Mobutu Sese Seko rais na dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zaire ya zamani, aliikimbia nchi hiyo baada ya vikosi vya majeshi ya waasi vilivyokuwa vikiongozwa na Laurent Kabila kukaribia mji wa Kinshasa. Mobutu alichukua madaraka ya nchi hiyo mnamo mwaka 1965 kupitia mapinduzi ya kijeshi na kisha kutawala kwa muda wa miaka 32. Licha ya kiongozi huyo kuwa dikteta asiye na huruma, lakini alikuwa akiungwa mkono na madola ya Magharibi hasa Marekani na Ufaransa. Kutokana na Congo DR kuwa katika eneo nyeti na muhimu kijiografia katikati mwa bara la Afrika na kuwa na utajiri mkubwa wa madini ikiwemo almasi, imekuwa ikizingatiwa sana na kumezewa mate na nchi za Magharibi. Siku moja baada ya Mobutu kuikimbia nchi hiyo, vikosi vya waasi viliuteka mji wa Kinshasa na kiongozi wao yaani Laurent Kabila, akashika hatamu za uongozi wa nchi.