May 17, 2019 22:54 UTC
  • Jumamosi, 18 Mei, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 12 ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani 1440 Hijria sawa na tarehe 18 Mei 2019 Miladia.

Siku hii ya leo kwa mujibu wa kalenda ya Kiirani, yaani tarehe 28 Ordibehesht ni siku ya kumuenzi mwanasayansi mkubwa, mshairi na msomi mtajika wa Irfan wa Iran, aliyefahamika kwa jina Hakim Omar Khayyam. Abul Fatah Omar ibn Ibrahim Khayyam Neishabouri, mwanafalsafa, mwanahesabati, mnajimu, mshairi, tabibu na mnajimu mkubwa wa Kiirani alizaliwa mwishoni mwa karne ya 5 au mwanzoni mwa karne ya 6 Hijria. Alizaliwa kati ya mwaka 417 na 440, katika mji wa Neishabour, katika mkoa wa  Khorasan Razavi kaskazini mashariki mwa Iran. Katika uhai wake, Khayyam alipata umashuhuri kutokana na busara na kipaji kikubwa alichokuwa nacho katika nyuga za utabibu, unajimu na hesabati, lakini dunia ya leo inamkumbuka na kumtambua kama bingwa wa falsafa. Kitabu chake mashuhuri alichokipa jina la Ru'ba'iyat  kinatambulika kote duniani, na kimetarjumiwa kwa lugha nyingi mashuhuri. Miongoni mwa kazi zake nyingine ni vitabu vya Nowruznome na Risala ya Mazingira. ***

 

Kwa mujibu wa baadhi ya wapokezi na kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Qamaria, leo ni siku ambayo Nabii Issa Ibn Maryam AS aliteremshiwa kitabu kitukufu cha Injili. Neno Injili ni la Kigiriki na lina maana ya bishara. Jina hilo limetajwa mara 12 katika Qur’ani Tukufu na kitabu hicho kinaitambua Injili kuwa ni kitabu cha Mwenyezi Mungu SWT chenye sheria na kanuni za mbinguni. Hata hivyo kitabu kinachojulikana hivi sasa kwa jina la Injili si kile alichoteremshiwa Nabii Issa Masih, bali ni riwaya na kumbukumbu zilizokusanywa na wanafunzi wake baada ya Yeye kupaa mbinguni. ***

Injili

 

Katika siku kama ya leo miaka 1439 iliyopita yaani tarehe 12 Ramadhani mwaka wa Kwanza Hijria, muda mfupi baada ya Mtume Mtukufu Muhammad (SAW) kuhamia Madina akitokea Makka, aliunga udugu baina ya Muhajirina na Ansar. Muhajirina ni watu ambao walihama na Mtume (SAW) kutoka Makka kwenda Madina na Ansar ni Waislamu wa mjini Madina waliowakaribisha na kuwanusuru Muhajirina katika mji huo. Kwenye sherehe hiyo ya kuunga udugu wa Waislamu, Mtume (SAW) alimtangaza Ali bin Abi Talib (AS) kuwa ndugu yake hapa duniani na Akhera. ***

Mkataba wa kuunga udugu

 

Miaka 843 iliyopita katika siku kama ya leo ya Ramadhani 12 mwaka ,  alifariki dunia Ibn al-Jawzi, faqihi na mtaalamu mkubwa wa hadithi katika karne ya 6 Hijria. Ibn al-Jawzi alizaliwa mwaka 510 Hijria na kufanya safari nyingi kwa ajili ya masomo. Mbali na kubobea katika masuala ya elimu ya fiq'hi na hadithi, alikuwa mtaalamu katika uwanja wa kutoa mawaidha na hata akaweza kuaminiwa na maulamaa wakubwa wa zama zake. Mwanazuoni huyo ameandika vitabu vingi na mashuhuri zaidi ni Al Muntadhim na Mawaidhul Muluk. ***

Ibn al-Jawzi

 

Siku kama ya leo miaka 215 iliyopita, yaani tarehe 18 Mei mwaka 1804 Miladia, Bunge la Seneti la Ufaransa lilipasisha uamuzi wa kumtangaza Napoleone Bonaparte kuwa mfalme wa Ufaransa na kwa utaratibu huo kwa mara nyingine tena utawala wa kifalme ukatawala nchini humo kwa miaka 15. Hata hivyo, mfumo wa kifalme ulifikia mwisho miaka kumi baadaye, sawa na tarehe 11 Aprili mwaka 1814, baada ya Napoleone Bonaparte kushindwa katika vita vyake na nchi za Ulaya na kubaidishwa. ***

Napoleone Bonaparte

 

Katika siku kama ya leo miaka 189 iliyopita, jeshi la Ufaransa lilianzisha operesheni ya kuikalia kwa mabavu Algeria. Kisingizio cha Charles wa Kumi mfalme dikteta wa wakati huo wa Ufaransa cha kutoa amri ya kufanywa mashambulio hayo, ilikuwa sababu ya hujuma hiyo kufuatia vitisho vilivyokuwa vimetolewa miaka mitatu kabla na mtawala wa wakati huo wa Algeria akiitaka Ufaransa ilipe deni la nchi hiyo la Franc milioni saba. Hata hivyo, kinyume na ilivyodhania Paris, wananchi wa Algeria walisimama kidete katika kukabiliana na mashambulio hayo. Ijapokuwa Ufaransa ilifanikiwa kuikalia kwa mabavu Algeria na kupora maliasili na utajiri wa nchi hiyo, lakini hatimaye nchi hiyo ya Kiafrika ilijipatia uhuru wake mwaka 1962. ***

Bendera ya Algeria

 

Siku kama ya leo miaka 147 iliyopita, alizaliwa Bertrand Russell mwanafalsafa na mwanahesabati mashuhuri wa Uingereza. Russell baada ya kumaliza masomo yake ya awali alijiunga na Chuo Kikuu cha Cambridge mjini London. Russell alikuwa mpinzani mkubwa wa Vita vya Kwanza na vya Pili vya Dunia, pamoja na vita vya Marekani dhidi ya Vietnam, na hata kufikia hatua ya kufungua mashtaka dhidi ya viongozi wa Marekani, mashtaka yaliyopewa jina lake la Russell. Msomi huyo alifanikiwa kupokea tuzo ya fasihi ya Nobel mwaka 1950. Russell alifariki dunia mnamo mwaka 1970. ***

Bertrand Russell

 

Miaka 45 iliyopita katika siku kama ya leo, nchi ya India ilifanya jaribio la kwanza la nyuklia katika jangwa la Rajasthan magharibi mwa nchi hiyo na jirani na mpaka wake na Pakistan. Kwa utaratibu huo, India nayo ikawa nchi ya sita baada ya Marekani, Umoja wa Kisovieti, Ufaransa, Uingereza na China katika uwanja huo wa nyuklia. Miaka 24 baadaye yaani mwaka 1998 India ilifanya majaribio mengine matano ya nyuklia na kufanikiwa kutengeneza silaha za atomiki. ***

Jaribio la nyuklia

 

Na katika siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, kwa mujibu wa azimio la Mkutano wa Kumi na Mbili wa Baraza Kuu la Kamati ya Kimataifa ya Makumbusho, siku hii iliainishwa na kutangazwa kuwa "Siku ya Makumbusho Duniani." Moja ya malengo muhimu ya baraza hilo lilikuwa ni kupanuliwa makumbusho katika kona mbalimbali duniani, kuweko ushirikiano wa kila upande wa majumba ya makumbusho ulimwenguni kwa shabaha ya kufikia malengo ya kiutamaduni na wakati huo huo kuzuia kuangamizwa athari za kale za kiutamaduni. Ni vyema kuashiria hapa kwamba, lengo  la kuanzishwa sehemu kwa jina la makumbusho ni kuhifadhi athari za kale za vizazi vilivyopita kwa ajili ya vizazi vijavyo. ***

Siku ya Kimataifa ya Makumbusho