Jumapili, tarehe 19 Mei, 2019
Leo ni Jumapili tarehe 13 Ramadhan mwaka 1440 Hijiria, inayosadifiana na tarehe 19 Mei mwaka 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1345 iliyopita yaani sawa na tarehe 13 Ramadhani mwaka 95 Hijria, alifariki dunia Hajjaj bin Yussuf Thaqafi, liwali katili na dhalimu katika kipindi cha utawala wa Bani Umayyah. Hajjaj bin Yussuf Thaqafi aliishi katika kipindi cha Abdul Malik Marwan na Hisham bin Marwan, na alikuwa mashuhuri kwa kuwatesa na kuwauwa wapinzani wa utawala wa Bani Umayyah, hasa wafuasi wa Imam Ali bin Abi Talib AS na watu wa familia ya Mtume Mtukufu Muhammad SAW. Baadhi ya wanahistoria wameandika kuwa, zaidi ya watu 120,000 waliuawa kutokana na amri iliyotolewa moja kwa moja na Hajjaj bin Yussuf Thaqafi. Miongoni mwa jinai zilizowahi kufanywa na Hajjaj Thaqafi ni pamoja na kushambulia mji mtakatifu wa Makka na kuharibu al Kaaba katika mwaka 74 Hijria.
Siku kama ya leo miaka Miaka 498 iliyopita, majeshi ya utawala wa kifalme wa Othmania yaliuteka mji muhimu wa Belgrade, uliokuwa mji mkuu wa Yugoslavia ya zamani. Mwishoni mwa karne ya 14 Miladia Utawala wa Othmania ulianza kusonga mbele katika eneo la Balkan na kuweza kulitawala karibu eneo lote hilo. Miaka 20 baadaye yaani mwaka 1541 utawala huo uliweza pia kuyadhibiti maeneo ya Hungary.
Siku kama ya leo miaka 257 iliyopita, alizaliwa katika familia masikini Johann Gottlieb Fichte mwanafalsafa wa Kijerumani. Johann alikuwa mmoja wa waasisi wakuu wa harakati ya kifalsafa iliyojulikana kama "German Idealism", harakati ambayo ilitokana na maandiko ya kinadharia na kimaadili ya rafiki yake Immanuel Kant. Johann Gottlieb Fitche aliathiriwa sana kinadharia na mwanafalsafa mwenzake huyo na kumkabidhi baadhi ya kazi zake. Johann Fitche ameandika vitabu vingi muhimu ambapo baadhi ni vile alivyovipa majina kama vile" Foundations of Nature Right, Mustakabali wa Binadamu na makala ya The Way Towards the Blessed Life.
Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita alifariki dunia Mirza Jahangir Khan Ghashghaei, faqihi na mtaalamu wa Irfan wa nchini Iran. Alizaliwa eneo la Ghashghaei katikati mwa Iran na kuanza kujifundisha elimu na maarifa ya Kiislamu ambapo aliinukia kielimu. Baadaye Mirza Jahangir Khan Ghashghaei alielekea mjini Isfahan moja ya miji mikubwa ya Iran na kujishughulisha na kazi ya kulea wanafunzi ambapo alichukua karibu miaka 50 kwenye kazi hiyo. Miongoni mwa wanafunzi wake mashuhuri alikuwa ni Ayatullah Mudarres na Ayatullah Borujerdi. Alifariki dunia akiawa na umri wa miaka 85 na kuzikwa mjini Isfahani.
Siku kama ya leo miaka 94 iliyopita, alizaliwa Malcolm X, kiongozi wa harakati za kupigania uhuru Wamarekani wenye asili ya Afrika. Malcolm X alizaliwa katika familia masikitini nchini humo na akiwa na umri wa miaka minne, alishuhudia kijiji chao kikiteketezwa moto na watu wa jamii ya Ku Klux Klan kutokana na mashambulizi ya kibaguzi. Baadaye alienda kujiunga na shule ya kutwa hata hivyo akiwa na umri wa miaka 15 hakuweza kukamilisha masomo yake kutokana na umasikini, hivyo akalazimika kufanya kazi katika mgahawa mmoja ambapo alijikuta akijiunga na utumiaji wa madawa ya kulevya na unyang’anyi. Kufuatia hali hiyo akiwa na umri wa miaka 21 alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela kutokana na hali hiyo. Akiwa jela alifahamiana na wafungwa wengi wenye asili ya Kiafrika waliotokana na familia za Kiislamu kama ambavyo pia alikuwa na mahusiano na Elijah Muhammad, kiongozi wa harakati ya siri ya Wamarekani weusi. Mahusiano na kiongozi huyo yaliendelea hata baada ya Malcolm X kutoka jela. Baada ya hapo alianza kusoma na kufanya utafiti mwingi kuhusiana na Uislamu ambapo kwa msaada wa Waislamu alifanikiwa kujenga misikiti miwili katika mji wa Detroit, Philadelphia nchini Marekani.
Siku kama ya leo miaka 84 iliyopita, Thomas Edward Lawrence mwanasiasa na afisa wa ujasusi wa Uingereza alifariki dunia katika ajali ya gari. Lawrence alizaliwa mwaka 1888 Miladia. Katika kipindi cha miaka kati ya 1910 hadi 1914, mwanasiasa huyo wa Uingereza aliwakilisha kamati ya masuala ya akiolojia (elimu kale) na pia kuhudumu huko Iraq, Syria na Palestina. Aidha alikuwa mfanyakazi wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza na mwaka 1916 aliteuliwa kuwa mkuu wa idara ya ujasusi ya jeshi la Uingereza nchini Misri. Thomas Edward Lawrence alichangia pakubwa kuingia madarakani kwa wafalme Fadhil huko Syria, Abdallah nchini Jordan na Mfalme Abdulaziz huko Saudi Arabia.
Na siku kama ya leo miaka 83 iliyopita, rada ilivumbuliwa na Robert Watson Watt mvumbuzi wa Kiingereza. Kifaa hicho ambacho ni muhimu kinachotumiwa katika ugunduzi na utambuzi kwenye oparesheni mbalimbali za kijeshi na kiraia, kwa mara ya kwanza kilitumika katika moja ya viwanja vya ndege vya Uingereza. Rada ilihesabiwa kama chombo muhimu cha kutoa tahadhari katika Vita vya Pili vya Dunia na hivi sasa kinatumika katika masuala mbalimbali.