May 21, 2019 00:14 UTC
  • Jumanne, tarehe 21 Mei, 2019

Leo ni Jumanne tarehe 15 ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka 1440 Hijria sawa na tarehe 21 Mei mwaka 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 2235 iliyopita yaani tarehe 21 Mei mwaka 216 Miladia jeshi la wapiganaji wa utawala wa Carthage chini ya uongozi wa (Hannibal) walitoa pigo kwa jeshi la Roma kaskazini mwa Italia. Hiyo ilikuwa vita vya pili vya Carthage, na Roma ilikuwa chini ya anuani ya " Vita vya Punik." Hannibal alikaribia kuisambaratisha kikamilifu Roma kwa kustafidi na tembo wa vitani na wapanda tembo wenye uzoefu hata hivyo kumalizika kwa chakula cha wanajeshi wa utawala wa Cartharge kuliwawafanya washindwe vita hivyo na kurudi nyuma. Jeshi la Roma liliikalia kwa mabavu ardh asili ya Carthage katika Tunisia ya sasa na kubomoa miji na kuwauwa kwa umati watu katika duru ya tatu na mwisho vita hivyo vya tawala mbili hizo za Mediterania. 

.

Hannibal

Miaka 1437 iliyopita katika siku inayosadifiana na hii ya leo, katika mwaka wa Tatu Hijria  alizaliwa Imam Hassan al-Mujtaba (as), mmoja wa Ahlul-Bait wa Bwana Mtume Muhammad SAW. Imam Hassan (as) alikulia na kupata malezi na usimamizi wa babu yake Bwana Mtume SAW, mama yake Bibi Fatimatul Zahra binti ya Mtume na baba yake, yaani Imam Ali (as). Baada ya kuuawa shahidi baba yake mwaka wa 40 Hijiria, mtukufu huyo alifanya kazi kubwa ya kusimamia na kuwaongoza Waislamu. Mwanzoni Waislamu wengi walimbai na kumpa mkono wa utiifu Imam Hassan, lakini mfumo wa utawala wa Bani Umayyah uliokuwa ukiongozwa na Muawiya mwana wa Abu Sufiyan ambao wakati huo ulikuwa na nguvu kubwa, ulianzisha uadui na chuki dhidi ya Imam huyo. Hatimaye Imam Hassan (as) alijiandaa kukabiliana na Bani Umayyah, lakini viongozi wengi wa jeshi lake walidanganyika na ahadi za uongo za maadui na kumuacha peke yake Imam, hali iliyomlazimisha mtukufu huyo kufanya suluhu na mtawala huyo wa Bani Umayyah kwa lengo la kuilinda na kuinusuru dini tukufu ya Uislamu.

Siku kama ya leo miaka 1057 iliyopita yaani tarehe 15 Ramadhani  mwaka wa 383 Hijria aliaga dunia katika mji wa Nishabur kaskazini mashariki mwa Iran Abubakar Muhammad bin Abbas "Kharazmi" aliyekuwa msomi na mwanafasihi mtajika wa Kiislamu. Kharazmi alikuwa hodari mno wa kubainisha mambo kwa ghibu na alikuwa na uwezo mkubwa wa kuhifadhi mashairi na historia ya Waarabu. Abubakar Muhammad bin Abbas Kharazmi ameacha athari iitwayo "Rasail" ambayo ni tunu kubwa katika fasihi ya Kiarabu na ambayo ni maarufu kwa jina la Rasail Kharazmi.

Abubakar Muhammad bin Abbas Kharazami

 

Miaka 28 iliyopita katika siku kama ya leo yaani tarehe 21 mwezi Mei mwaka 1991 aliuawa Rajiv Gandhi Waziri Mkuu wa zamani wa India. Gandhi alikuwa mwana wa Indra Gandhi Waziri Mkuu wa zamani wa India. Alizaliwa Agosti 20 mwaka 1944 huko Mumbai (Bombay inatamkwa) na kukulia nyumbani kwa babu yake Jawaharlal Nehru waziri Mkuu wa kwanza wa India. Baadaye Rajiv Gandhi alipata masomo katika Chuo Kiku cha Cambridge Uingereza na kisha alijiunga na Shirika la Ndege la India baada ya kuhitimu masomo ya urubani. Rajiv aliingia katika siasa baada ya kifo cha mdogo wake wa kiume ambaye alikuwa akimtaja kuwa mrithi wa Indira Gandhi. Rajiv alichaguliwa kuwa mbunge katika uchaguzi mdogo.  Mwaka 1983 Rajiv Gandhi aliteuliwa kuwa Katibu Mkuu wa chama cha Kongresi ambacho kilikuwa chama tawala na kukipanga upya. Rajiv alishindwa katika uchaguzi wa bunge la wawakilishi  na mwaka 1989 alijiuzulu  baada ya kuwa Waziri Mkuu wa India kwa miaka 5. Rajiv Gandhi alikuwa na nia ya kushiriki katika uchaguzi huo wa bunge la India hata hivyo tarehe 21 Mei mwaka 1991 akiwa na umri wa miaka 47 aliuawa katika mlipuko wa bomu uliotokea katika mkutano wa kampeni za uchaguzi kusini mwa India.  

Rajiv Gandhi, Waziri Mkuu wa zamani wa India