Jumapili, tarehe 9 Juni, 2019
Leo ni Jumapili tarehe 5 Shawwal 1440 Hijiria, sawa na tarehe 9 Juni 2019 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 1951 iliyopita Nero, mfalme katili na mmwagaji damu wa Roma alijiua akiwa na umri wa miaka 31 na baada ya kutawala kwa miaka 14. Inasemekana kuwa Claudius wa Kwanza wa Roma alimchukua Nero na kumfanya mwanaye. Hata hivyo Nero alimuua kwa sumu na baadaye kuchukua nafasi yake ya ufalme. Katika kipindi chote cha utawala wake, Nero aliweza kuwaua ndugu na jamaa zake akiwemo mama, mke na kaka yake. Mfalme huyo katili wa Roma alifanya mauaji makubwa dhidi ya wananchi sambamba na kuwauwa kwa halaiki Wakristo na pia kuuchoma moto mji huo wa Roma. Kwa sababu hiyo kulijitokeza harakati za uasi dhidi yake. Mtawala huyo katili na dhalimu aliamua kujinyonga baada ya kuona harakati za mwisho za uasi dhidi yake zinakaribia kupata ushindi.
Siku kama ya leo miaka 1380 iliyopita yaani sawa tarehe 5 Shawwal mwaka 60 Hijria, Muslim bin Aqil, binamu wa Imam Hussein (as) aliwasili katika mji wa Kufa moja ya miji ya Iraq, kwa shabaha ya kuwalingania wenyeji wa mji huo kwenye njia ya haki na kuchukua baia ya Imam Hussein. Kabla ya hapo watu wa Kufa walikuwa wamemwandikia barua nyingi Imam Hussein (as) wakimuomba aende kwenye mji huo na awaongoze kwenye harakati dhidi ya utawala wa kidikteta wa Bani Umayyah. Baada tu ya Muslim bin Aqil kuwasili katika mji wa Kufa aliwasomea wenyeji wa mji huo barua ya Imam Hussein (as) iliyowakaribisha kujiunga na harakati ya kiongozi huyo. Mwanzoni watu wa mji wa Kufa walikubali ujumbe wa Imam Hussein lakini baadaye walikengeuka. Mwishowe watu hao walimuacha peke yake Muslim bin Aqil na mjumbe huyo wa Imam Hussein akauawa shahidi na askari wa utawala wa Bani Umayyah.
Siku kama ya leo miaka 245 iliyopita alizaliwa Joseph von Hammer, mtaalamu wa masuala ya mashariki ya duni wa Austria. Baada ya kujifunza lugha za Kiarabu, Kifarsi na Kituruki aliteuliwa na serikali ya Austria kuwa mfasiri wa ubalozi wa serikali hiyo katika utawala wa Othmania. Ni katika wakati huo ndipo Joseph von Hammer akatumia fursa iliyojitokeza kwa ajili ya kufuatilia masuala ya utamaduni ya nchi za Iran, Russia, Syria, Lebanon na Misri, kama ambavyo pia alijifunza mafunzo ya dini ya Kiislamu. Kutokana na juhudi zake kubwa za kutambua tamadunia za nchi za Mashariki, alitunukiwa zawadi mbalimbali barani Ulaya. Baadhi ya sentesi na maandishi yake yanaonyesha kwamba Hammer alijiunga na dini ya Uislamu ambapo hata jiwe alilolichonga mwenyewe kwa ajili ya kuwekwa juu ya kaburi lake liliandikwa aya kadhaa za Qur'ani Tukufu. Miongoni mwa athari muhimu za Joseph von Hammer ni pamoja na kitabu cha 'Historia ya utawala wa Othmania' 'Picha za watawala Waislamu' na 'Historia ya Malenga wa Othmania.' Joseph von Hammer alifariki dunia mwaka 1856 Miladia.
Siku kama ya leo miaka 134 iliyopita majeshi ya Ujerumani yaliivamia nchi ya Magharibi mwa Afrika ya Togo. Katika kipindi hicho mwambao wa nchi hiyo ulikuwa umegeuzwa na watu wa Ulaya kuwa eneo muhimu la biashara. Nchi ya Togo iliendelea kuwa chini ya wakoloni wa Ujerumani, hadi kipindi cha Vita vya Kwanza vya Dunia. Baada ya Wajerumani kuondoka nchini Togo, Ufaransa na Uingereza ziliikalia tena kwa mabavu nchi hiyo. Hatimaye mwaka 1960 Togo iliweza kujipatia uhuru wake.
Siku kama ya leo miaka 57 iliyopita moto mkubwa ulitokea katika Chuo Kikuu cha Algiers mji mkuu wa Algeria. Moto huo ulichoma zaidi ya nakala laki tano za vitabu vyenye thamani kubwa zilizokuwa kwenye maktaba ya chuo hicho. Asilimia kubwa ya vitabu vilivyoungua vilikuwa miongoni mwa marejeo muhimu na nadra. Chuo Kikuu cha Algiers na maktaba yake vilichomwa moto na jeshi la siri la Ufaransa nchini Algeria. Jeshi hilo la siri liliundwa na askari wa Ufaransa waliokuwa wakipinga suala la kupewa uhuru Algeria. Moto huo ulikuwa miongoni mwa makumi ya mioto kadhaa iliyotokea katika siku hiyo nchini Algeria na mingi ilisaabishwa na jeshi la siri la Ufaransa.
Siku kama ya leo miaka 51 iliyopita, alifariki dunia Ayatullah Sayyid Muhammad Hassan Ilahi Tabatabai, mmoja wa maulamaa na wataalamu wa elimu ya irfani. Sayyid Muhammad Tabatabai alizaliwa mjini Tabrizi kaskazini mwa Iran, mwaka 1325 Hijiria. Akiwa na miaka 19 alielekea mjini Najaf, Iraq akiwa na kaka yake mkubwa Allamah Muhammad Hassein Tabatabai na kupata kusoma elimu ya dini mjini hapo. Baada ya kutabahari katika elimu ya Kiislamu alirejea eneo alikozaliwa la Tabriz na kujishughulisha na kuwalea wanafunzi.