Jun 23, 2019 18:11 UTC
  • Maktaba ya Imam Khomeini (MA) na sauti-19

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 19 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Katika kipindi kilichopita tuliendelea kufafanua nafasi ya vyama na makundi ya kisiasa katika mtazamo wa Imam Khomeini (MA) ndani ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambapo tumekuwa tukielezea misimamo ya mtukufu huyo katika uwanja huo. Leo pia tutaendelea kubainisha suala hilo hivyo kuweni pamoja nami hadi mwisho wa kipindi hiki. 

Imam Khomeini (MA) sambamba na kukubali msingi wa uhuru na shughuli za vyama na mirengo ya kisiasa na kadhalika juhudi zake za kuzifanya shughuli hizo kuwa rasmi na za kisheria katika mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, alitoa pendekezo la kuundwa mirengo miwili ya chama cha 'Hizbullah' na 'Hizbu Mustadh'afiina' yaani chama cha wanyonge. Akibainisha nini maana ya chama cha Hizbullah na kuenea chama hicho kati ya wananchi wote wa Iran sambamba na kujibu swali hili kwamba, je, ni chama au kundi gani la kisiasa analoliona kuwa karibu zaidi alisema: "Nara na matakwa ya mwamko wa Kiislamu nchini Iran ni yenye kukubalika kwa kiasi kikubwa kwa kadiri kwamba hakuna mrengo unaoweza kupinga nara hiyo na hata kama utaipinga basi hautokuwa na nafasi kati ya wananchi. Mwamko wa taifa la Iran umevunja mipaka na mirengo ya kichama na kisha kuja na chama kimoja nacho ni chama cha wananchi Waislamu wa Iran, yaani chama cha Kiislamu na chama cha Mwenyezi Mungu." Hotuba ya tarehe 23/10/1357.

Wapalestina watu wanyonge duniani

 

Kadhalika mtukufu huyo alitoa pendekezo la kuundwa chama cha walionyongeshwa duniani 'Hizbu Mustazafiina al-Aalam' kinachowajumuisha Waislamu na wasiokuwa Waislamu ambapo katika kufafanua suala hilo alisema: "Ninatarajia kuona kukiundwa chama chenye jina la watu walionyongeshwa kwa ajili ya dunia yote ambapo watu wote wanyonge wataweza kushiriki katika chama hicho na kutatua matatizo ambayo yamefunga njia ya wanyonge hao, kisha wasimame dhidi ya waporaji wa Mashariki na Magharibi. Na wasiruhusu mabeberu wa dunia kuwafanyia dhulma watu walionyongeshwa." Hotuba ya tarehe 26/5/1358.

********

Imam Khomeini (MA) aliitaja nadharia ya kuundwa chama cha Hizbullah na chama cha Watu Wanyonge katika fremu moja na inayokamilishana na kwamba mambo hayo ni yenye kufuatilia masuala katika viwango vitatu vya kitaifa, kieneo na kimataifa. Akiashiria tajriba ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran anasema: "Hivi sasa ambapo mrengo wa watu walionyongeshwa umepatikana katika miji ya Waislamu, hivyo suala hilo ni lazima lipanuke katika uga mpana zaidi kati ya watu wa matabaka yote ya historia ya wanadamu kwa jina la 'Chama cha Wanyonge' ambacho ndicho chama kile kile cha Hizbullah ambapo kwa irada ya Mwenyezi Mungu Mtukufu watu wanyonge ni lazima watawale dunia." Hotuba ya tarehe 26/5/1358.

Wapalestina wanaokandamizwa na kuuliwa kila uchao na askari katili wa Israel

 

Katika sehemu nyingine na kuhusiana na nafasi ya chama hicho katika ulimwengu wa Kiislamu alisema: "Nchi zote za Kiislamu zinatakiwa kujisahihisha kutokana na hatari ya makosa yaliyopita, ambapo zinatakiwa kujiunga na umoja wa Waislamu na muungano wa chama cha wanyonge dhidi ya mabeberu." Hotuba ya tarehe 26/5/1358. Mbali na hayo Imam Khomeini (MA) alikutaja kuundwa vyama vya Hizbullah na Chama cha Wanyonyonge kuwa kusikokiuka shughuli za vyama vya kisiasa katika uga wa kieneo na kitaifa na kuhusiana na hilo alisema: "Tulisema kwamba uwepo wa chama kwa jina la Wanyonge kwa ajili ya dunia yote hauna maana kwamba vyama vya kisiasa nchini Iran sio sahihi. Isije ikatokea vyama katika eneo vikatwaa nafasi ya vyama vingine vya maeneo. Na iwapo kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu Waislamu watafanikiwa kuunda chama kama hicho, yaani chama cha wanyonge, basi kitakuwa kimefanikiwa kushika nafasi muhimu. Lakini hiyo haina maana ya kufuta chama kingine katika eneo, bali katika maeneo hayo vyama vitakuwepo na kwa uhuru kamili." Hotuba ya tarehe 2/6/1358.

********

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu ya 19 ya mfululizo wa vipindi vinavyofafanua nadharia ya Imam Khomeini (MA), kuhusu Mapinduzi kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Katika mtazamo muhimu na kwa kutegemea tajriba ya kihistoria ya wananchi wa Iran na pia tajriba ya watu wa nchi nyingine, alielezea madhara ya mgawanyiko katika nchi ambapo aliwatahadharisha wananchi kuhusiana na makundi matatu nchini kujishughulisha na vyama na mirengo ya kisiasa kwa kusema: Kundi la kwanza ni majeshi, likiwemo Jeshi la Walinzi wa Mapinduzi ya Kiislamu (Sepah) na polisi. Pili ni maafisa usalama na wafanyakazi wote wa Wizara ya Intelejensia. Na tatu ni vyombo vya serikali. Alifafanua madhara makubwa ya majeshi kujishughulisha na makundi na vyama vya kisiasa huku akiamini kwamba kitendo hicho kinatoa pigo kubwa kwa majeshi hasa kwa kuwa majeshi hayo kazi yao kuu ni kulinda msingi wa mfumo na ardhi ya nchi. Imam alisema: "Kati ya mambo ambayo nayafahamu kwa majeshi, ni kutoingilia masuala ya kisiasa." Hotuba ya tarehe 4/12/1359.

Matunda ya fikra za Imam Khomeini za kuanzisha harakati zitakazowatetea Waislamu kutokana na njama chafu za Israel

 

Aidha katika sehemu nyingine anasema: "Viongozi wa jeshi na majeshi yote ni lazima wawe makini kwa kuwazuia askari  kujihusisha katika masuala ya kisiasa. Hatua ya jeshi kuingia katika masuala ya kisiasa ni sawa na kusambaratisha sifa ya jeshi hilo. Masuala ya kisiasa kwa jeshi ni mabaya zaidi kuliko hata matumizi ya madawa ya kulevya aina ya heroin, hii ni kwa kuwa heroin inamuangamiza mtu binafsi anayeitumia, na masuala ya kisiasa nayo yanaangamiza jeshi lote. Kwa kuwa mmeona namna ambavyo jambo hilo linavyoangamiza jeshi, hivyo mnatakiwa kutumia nguvu zote katika kulizuia jeshi kujihusisha na siasa." Hotuba ya tarehe 24/3/1360.

********

Umuhimu wa kutoingia majeshi katika shughuli za vyama kwa ajili ya kulinda uimara wa vyombo hivyo vya ulinzi na pia usalama wa vyama vya siasa, umekuwa mkubwa kiasi kwamba Imam Khomeini na kwa mara kadhaa alionya vyombo hivyo kutoingia katika uga huo. Katika uwanja huo Imam Khomeini alisisitiza kwamba hakuna tofauti yoyote kati ya makundi na mirengo ya kisiasa na kwamba majeshi hayatakiwi kujiunga na kundi lolote la kisiasa hata kama iwe tu ni kwa kuunga mkono. Kadhalika Imam aliwahutubia maafisa usalama na watumishi wa Wizara ya Intelejensia, na kuwataka kuchukua tahadhari ya kutojiunga na makundi na vyama vya siasa kwa kusema: "Watu wote wanaohudumu katika wizara hiyo hawatakiwi kuwa katika kundi au chama chochote….Kitendo hicho kinakinzana na majukumu yenu." Hotuba ya tarehe 9/12/1363.

 

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 19 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.