Jun 25, 2019 14:10 UTC

Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji na karibuni kutegea sikio sehemu ya 23 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomein (MA) ambacho kinakujieni kwa mnasaba wa miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran.

Katika kipindi kilichopita tuliendelea kuzungumzia mtazamo wa Imam Khomeini (MA) kuhusiana na nafasi athirifu ya wanawake katika kuwasaidia wanamapambano na askari wa Iran katika kipindi cha vita vya kulazimishwa vya miaka minane vilivyoanzishwa na utawala wa Baathi wa nchini Iraq chini ya Saddam. Leo pia tutaendelea kuzungumzia suala hilo, hivyo endelea kuwa nami hadi mwisho wa kipindi hiki. Ndugu wasikilizaji akiendelea kubainisha nafasi chanya ya uungaji mkono wa wanawake kwa serikali, Imam Khomeini (MA) alitaja misaada na wanawake kujitolea katika mali na fedha zao kuwa aina nyingine ya wanawake kuwa mstari wa mbele katika nyuga tofauti za kijamii kwa lengo la kufikiwa uadilifu wa kijamii nchini. Katika uwanja huo, Imam Khomeini anasema: “Dada zetu ambao wameshiriki katika mwamko wa Mapinduzi, thamani walizojitolea, ni zaidi ya thamani walizojitolea wanaume. Wakiwa katika pazia la iffa walitoka nje na vazi hilo wakapiga nara pamoja na wanaume na wakachangia kufikiwa ushindi. Na hivi sasa pia kwa kile walichokiandaa maishani kwa nia na malengo halisi kwa ajili ya watu masikini, ni chenye thamani kubwa kiasi kwamba hata kama watatoa mamilioni ya pesa, bado hawawezi kufikia thamani hiyo.” Hotuba yake mbele ya wanawake tarehe 27/2/1358.

Wanawake wa Iran walikuwa na mchango mkubwa katika harakati za mapinduzi ya Kiislamu

Kadhalika Imam Khomeini alizitaja juhudi za wanawake katika kuwaunga mkono watu wasiojiweza na wenye hali ngumu katika jamii kuwa ni jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu na kuhusu hilo alisema: “Katika kipindi chetu wanawake wamethibitisha kwamba, katika jihadi si tu kwamba wako pamoja na wanaume, bali wako mbele yao. Wanawake wa Iran pia wameshiriki jihadi kubwa ya kibinaadamu na pia jihadi ya kifedha. Katika kipindi cha Mwamko matabaka matakatifu ya wanawake yalikuwa msitari wa mbele na katika kujitolea kwa mali pia walikuwa msitari wa mbele. Wanawake walijitolea dhahabu na vito vyao vya thamani kwa ajili ya watu wasiojiweza. Msingi wa mambo hayo ulitokana na nia njema. Mwenyezi Mungu aliteremsha Aya kadhaa kwa ajili ya Amirul-Muuminina Ali Bin Abitwalib (as) kwa hatua yake na familia yake ya kutoa sadaka vipande kadhaa vya mkate. Aya hizo hazikushuka kutokana na vipande vya mkate tu, bali zilishuka kutokana na ikhlasi ya kile walichokifanya kwa ajili ya Mwenyezi Mungu.” Hotuba ya Imam Khomeini mbele ya wanawake tarehe 27/2/1358.

******

Kadhalika Imam Khomeini (MA) alipongeza kujitolea wanawake katika kulea watoto wao kishujaa na kuwaweka mstari wa mbele katika Mapinduzi na vita na kuitaja hatua hiyo kuwa ya kupongezwa na alama ya imani iliyofanikisha ushindi dhidi ya utaghuti kwa kusema: “Nguvu ya imani katika kujitolea muhanga na kutaka kufa shahidi ambako kumekuwa kukikaririwa na vijana, ambapo wanawake wanasema kuwa kijana wangu fulani amekufa shahidi, hivyo ninao vijana wengine wawili ambao nitawatoa waende kufa shahidi kama alivyofanya mwenzao, hisia hiyo ya kutamani shahada na kujitolea nafsi ambayo ilikuwa haijawahi kutokea kwa taifa lolote, ndio iliushinda utwaghuti. Hii ndio maana halisi ya imani.” Hotuba yake ya tarehe 4/7/1358.

Wanawake wa Iran katika juhudi zao za kujenga taifa

Aidha akizihutubia familia za mashahidi wa kikosi cha anga cha jeshi la Iran kutokana na msimamo wao wa kishujaa katika kipindi cha vita vya kujitetea kutakatifu, aliwapongeza kwa kusema: “Ninakushukuruni nyinyi wanawake watukufu ambao kwa uwazi na kwa moyo mlisimama upande wangu na kukabiliana kwa ushujaa na wapinzani wa mwamko katika njia ya kufikiwa nchi ya Kiislamu….Maneno yenu nyinyi wanawake watukufu yalikuwa yakionyesha uwepo wa msimamo thabiti (istiqama).  Kwa hakika ninatoa shukurani za dhati kwenu familia za mashahidi wa askari wa kikosi cha anga na mashahidi wengine ambao nao walikuwa na moyo huohuo wa kusimama dhidi ya njama za adui.” Hotuba yake ya tarehe 7/10/1359.

*********

Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu 23 ya mfululizo wa vipindi vinavyozungumzia kiini na kichochezi cha Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran chini ya usimamizi wa Imam Khomeini (MA), kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Baada ya hayo sasa tuzungumzie ushiriki wa kisiasa wa wanawake katika serikali ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Ndugu wasikilizaji kwa kuzingatia kuwa katika dunia ya leo suala la kutetewa haki za kisiasa na kijamii za wanawake ni jambo ambalo limeshika kasi katika nchi nyingi ambapo hata baadhi duru za uistikbari zimekuwa zikijitahidi kueneza propaganda dhidi ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu nchini Iran na waasisi wake kwa kudai kuwa eti haki za wanawake nchini hapa zinakiukwa, hivyo tumeonelea ni vyema kuashiria suala hili kwa kifupi sambamba na kuonyesha msimamo wa Imam Khomeini (MA) katika uwanja huo.

Wanawake wa Iran hawakandamizwi na badala yake wapo kila uwanja wa maendeleo

Akitoa radiamali yake kwa madai ya wale waliokuwa wakiamini kwamba Uislamu unakandamiza haki za wanawake, Imam Khomeini alisisitiza kwamba dini ya Uislamu ndiyo iliyotoa mwito wa kutetea haki za wanawake kwa kusema: “Uislamu una mtazamo maalumu kuhusu wanawake. Uislamu ulidhihiri wakati ambao katika bara Arabu mwanamke alikuwa amepoteza utambulisho wake. Uislamu uliwatukuza na kuwainua wanawake. Uislamu uliwaweka katika kiwango sawa wanawake na wanaume. Kwa hakika Uislamu umewapa wanawake uzingatiaji mkubwa kuliko wanaume.”Hotuba yake mbele ya wanawake tarehe 15/12/1357. Kadhalika Imam Khomeini (MA) akijibu shubuha iliyotolewa na baadhi ya watu waliodai kwamba Uislamu unawataka wanawake kukaa tu majumbani kwao sambamba na kuwazuia kwenda kusoma katika vyuo vikuu ndani ya mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu alisema: “Propaganda kwamba eti iwapo Uislamu utashika hatamu mathalan, utawalazimisha wanawake kukaa majumbani mwao na kuwafungia milango ili wasitoke nje, ni madai potofu ambayo yanatolewa dhidi ya dini ya Uislamu. Hata mwanzo wa Uislamu wanawake walikuwa katika majeshi, na walienda katika medani za vita, Uislamu haupingi vyuo vikuu, lakini unapinga ufisadi katika vyuo vikuu. Uislamu unapinga kubakia nyuma kwa vyuo vikuu kama ambavyo pia unapinga vyuo vikuu kuwa na mitazamo ya ukoloni; kwa hakika Uislamu haupingi chuo kikuu. Uislamu haupingi kwa namna yoyote ile mambo hayo na pia haumzuii yeyote kati yenu kustafidi na mambo hayo……Katika kipindi cha Mtume wa Uislamu (saw) wanawake hawakuwa na nafasi yoyote, lakini Uislamu ulikuja na kuwapa nafasi sawa na wanaume.” Hotuba yake ya tarehe 21/9/1357.

******

Kwa mtazamo wa Imam Khomeini (MA) wanawake wana nafasi muhimu katika jamii na serikali ya Kiislam ina jukumu la kuandaa mazingira yatakayowafanikisha waweze kufikia nafasi muhimu ya kibinaadamu katika jamii. Akijibu swali la baadhi ya waandishi wa habari wa kigeni ambao katika kipindi cha mwamko wa mapinduzi ya wananchi wa Iran walidai kwamba iwapo mfumo wa jamhuri ya Kiislamu ungeasisiwa, basi ingekuwa sababu ya kuwawekea vikwazo na mashinikizo wanawake katika nyuga tofauti za kisiasa na kijamii, Imam Khomeini alionyesha masikitiko makubwa juu ya madai hayo ambapo aliwatoa hofu wachambuzi na wataalamu wa masuala ya kisiasa kwamba mfumo wa Kiislamu haungeweka vikwazo hivyo vya kuzuia nafasi na ushiriki wa wanawake katika nyuga mbalimbali za kisiasa na kijamii nchini.

Wanawake wa Iran wanashiriki sekta tofauti za ujenzi wa taifa kwa uhuru

Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 23 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini. 

 

 

Tags