Maktaba ya Imam Khomeini (MA) na sauti-27
Ni matumaini yangu kuwa hamjambo wapenzi wasikilizaji popote pale mlipo wakati huu. Ninakukaribisheni tena kusikiliza kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini kinachokujieni kila wiki, siku na saa kama hii, kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran hii kiwa ni sehemu ya 27.
Katika kipindi kilichopita tulizungumzia shauri na usia za Imam kwa vijana, leo pia tutaendelea kufafanua suala hilo, hivyo endeleeni kuwa pamoja nami hadi mwisho wa kipindi hiki.
Ndugu wasikilizaji Imam Khomeini alisisitizia sana udharura wa kuishi vyema na marafiki wema ambao hawatomfanya mtu kumsahau Mwenyezi Mungu sambamba na kujiepusha kuishi au kuwafuata watu wasio wema hasa katika kipindi cha ujana kwa ajili ya kuilea na kuitakasa nafsi kwa kusema: “Katika usia wangu nikiwa ninakaribia kufariki dunia na nikiwa ninapumua pumzi zangu za mwisho, wewe ambaye unastafidi na neema za ujana ninakuusia kuchagua marafiki wema walioshikamana na umaanawi na wale ambao hawakutilii maanani kupenda dunia na mapambo yake wala hawavuki mpaka katika kujikusanyia mali kwa zaidi ya kiasi. Wale ambao vikao na sherehe zao hazichanganyiki na madhambi na wenye tabia njema, ambao athari njema ya kuishi nao imejaa kheri na kuwa mbali na ufisadi.” Hotuba yake ya tarehe 8/2/1361.
Aidha akiashiria nukta muhimu kwamba kifo hakimtambui mzee wala kijana na kwamba mwanadamu katika kila wakati anatakiwa kuwa amejiweka tayari kukikabili kifo kwa kujirekebisha na kuilea vyema nafsi yake hususan katika kipindi cha ujana anasema: “Ninazungumza na wewe mwanangu ambaye hivi sasa ni kijana. Ni lazima ufahamu kwamba vijana kufanya toba ni rahisi sana kwao na kujirekebisha na kujilea kwa ndani kunaweza kufanyika kwa haraka sana. Katika uzee kuna vishawishi vingi vya nafsi, kupenda vyeo, kupenda mali na kujiona mkubwa ambavyo ni vingi zaidi kuliko vinavyowakabili vijana. Roho ya vijana ni nyepesi na yenye kukubali kurekebika. Kwa kijana ni rahisi sana kujiepusha na shari ya nafsi inayoamrisha maovu na kushikamana na umaanawi. Vijana hawatakiwi kukumbwa na hadaa na vishawishi vya kinafsi na kishetani. Kifo kipo karibu kwa kijana na mzee. Ni kijana yupi anayeweza kujipa matumaini kwamba ataweza kufikia uzee? Na ni mtu gani ameepukika na ajali za kila siku? Ajali za kila siku zipo karibu sana kuwapata vijana. Mwanangu usipoteze fursa na jitahidi ujirekebishe ukiwa kijana.” Hotuba ya Imam tarehe 8/2/1361.
*********
Kama kwanza ndio unafungulia redio yako, kipindi kilicho hewani ni sehemu 27 ya mfululizo wa vipindi vinavyozungumzia nadharia na mitazamo ya Mwasisi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran yaani Imam Khomeini (MA), kinachokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.
Ndugu wasikilizaji Imam Khomeini sambamba na kukosoa njama za kuwahadaa kwa anasa vijana na kuwafanya wapuuze matukufu kulikofanywa na utawala wa Kitwaghuti wa Shah ambao badala ya kuimarisha ustawi na maendeleo nchini na pia kupambana na ufisadi na maovu ndani ya jamii, ulijikita katika kueneza anasa, Imam alisema kuwa moja ya malengo ya utawala huo lilikuwa ni kuwaharibu vijana. Imam Khomeini alisema: “Masuala ya tasnia ni huru katika Uislamu iwapo hayatafungamana na ufisadi wa kimaadili na heshima ya mwanadamu. Uislamu unapinga kila jambo ambalo liko kinyume na maslahi ya wananchi na badala yake unaunga mkono maslahi yote ya wananchi……Mipango yote waliyoiweka watawala kuanzia ya kiutamaduni na kiusanii na mipango mingine ya kikoloni, ilikuwa na lengo la kuwalaghai kwa ufisadi ili vijana wasiweze kuwa na uchungu na nchi yao.” Hotuba ya Imam tarehe 1/10/1357. Kadhalika Imam Khomeini alifahamu vyema njama za kuwaharibu vijana wa Iran katika kipindi cha utawala wa kitwaghuti kupitia njama zilizopandikizwa na wakoloni ambapo alisema kuwa lengo lao kuu lilikuwa ni kukitenga mbali kizazi cha vijana na mustakbali wa jamii na taifa lao.
Kuhusiana na suala hilo alisema: “Vituo hivi ambavyo wameviunda kwa ajili ya anasa za vijana, na maduka haya yanayouza vileo kwa ajili ya vijana, vyote hivyo ni mradi ambao malengo yake ni kuwaangamiza vijana katika masomo yao vyuoni kwa kuwafanya wasiweze kufuatilia masuala ya nchi yao. Ili kwamba kila kitendo mnachotaka kukifanya, basi muwe huru kukifanya, lakini msiweze kuwafuatilia wao (watawala).” Hotuba ya Imam hapo tarehe 21/1/1361. Katika sehemu nyingine mtukufu huyo alisema: “Redio, televisheni, magazeti na sinema ni miongoni mwa nyenzo za upotoshaji na kuwalewesha wananchi hususan kizazi cha vijana….. Ni filamu za televisheni zinazotengenezwa na Wamagharibi au Wamashariki ambazo zinalielekeza tabaka la vijana wa kike na kiume kwenye njia isiyo sahihi ya maisha na kuwafanya kuwa watu wasio na habari kuhusu uwezo na shakhsia zao…..” Usia wa Imam Khomeini (MA).
********
Ndugu wasikilizani Imam Khomeini aliwataja vijana wa Iran kuwa vijana waumini na wenye msimamo thabiti na wanamapambano dhidi ya njama haribifu za utawala wa kitwaghuti wa Shah na waungaji mkono wake wa kigeni. Ni kwa kuzingatia kuwa vijana wa nchi hii waliweza kushinda njozi za vibaraka wachafu wa ukoloni, ndipo utawala wa Shah ukaamua kuwawekea vishawishi vya anasa vijana hao. Akijibu barua ya wanafunzi wa vyuo vikuu vya jumuiya za Kiislamu na wanafunzi barani Ulaya Imam Khomeini alisema: “Ninapoona kwamba tabaka la vijana wenye ghera la wanafunzi wakongwe na wapya ndani na nje ya nchi pamoja matabaka ya wananchi watukufu Waislamu, wameushinda usingizi fofo unaotokana na njama za vibaraka wachafu wa wakoloni, na sasa wameamka na kuwa wenye fikra sahihi, ninahisi furaha na matumaini.” Mwisho wa kunukuu. Aidha aliwataja vijana na wanafunzi wa vyuo vikuu kuwa ni kundi moja linalounda jamii na hivyo akalitaka kundi hilo kufanya juhudi ya kuwaamsha wananchi kutoka kwenye usingizi wa kughafilika. Akiwahutubu wanafunzi wa vyuo vikuu wa jumuiya za Kiislamu na wanafunzi barani Ulaya Imam Khomeini alisema: “Ninakutakeni nyinyi vijana wenye fikra zenye mwanga kwamba, msikumbwe na mughafala wa usingizi huu wa kifo sambamba na kufichua uhaini na jinai zinazotekelezwa na wakoloni pamoja na vibaraka wao wasio na utamaduni.” Mwisho wa kunukuu.
Wapenzi wasikilizaji sehemu ya 27 ya kipindi hiki cha Katika Maktaba ya Imam Khomeini (MA) ambacho kimekujieni kwa mnasaba wa kutimia miaka 40 ya Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran na kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, inaishia hapa kwa leo. Mimi ni Sudi Jafar, kwaherini.