Jul 08, 2019 02:43 UTC
  • Jumatatu, tarehe 8 Julai, 2019

Leo ni tarehe 5 Dhilqaadi 1440 Hijria sawa na Julai 8 mwaka 2019.

 Tarehe 5 Dhilqaadi miaka 776 iliyopita aliaga dunia Radhiyuddin Ali bin Mussa bin Ja'far maarufu kwa jina la Ibn Twaus, faqihi, mpokezi wa hadithi na mwanazuoni mashuhuri wa Kiislamu katika eneo la Hillah nchini Iraq. Alipitisha kipindi cha utotoni katika mji huo na baadaye alihamia Baghdad ambako aliishi kwa kipindi cha karibu miaka 15. Ibn Twaus alipata umashuhuri mkubwa katika elimu na ucha-Mungu na ameandika vitabu vingi ambavyo ni marejeo ya taaluma za Kiislamu. Kitabu mashuhuri zaidi cha msomi huyo ni "al Luhuf" ambacho ndani yake anazungumzia matukio ya Siku ya Ashura na harakati ya Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib (as) katika medani ya Karbala na katika uwanja huo kitabu hicho hakina kifani.

Ibn Twaus

Miaka 63 iliyopita katika siku kama hii ya leo alifariki dunia mtaalamu, mwanafikra na mwandishi wa Kitaliano Giovanni Papini. Alizaliwa mwaka 1881 katika mji wa Florence nchini Italia. Giovanni alipitia kipindi kigumu cha utoto na ujana wake. Hata hivyo hamu kubwa ya masomo ilimpelekea kwenda katika maktaba za kijamii na kuzidisha elimu na taratibu alidhihirisha uwezo wake mkubwa katika taaluma ya fasihi. Msomi huyu ameandika vitabu vingi kama "A Man--Finished," "The Failure," na "Life of Christ,".

Katika siku kama ya leo miaka 34 iliyopita alifariki dunia Ayatullah Muhammad Mahdi Rabbani Amlashi aalimu na mujahidi wa Kiirani. Ayatullah Amlashi alizaliwa mwaka 1313 Hijria Shamsiya katika familia ya kidini katika mji mtukufu wa Qum na kuanza masomo ya kidini katika mji huo. Mwanazuoni huyo alipambana vilivyo kwa miaka mingi katika njia ya kuutetea Uislamu na kulinda thamani zake. Kama walivyokuwa viongozi na wafuasi wengine wa Imam Khomeini Mwenyezi Mungu amrehemu mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran, Ayatullah Rabbani Amlashi katika uhai wake hakuacha kufanya juhudi za kupambana dhidi ya utawala wa Shah licha ya kufungwa na kubaidishwa.

Ayatullah Muhammad Mahdi Rabbani Amlashi

Na siku kama ya leo miaka 25 iliyopita, alifariki dunia Kim Il-sung aliyekuwa Kiongozi na Katibu Mkuu wa Chama cha Kikomonisti wa Korea Kaskazini. Kim Il-sung alizaliwa mwaka 1912. Akiwa na cheo cha ukapteni jeshini alirejea kaskazini mwa nchi hiyo mwaka 1945 akiandamana na jeshi. Alipanda ngazi ya uongozi haraka na akachaguliwa kuwa kiongozi wa chama cha wakomunisti wa nchi hiyo. Mwaka 1948 wakati nchi hiyo ilipoasisiwa na kuwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Korea, Kim Il-sung alifikia cheo cha uwaziri mkuu. Katika vita vya Korea, Kim Il-sung aliteuliwa kuwa kamanda mkuu wa majeshi ya nchi hiyo na mwaka 1972 akawa rais wa taifa hilo.

Kim Il-sung