Jul 14, 2019 21:53 UTC
  • Jumatatu, Julai 15, 2019

Leo ni Jumatatu tarehe 12 Mfunguo Pili Dhulqaada 1440 Hijria sawa na Julai 15 mwaka 2019 Milaadia.

 Katika siku kama ya leo miaka 431 kulitokea vita vya Bahari ya Manche (English Channel) kati ya jeshi la majini la Uhispania maarufu kama Jeshi la majini lisiloshindwa na jeshi la majini la Uingereza. Katika vita hivyo meli kubwa 135 za kivita za Uhispania ziliishambulia Uingereza kwa shabaha ya kulipiza kisasi cha mauaji ya malkia Mary Stuart wa Scotland lakini kutokana na kimbunga kikali meli 85 za Uhispani zilizama majini na kikosi cha jeshi la majini kisichoshindwa cha Uhispania kikapata kipigo kikubwa. Tangu wakati huo nyota na umashuhuri wa kikosi hicho ukaanza kuzama.

Vita vya Bahari ya Manche (English Channel)

Tarehe 15 Julai miaka 115 iliyopita alifariki dunia Anton Chekhov aliyekuwa mwandishi mashuhuri wa riwaya na michezo ya kuigiza wa karne ya 19 nchini Russia. Chekhov pia alikuwa tatibu na alianzia zahanati ya kutoa matibabu ya bure kwa watu wasiojiweza ambako alitoa huduma hiyo yeye mwenyewe. Umahiri wa Anton Chekhov ulikuwa katika kuandika riwaya na visa vifupi. Falsafa yake ilijengeka juu ya msingi wa kuishi maisha ya chini na ya watu wa kawaida na daima alikuwa akisema: Kuhisi furaha na saada ni neema kubwa ya Mwenyezi Mungu. Aliamini kuwa iwapo mwanadamu ataongozwa vizuri katika kipindi cha ujana hapana shaka atakuwa na maisha mazuri na yasiyo na taabu. Ivanov", "The Seagull", "Uncle Vanya", "Three Sisters" na "The Cherry Orchard" ni miongoni mwa vitabu vya visa na michezo ya kuigiza vya mwandishi huyo mashuhuri. 

Anton Chekhov

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita inayosadifiana na tarehe 24 Tir 1318 Hijria Shamsia, alizaliwa Ayatullahil Ali Khamenei Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mji wa Mash'had ulioko kaskazini mashariki mwa Iran. Baada ya kumaliza masomo katika shule ya sekondari, alijikita zaidi katika masomo ya kidini kutoka kwa baba yake, na kupiga hatua kubwa ya kielimu katika kipindi kifupi. Ayatullah Khamenei alielekea mjini Qum kwa masomo ya juu ya kidini, na kupata fursa ya kunufaika na elimu kutoka kwa maulamaa wakubwa katika mji huo, kama vile Imam Khomeini MA, Ayatullahil Udhma Burujerdi na Allamah Tabatabai katika masomo ya fiqh, usulul na falsafa. Akiwa bado kijana, licha ya kuendelea na masomo, lakini alikuwa mstari wa mbele katika harakati za mapinduzi dhidi ya utawala wa kibaraka wa Shah hapa nchini, na mara kadhaa alitiwa mbaroni, kutumikia vifungo na hata kubaidishwa. Mara baada ya kufariki dunia Imam Khomeini (MA) mwaka 1368 Hijria Shamsia, Baraza la Wanachuoni linalomchagua Kiongozi Muadhamu, lilimchagua Ayatullah Khamenei wakati huo akiwa rais wa nchi, kuwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Ayatullah Sayyid Ali Husseini Khamenei

Ayatullah Sayyid Ali Husseini Khamenei alijiunga na harakati za Imam Khomein MA za kuupinga utawala wa kidikteta wa Shah katika kipindi cha ujana wake. Alieneza fikra za Imam Khomein na kufichua ufisadi wa viongozi wa wakati huo. Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikamatwa na kutiwa gerezani mara kadhaa. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alikuwa mwanachama wa Baraza la Mapinduzi na aliwahi kuchaguliwa kuwa mbunge na mwanachama wa Baraza la Wataalamu wanaomchagua Kiongozi Muadhamu. Vilevile alikuwa Rais wa Iran kwa awamuu mbili mfululizo na mwaka 1989 baada ya kuaga dunia Imam Khomeini MA, alichaguliwa na Baraza la Wataalamu kuwa Kiongozi Mkuu wa pili wa Jamhyuri ya Kiislamu ya Iran.

Miaka 75 iliyopita katika siku kama ya leo mwafaka na tarehe 15 Julai 1944, ndege za kivita za jeshi la anga la Marekani zilianzisha mashambulizi makubwa huko Japan wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Ndege za kivita za Marekani aina ya B-29 zilishiriki kwenye mashambulizi hayo kwa kurusha makombora katika maeneo mbalimbali ya nchi hiyo. Mashambulizi hayo yaliharibu viwanda zaidi ya elfu tatu vya Japan vikubwa kwa vidogo na kuuwa kwa umati makumi ya maelfu ya raia wa nchi hiyo.

Vita vya Pili vya Dunia

Siku kama ya leo miaka 61 iliyopita, Nuri Said Pasha Waziri Mkuu wa zamani wa Iraq aliuawa baada ya kujiri mapinduzi ya umwagaji damu. AlijIunga na jeshi la utawala wa Othmania akiwa na umri wa miaka 21 na kushiriki katika vita vya utawala wa Othmania na Bulgaria vilivyojiri mwaka 1912. Nuri Said Pasha sambamba na kuwa mwanajeshi, alianzisha harakati za kisiasa na alizingatiwa na Uingereza wakati wa malalamiko ya kisiasa dhidi ya utawala wa Othmania. Hatimaye mwaka 1930 akipata himaya ya Uingereza alichaguliwa kuwa waziri Mkuu wa Iraq.

Nuri Said Pasha

Katika siku kama ya leo miaka 51 iliyopita, yaani tarehe 24 Tir mwaka 1347 Hijria Shamsia, Ismail Balkhi mwanamapambano na mwanafikra wa Kiafghani alikufa shahidi mjini Kabul. Alizaliwa katika kijiji kimoja kaskazini mwa Afghanistan. Alianza kusoma kwa bidii masomo ya dini tangu akiwa mdogo na kipindi fulani alifanya safari nchini Iran na Iraq, lengo likiwa ni kujiendeleza zaidi kielimu katika masomo ya dini. Ismail Balkhi alikuwa akiendesha mapambano dhidi ya udikteta na daima alikuwa akiwashajiisha wananchi Waislamu wa Afghanistan kupambana na tawala dhalimu. Kutokana na harakati hizo, shahidi Balkhi alikuwa chini ya mashinikizo ya watawala wa wakati huo wa Afghanistan na kufungwa jela kwa miaka kadhaa.

Ismail Balkhi

Na siku kama hii ya leo miaka 9 iliopita, miripuko miwili ya kigaidi ilitokea katika mji wa Zahidan kusini mashariki mwa Iran na kuuwa watu 72 na kujeruhi wengine 169. Miripuko hiyo ilitokea mbele ya msikiti wa Zahidan wakati wa madhimisho ya kukumbuka siku ya kuzaliwa Imam Hussein AS. Kundi la kigaidi la Jundullah lilitangaza kuhusika na miripuko hiyo. Kundi hilo aidha limehusika katika oparesheni nyingi za kigaidi na kuuwa raia wengi wa Iran. Oparesheni ya kigaidi ya huko Zahidan ilifanywa mwezi mmoja baada ya kunyongwa Abdulmalik Rigi kiongozi wa zamani wa kundi la kigaidi linalojiita Jundullah, ambaye alitiwa mbaroni katika oparesheni moja ya kiusalama iliyofanywa na vikosi vya Iran. Baada ya kutiwa mbaroni, Abdul Malik Rigi, alikiri kuwa na uhusiano na Marekani. Magaidi watatu waliokuwa na ushawishi mkubwa katika kundi hilo walikamatwa na baadaye kunyongwa baada ya kutokea miripuko hiyo ya kuhuzunisha.

Gaidi aliyejilipua katika msikiti wa Zahidan, Iran