Jumatatu tarehe 22 Julai 2019
Leo ni Jumatatu tarehe 19 Dhulqaada 1440 Hijria sawa na tarehe 22 Julai 2019.
Siku kama ya leo miaka 406 iliyopita, Mikhail Ramanov alikalia kiti cha utawala wa Russia na kwa utaratibu huo, utawala wa miaka 304 wa familia ya Ramanov ukawa umeanza nchini humo. Miaka mitatu baada ya mashambulio ya vikosi vya Poland dhidi ya Russia, mmoja wa makamanda wa Kirusi alifanikwa kuvishinda vikosi hivyo na kuudhibiti mji wa Moscow. Baada ya jeshi la Poland kufukuzwa nchini humo, Mikhail Ramanov akashika hatamu za uongozi wa nchi hiyo. Katika kipindi cha utawala wa familia ya Ramanov, Russia ilipanuka lakini kwa upande wa uchumi haikupiga hatua kubwa.
Siku kama ya leo miaka 104 iliyopita, kulitokea vita vilivyojulikana kwa jina la Vita vya Isonzo. Vita hivyo vilitokea sambamba na kujiri Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. Vita vya Isonzo vilitokea katika maeneo ya milimani yaliyojulikana kwa jina hilo nchini Italia. Vita hivyo vilikuwa baina ya jeshi la Italia na Austria. Watu wapatao 70,000 wengi wao wakiwa ni Wataliano waliuliwa katika vita hivyo. Pamoja na hayo, jeshi la Italia lilipata ushindi dhidi ya jeshi la Austria.
Siku kama ya leo miaka 67 iliyopita, sawa na tarehe 31 Tir mwaka 1331 Hijria Shamsia, Mahakama ya Kimataifa ya The Hague Uholanzi, ilitoa hukumu ya kutupilia mbali mashtaka ya Uingereza dhidi ya Iran kuhusiana na kutaifishwa sekta ya mafuta ya Iran na kufanywa kuwa mali ya taifa. Bunge la Iran tarehe 29 Isfand mwaka 1329 Hijria Shamsia lillikuwa limeitangaza kutaifishwa sekta ya mafuta ya Iran na kwa utaratibu huo, likawa limekata mikono ya serikali ya Uingereza iliyokuwa ikinufaika na mafuta hayo. Uingereza ambayo ilikuwa ikipata faida kubwa kutokana na kupora utajiri wa mafuta wa Iran iliamua kuishtaki katika Mahakama ya The Hague. Hata hivyo katika siku kama ya leo, mahakama hiyo ilitupilia mbali mashataka hayo ya Uingereza.
Siku kama ya leo miaka 58 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 22 Julai 1961, yalianza mapigano makali kati ya majeshi ya Ufaransa na Tunisia, baada ya vikosi vya Ufaransa kuushambulia mji wa kihistoria wa Bizerte ulioko kaskazini mashariki mwa Tunisia. Mara baada ya Tunisia kujitawala kutoka kwa mkoloni Mfaransa mwaka 1956, mkoloni huyo aliendelea kuikalia kwa mabavu bandari ya Bizerte, na kuifanya kuwa kambi ya jeshi la anga la nchi hiyo. Hata hivyo majeshi ya Tunisia yalifanikiwa kuikomboa bandari hiyo kwenye mapigano hayo makali yaliyopelekea Watunisia 750 kuuawa.
Siku kama ya leo miaka 31 iliyopita, kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, jeshi la mtawala wa wakati huo wa Iraq, dikteta Saddam Hussein lilianza kufanya mashambulio makubwa dhidi ya maeneo ya kusini mwa Iran. Mashambulio hayo yalianza siku nne tu baada ya Iran kulikubali azimio nambari 598 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Azimio hilo lililokuwa limepasishwa takribani mwaka mmoja kabla, lilisisitiza juu ya usitishaji vita, kuuarifisha utawala wa Saddam kuwa utawala vamizi, likataka kulipwa fidia waathiriwa wa hujuma hiyo, kubadilishana mateka Iran na Iraq na kurejea vikosi vya nchi mbili hizo katika mipaka ya kimataifa. Utawala vamizi wa Iraq hapo kabla ulikuwa umelikubali azimio hilo na ulikuwa ukiendesha propaganda dhidi ya Iran kutokana na kutolikubali azimio hilo. Lakini wakati Iran ilipotangaza kulikubali, jeshi la dikteta Saddam kwa mara nyingine tena likaishambulia ardhi ya Iran.
Siku kama ya leo miaka 17 iliyopita, utawala wa Kizayuni wa Israel ukitumia ndege zake za kijeshi uliyashambulia maeneo ya Ukanda wa Gaza. Wapalestina 16 waliuawa shahidi katika mashambulio hayo ya kinyama yaliyofanywa usiku watu wakiwa wamelala. Salah Shahada kamanda wa Brigedi ya Izzu Diin Qassam Tawi la Kijeshi la Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina HAMAS alikuwa miongoni mwa watu waliouawa shahidi kufuatia mashambulio hayo. Aidha miongoni mwa waliouawa shahidi walikuwamo watoto wadogo 9. Kabla ya Salah Shahada kuuawa shahidi, mwanaharakati huyo aliwahi kukamatwa na utawala dhalimu wa Israel mara kadhaa na kutiwa jela.
Na siku kama ya leo miaka 16 iliyopita wana wa dikteta wa zamani wa Iraq Saddam Hussein, Uday na Qusay waliuawa katika maeneo ya Mosul kaskazini mwa Iraq. Baada ya Marekani na Uingereza kuivamia Iraq April 2003, Uday na Qusay pamoja na viongozi kadhaa wa utawala wa zamani wa nchi hiyo, waliukimbia mji mkuu wa Iraq, Baghdad. Kufuatia kufichuliwa na watu wao wa karibu nyumba walimokuwa, vikosi vya Marekani viliishambulia nyumba hiyo na kuwauwa. Uday aliyekuwa mtoto mkubwa wa Saddam na Qusay walikuwa wakishirikiana na baba yao kutekeleza mauaji dhidi ya raia wasio na hatia wa Iraq.