Larijani: Iran inaendelea kuunga mkono muqawama katika hali zote
(last modified Sat, 16 Nov 2024 04:50:20 GMT )
Nov 16, 2024 04:50 UTC
  • Larijani: Iran inaendelea kuunga mkono muqawama katika hali zote

Mshauri wa Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Seyyed Ali Khamenei amesisitiza kuwa, Iran inaendelea kuunga mkono kwa kila hali harakati za Muqawama au mapambano ya Kiislamu katika eneo.

Ali Larijani aliyasema hayo mbele ya waandishi wa habari katika mji mkuu wa Lebanon Beirut siku ya Ijumaa kufuatia mkutano wake na Spika wa Bunge la nchi hiyo Nabih Berri.

Katika kujibu swali kuhusu iwapo Jamhuri ya Kiislamu imekata tamaa kuunga mkono muqawama, Larijani amesisitiza kuwa Iran inaunga mkono muqawama kwa hali zote huku akibainisha kuwa safari yake ya Lebanon ilikuwa na lengo la kufikisha ujumbe huu.

Amesema Iran inaona ni jukumu lake kusaidia watu wa Lebanon na malengo yao,  huku akielezea matumiani kuwa hali nchini humo itaboreka haraka iwezekanavyo.

Spika huyo wa zamani wa bunge la Iran ametumai kuwa watu ambao wamefurushwa makwao kutokana na mashambulizi ya mara kwa mara ya Israel kusini mwa Lebanon wataweza kurejea katika makazi yao hivi karibuni.

Utawala wa Israel umeshadidisha mashambulizi yake makali dhidi ya Lebanon tangu Oktoba mwaka jana, na kuua zaidi ya watu 3,360 na kuharibu nyumba 100,000.

Larijani amesema ana imani kuwa Harakati ya Muqawama ya Hizbullah ya Lebanon ina uwezo wa wa kuilinda nchi, akisema, "Hizbullah ni harakati madhubuti. Taifa la Lebanon ni taifa imara pia".

Aidha Larijani amesema amemkabidhi Nabih Berri  ujumbe kutoka kwa Ayatollah Khamenei, lakini hakutoa maelezo zaidi kuhusu yaliyomo kwenye ujumbe huo.