Nigeria yaripoti vifo 15,000 vinavyohusiana na UKIMWI kila mwaka
(last modified Sat, 16 Nov 2024 02:53:39 GMT )
Nov 16, 2024 02:53 UTC
  • Nigeria yaripoti vifo 15,000 vinavyohusiana na UKIMWI kila mwaka

Nigeria inarekodi takriban vifo 15,000 vinavyohusiana na Ugonjwa wa Ukimwi kila mwaka licha ya juhudi za serikali za kukabiliana na kuenea ugonjwa huo hatari katika nchi hiyo yenye watu wengi zaidi barani Afrika.

Temitope Ilori, mkuu wa Shirika la Taifa la Kudhibiti Ukimwi nchini Nigeria (NACA) amewaambia waandishi wa habari wakati wa shughuli ya uhamasishaji huko Abeokuta, makao makuu ya jimbo la Ogun la kusini magharibi mwa Nigeria kwamba, zaidi ya kesi 22,000 mpya za Virusi vya Ukimwi (VVU) ambavyo hushambulia kinga ya mwili katika hatua ya awali ya UKIMWI, zimeripotiwa nchini humo tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi hivi sasa.

Akizungumzia kuongezeka kiwango cha maambukizi ya Ukimwi nchini Nigeria, Ilori amesema: "Takriban watoto 140,000 wenye umri wa kati ya miaka 0 hadi 14 wanaishi na VVU."

Afisa huyo amesema kuwa, Nigeria inaendelea kukabiliwa na changamoto kubwa katika kuzuia maambukizi ya ugonjwa huo kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto akilalamikia kupungua msaada wa kitaifa wa kuzuia kuenea ugonjwa huo wa kuambukiza.

Akitoa takwimu rasmi, Ilori amesema: Mwaka 2023 pekee, Nigeria ilirekodi maambukizi 75,000 mapya ya VVU na vifo 45,000 vinavyohusiana na VVU/UKIMWI.