Jul 26, 2019 23:45 UTC
  • Jumamosi, 27 Julai, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 24 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1440 Hijria mwafaka na tarehe 27 Julai 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1240 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, Imam Ridha (a.s) aliondoka mjini Madina na kuanza safari yake ya kuelekea Marw kaskazini mashariki mwa Iran ya kale. Imam Ridha alifanya safari hiyo kwa lazima na mashinikizo ya Maamun Khalifa wa Saba wa utawala wa Bani Abbas. Lengo la Maamun kutaka Imam Ridha apelekwe Marw lilikuwa kumfanya awe karibu na hivyo kudhibiti nyendo zake. Japokuwa kidhahiri Maamun alimfanya Imam kuwa mrithi wa kiti, cheo ambacho Imam Ridha alikikubali kwa kulazimishwa, lakini uhakika wa mambo ni kuwa alitaka kuimarisha misingi ya utawala wake. Imam Ridha aliendelea kuutambua utawala wa Maamun kwamba, si halali na alikuwa akifichua uovu na dhulma za utawala huo. Hatimaye Maamun alishindwa kuvumilia shakhsia ya kielimu na kimaanawi ya Imam pamoja na ushawishi wake kwa watu, hivyo akaamua kumpa sumu na kumuua shahidi. ***

Njia aliyopita Imam Ridha AS kutoka Madina hadi Marw

Miaka 247 iliyopita katika siku kama ya leo, ulitiwa saini mkataba wa kwanza wa kuigawa Poland kati ya madola matatu makubwa ya Ulaya katika karne ya 18. Poland ambayo hii leo ni moja ya nchi zilizo huru za mashariki mwa Ulaya, iligawanywa baina ya nchi tatu za Urusi, Austria na Prussia kwa kutiwa saini makubaliano yaliyotajwa. Ni muhimu kuashiria hapa kwamba hadi sasa Poland imeshawahi kugawanywa mara nne kati ya nchi tofauti. ***

Poland

Katika siku kama ya leo miaka 40 iliyopita,  mwafaka na tarehe 5 Mordad mwaka 1358 Hijria Shamsiya, Swala ya kwanza ya Ijumaa katika mji wa Tehran baada ya Mapinduzi ya Kiislamu ilisaliwa katika Chuo Kikuu cha Tehran ikiongozwa na marehemu Ayatullah Taleghani, mmoja wa maulamaa wakubwa wa Kiislamu, kufuatia agizo la Imam Ruhullah Khomeini, Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kabla ya Mapinduzi ya Kiislamu hapa nchini, Swala ya Ijumaa haikuwa ikifanyika kutokana na kuweko anga ya udhibiti na ukandamizaji wa serikali ya Shah. ***

Ayatullah Mahmoud Taleghani

Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, Muhammad Reza Pahlavi mfalme wa mwisho wa Iran aliaga dunia huko Cairo, Misri. Aliingia madarakani baada ya baba yake yaani Rezakhan kuondolewa kwenye uongozi na kubaidishwa na Waingereza. Kama alivyokuwa baba yake, Muhammad Reza Pahlavi alikuwa na uhusiano mkubwa na Uingereza na ndio maana akafanya jitihada za kulinda maslahi haramu ya nchi hiyo nchini Iran. Hata hivyo baada ya harakati za wananchi na kushinda harakati ya kuitaifisha sekta ya mafuta, maslahi ya Waingereza nchini Iran yalifikia tamati. Shah aliwakandamiza wananchi wa Iran kwa ngumi ya chuma na alikuwa kibaraka mkubwa wa Marekani. Suala hilo lilizidisha kasi ya harakati za Mapinduzi ya Kiislamu zilizoongozwa na hayati Imam Khomeini na mwaka 1357 Mapinduzi ya Kiislamu yalihitimisha utawala dhalimu wa Shah ambaye alikimbilia nje ya nchi na kufia Misri katika siku kama hii ya leo. ***

Muhammad Reza Pahlavi katika siku za mwisho za uhai wake

Na miaka 31 iliyopita katika siku kama ya leo, ilianza operesheni kubwa ya kijeshi iliyopewa jina la "Mirsad" huko magharibi mwa Iran kwa lengo la kuwasambaratisha vibaraka wa kundi la kigaidi la Munafiqin. Kundi la Munafiqin ambalo lilikuwa limekusanya magaidi katika mpaka wa Iran na Iraq wakiwa na silaha nzito kutoka kwa utawala wa zamani wa Baghdad lilianza kuishambulia ardhi ya Iran siku mbili kabla ya kuanza operesheni hiyo. Kiongozi wa Munafiqin alidhani kuwa magaidi hao wangeweza kuvuka barabara kuu za Iran bila ya kizuizi na tabu yoyote na kufika haraka mjini Tehran. Hata hivyo wanajeshi wa Iran wakishirikiana na wananchi waliojitolea katika operesheni hiyo ya Mirsad waliwazingira vibaraka hao wa Munafiqin huko magharibi mwa nchi na kuwasambaratisha magaidi hao walio na uhusiano mkubwa na nchi za kigeni. ***

Operesheni ya Mirsad