Jul 26, 2019 23:58 UTC
  • Alkhamisi, tarehe 25 Julai, 2019

Leo ni Alkhamisi tarehe 22 Dhulqaada 1440 Hijria sawa na tarehe 25 Julai mwaka 2019.

Miaka 904 iliyopita katika siku kama ya leo kazi ya kuandika tafsiri mashuhuri ya Majmaul Bayan ilimalizika. Kitabu hicho kiliandikwa na Sheikh Tabarsi mmoja wa wafasiri wakubwa wa Qur'ani Tukufu na miongoni mwa maulamaa mashuhuri wa Iran aliyekuwa mashuhuru kwa jina la Aminul Islam kutokana na uaminifu na uchamungu wake. Kitabu hicho ni miongoni mwa tafsiri mashuhuri za Qur'ani kutokana na mbinu yake ya kuvutia katika mtazamo wa fasihi. Tafsiri hiyo imechapishwa mara kadhaa katika nchi za Iran, Lebanon na Misri.

Tafsiri ya Qur'ani ya Majmaul Bayan

Miaka 125 iliyopita katika siku kama ya leo, vita kati ya Uchina na Japan vilianza kwa mashambulio yaliyofanywa na vikosi vya jeshi la Japan dhidi ya maeneo ya pwani ya Uchina. Vita hivyo vilitokea baada ya mashambulio yaliyofanywa na Japan kwa lengo la kuiteka ardhi kubwa ya Peninsula ya Korea na kaskazini mwa China. Japan ndiyo iliyoshinda katika vita hivyo kutokana na kujizatiti vyema kwa silaha za kisasa.

China na Japan

Tarehe 25 Julai mwaka 1938 yaani miaka 81 iliyopita, Wapalestina 62 wasio na hatia  waliuawa na mamia ya wengine kujeruhiwa katika milipuko miwili ya mabomu iliyotokea kwa nyakati tofauti katika soko la kuuzia mboga za majani huko Palestina. Makundi ya kigaidi ya Wazayuni ndiyo yaliyotega mabomu hayo mawili na lengo lao lilikuwa ni kuzusha hali ya machafuko na ukosefu wa amani kwa Wapalestina. 

Mlipuko wa bomu

Miaka 37 iliyopita katika siku kama ya leo mnamo tarehe 3 mwezi Mordad mwaka 1361 Hijria Shamsiya, alifariki dunia Dakta Hamid Inayat, mwandishi na mtarjumi mahiri wa Kiirani. Dakta Hamid alielekea nchini Uingereza baada ya kupata shahada ya chuo kikuu nchini Iran na akiwa huko alihitimu shahada ya udaktari katika taaluma ya uchumi na sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha London. Dakta Hamid Inayat baadaye alirudi Iran na kuanza kufundisha katika Chuo Kikuu cha Tehran. Dakta Inayat ameandika na kutarjumu vitabu vingi vya falsafa na fikra za kisiasa. Miongoni wma vitabu vya msomi huyo ni Uislamu na Usoshalisti na Fikra za Kisiasa za Magharibi.

Dakta Hamid Inayat

Na miaka 26 iliyopita katika siku kama ya leo, jeshi la utawala wa Kizayuni wa Israel kwa mara nyingine tena lilianzisha mashambulizi makubwa ya anga na baharini huko kusini mwa Lebanon. Mashambulizi hayo yalikuwa operesheni kali zaidi ya kijeshi kuwahi kufanywa na Wazayuni dhidi ya Lebanon baada ya mashambulio waliyoyafanya dhidi ya ardhi nzima ya Lebanon mwaka 1982.

Mashambulizi ya Israel kusini mwa Lebanon