Jul 27, 2019 23:43 UTC
  • Jumapili, tarehe 28 Julai, 2019

Leo ni Jumapili tarehe 25 Mfunguo Pili Dhul-Qaadah 1440 Hijria, mwafaka na tarehe 28 Julai 2019 Miladia.

Siku kama ya leo 1430 iliyopita Nabii Muhammad (saw) akiwa na masahaba na Waislamu zaidi ya laki moja aliondoka Madina na kuelekea mji wa Makka kwa ajili ya kuzuru Nyumba Tukufu ya Mwenyezi Mungu ya al Kaaba. Tangu alipohamia mjini Madina Mtume (saw) alielekea Makka mara tatu kwa ajili ya kuzuru al Kaaba, lakini ni mara mbili tu ndizo alizofanikiwa kutekeleza ibada ya Hija. Katika safari yake ya mwisho ya Hija mtukufu huyo aliwafunza Waislamu namna ya kutekeleza ibada hiyo kwa njia sahihi. Na wakati akirejea Madina Mtume Muhammad (saw) alifika katika eneo la Ghadir Khum na hapo akawakusanya masahaba zake na kwa amri ya Mola wake akamtangaza Imam Ali bin Abi Twalib (as) kuwa Khalifa na kiongozi wa Umma wa Kiislamu baada yake. Hiyo ilikuwa safari ya mwisho ya Hija ya Mtume ambayo ni maarufu kwa jina la Hijjatul Widaa. Miezi kadhaa baada ya safari hiyo Mtume Mtukufu aliaga dunia na kurejea kwa Mola wake.

Hijja ya kuaga

Siku kama ya leo miaka 290 iliyopita, harakati ya kwanza ya mapambano ya watumwa weusi wa Marekani ilianza huko kaskazini mwa nchi hiyo. Waanzilishi wa harakati hiyo ambao walikuwa watu 44 walimuua kila mzungu waliyekutana naye katika njia yao kutoka Carolina Kusini kuelekea Florida. Lakini walizingirwa na jeshi la Waingereza na kuuawa kabla ya kuingia Florida na kupata uhuru. Baada ya hapo watumwa weusi waliendeleza mapambano ya ukombozi na kupigania haki zao za kiraia. Watumwa weusi walikuwa wakitekwa nyara au kununuliwa kutoka Afrika tangu mwanzoni mwa karne ya 17 na kupelekwa Marekani kwa ajili ya kuuzwa na kufanyishwa kazi na mabwana zao. 

Mapambano ya watumwa weusi wa Amerika ya Kaskazini

Siku kama ya leo miaka 198 iliyopita, nchi ya Peru ilijipatia uhuru wake na siku hii hutambuliwa kuwa ni siku ya kitaifa nchini humo. Peru ilikuwa sehemu ya asili ya watu waliostaarabika wa Inca na tokea karne ya 12 hadi ya 16 ufalme wa watu hao ndio uliotawala kaskazini magharibi mwa Amerika ya Kusini. Mwanzoni mwa karne ya 16 wakoloni wa Uhispania waliingia Peru na baada ya mauaji ya kikatili dhidi ya Wahindi Wekundu hatimaye ardhi ya Peru ikatawaliwa na wakoloni wa Uhispania. Wahispania waliendelea kuikalia kwa mabavu ardhi hiyo sambamba na kupora mali na raslimali za watu wa Peru hali iliyopelekea kupamba moto mapinduzi ya wapigania uhuru nchini humo. Peru iko kaskazini magharibi mwa Amerika ya Kusini, huku ikipakana na nchi za Ecuador, Colombia, Chile, Brazil na Bolivia.

Bendera ya Peru

Siku kama ya leo miaka 141 iliyopita, ulitiwa saini mkataba wa kihistoria wa Barlin, mwishoni mwa kongamano lililofanyika mjini humo kati ya wajumbe wa nchi za Russia, Ujerumani, Ufaransa, Uingereza na Austria. Mkutano wa Berlin ulifanyika kwa ombi la kansela wa wakati huo wa Ujerumani Otto Von Bismarck. Kutiwa saini mkataba huo kuliifanya Ujerumani kuwa na satua ya kisiasa na kijeshi na kuandaa uwanja wa kujitanua zaidi nchi hiyo. Kimsingi kutiwa saini mkataba huo wa Berlin kulikuwa moja ya mambo yaliyoandaa uwanja wa kutokea Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. 

Kongamano la Berlin

Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita, wakati wa kukaribia kuanza Vita vya Kwanza vya Dunia, utawala wa kifalme wa Austria ulitangaza vita dhidi ya serikali ya Serbia kwa kisingizio cha kuuawa mrithi wa kiti cha ufalme wa nchi hiyo huko Serbia. Hata hivyo sababu kuu ya kutolewa tangazo hilo la vita ilikuwa ni upinzani wa wananchi wa Serbia dhidi ya uingiliaji wa Austria katika masuala ya ndani ya nchi yao na pia kufanyika uasi dhidi ya nchi hiyo.

Gavrilo Princip 

Siku kama ya leo miaka 43 iliyopita, tetemeko kubwa la ardhi liliukumba mji wa Tangshan mashariki mwa China. Tetemeko hilo ambalo lilikuwa na ukubwa wa 7.8 kwa kipimo rishta lilipelekea kuuawa watu wapatao laki sita na malaki kadhaa ya wengine kujeruhiwa sambamba na kuwa wakimbizi. Hata hivyo ripoti rasmi iliyotangazwa na viongozi wa China ilionyesha kuwa, idadi ya watu waliouawa katika tetemeko hilo ilikuwa laki mbili na 40 elfu. Hilo lilikuwa tetemeko kubwa zaidi kuwahi kuikumba China katika karne ya 20 na kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa tangu tetemeko la mwaka 1556 ambalo lilipelekea kuuawa kwa watu laki nane na elfu 30.

Mtetemeko wa ardhi

Na siku kama ya leo miaka 30 iliyopita, yaani sawa na tarehe 6 Mordad 1368 Hijria Shamsia, wananchi Waislamu wa Iran walishiriki kwenye kura ya maoni ambapo walipiga kura za ndio na kupasisha marekebisho yaliyofanywa katika katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Imam Khomeini (MA) aliagiza kufanyiwa marekebisho katiba ya Iran na kuundwa majlisi kwa ajili ya kutekeleza suala hilo muda mfupi kabla ya kufariki dunia. Miongoni mwa mabadiliko hayo, ni kuondoa sharti la Umarjaa kwa ajili ya kuchukua wadhifa wa uongozi wa juu nchini, kuongezwa nguvu za rais na kuondoa nafasi ya uwaziri mkuu.

Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran