Alkhamisi tarehe 15 Agosti mwaka 2019
Leo ni Alkhamisi tarehe 13 Dhulhija 1440 Hijria inayosadifiana na tarehe 15 Agosti mwaka 2019.
Katika siku kama ya leo miaka 102 iliyopita yaani tarehe 13 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1338 Hijria, alifariki dunia Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi, msomi mkubwa na mwanamapambano wa Iran. Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi ni mmoja wa maulama wakubwa wa Kishia na aliyepambika kwa elimu na uchaji-Mungu huko mjini Shirazi, moja ya miji ya Iran ya leo. Msomi huyo alipata umashuhuri kutokana na kuongoza mapinduzi ya Waislamu dhidi ya Uingereza. Baada ya Ayatullah Mirza Muhammad Taqi Hairi Shirazi kugundua kuwa Uingereza ilikuwa na lengo la kudhibiti nchi za Kiislamu kupitia pendekezo la kutaka kukubaliwa mwakilishi wa Londoni nchini Iraq kuwa rais wa nchi hiyo, alitoa fatuwa mashuhuri iliyopewa jina la fatwa ya kujilinda ambayo ilihalalisha mapambano ya silaha ya wananchi wa Iraq dhidi ya mkoloni Mwingereza. Fatwa hiyo iliitia hofu Uingereza ambayo ililazimika kuachana na mpango huo wa kikoloni.

Siku kama ya leo miaka 105 iliyopita, mfereji wa Panama ulifunguliwa rasmi kufuatia kupita meli ya kwanza katika kanali hiyo. Ujenzi wa kanali hiyo ulianzishwa na wahandisi wa Kifaransa na baadaye serikali ya Marekani ilinunua kampuni ya Ufaransa iliyokuwa ikijenga mfereji huo na kukamilisha ujenzi wake. Kujengwa mfereji huo wenye urefu wa zaidi ya kilomita 60 kuliunganisha bahari mbili za Pacifi na Atlantic.

Miaka 72 iliyopita India ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Muingereza, baada ya miaka mingi ya mapambano ya kupigania uhuru. India ina historia kongwe na watawala mbalimbali wa ndani na nje wamewahi kutawala nchini humo. Mapambano ya wananchi wa India dhidi ya mkoloni Muingereza yalipamba moto zaidi baada ya kuasisiwa Chama cha Congress ya Kitaifa na kujiunga na chama hicho Mahatma Gandhi.

Miaka 71 iliyopita, sawa na tarehe 15 Agosti 1948 nchi ya Korea ya Kusini iliundwa baada ya kujitokeza mgawanyiko wa visiwa vya Korea. Visiwa vya Korea vilikabiliwa na uvamizi na kukaliwa kwa mabavu wa madola yenye nguvu katika eneo hilo kama vile China na Japan tokea nusu ya kwanza ya karne ya ishirini.

Miaka 59 iliyopita katika siku kama hii ya leo nchi ya Jamhuri ya Congo Brazzaville ilipatia uhuru kutoka kwa mkoloni Mfaransa. Huko nyuma Congo Brazzaville ilikuwa sehemu ya ardhi ya Congo katika Afrika Magharibi iliyojumuisha Zaire ya zamani na Angola. Kongo Brazzaville iligunduliwa na Wareno katika karne ya 15 na baadaye ilikaliwa kwa mabavu na wakoloni wa Kifaransa kwa miaka kadhaa mfululizo. Kongo Brazaville iko magharibi mwa Afrika ikipakana na Jamhuri ya Afrika ya Kati, Cameroon, Gabon, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Angola.
Katika siku kama ya leo miaka 51 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria, alifariki dunia mwanazuoni mkubwa wa Kiislamu Allamah Agha Bozorge Tehrani. Alipata elimu ya msingi mjini Tehran na baadaye alielekea Najaf, Iraq kwa ajili ya elimu ya juu. Allamah Agha Bozorge Tehrani alikwea kwa kasi daraja za elimu na kuwa miongoni mwa wanazuoni wakubwa wa kidini. Allamah Tehrani alisafiri na kufanya uchunguzi katika maktaba nyingi za maeneo mengi kama Iran, Misri, Syria, Iraq, Hijaz, Palestina na kadhalika kwa ajili ya kutayarisha ensaiklopedia ya vitabu vya Kiislamu. Alifanikiwa kuandika tabu hilo kubwa lenye juzuu 26 ambalo alilipa jina la "Adhari'a ila Tasaanifish Shia". Kitabu kingine muhimu cha Allamah Agha Bozorge Tehrani ni "Tabaqatu Aalami Shia" chenye juzuu 8. Msomi huyo mkubwa wa Kiislamu alifariki dunia katika mji mtakatifu wa Najaf na kuzikwa katika maktaba yake kama alivyokuwa ameusia.

Miaka 29 iliyopita katika siku kama ya leo, inayosadifiana na tarehe 24 Mordad 1369 Hijria Shamsia, Saddam Hussein Rais wa zamani wa Iraq alimtumia barua Hujjatul Islam Walmuslimin Hashemi Rafsanjani aliyekuwa Rais wa Iran wakati huo, akimjulisha kwamba amekubali kikamilifu vipengee vya makubaliano ya mpaka yaliyotiwa saini 1975 nchini Algeria. Hata hivyo, tarehe 27 Shahrivar 1359 Hijria Shamsia, Saddam Hussein baada ya kushawishiwa na madola ya kibeberu ya Magharibi, alijitokeza kwenye televisheni ya Iraq na kuuchanachana mkataba huo, na baada ya siku chache, alianza kuivamia ardhi ya Iran. Saddam Hussein na waitifaki wake walidhani kwamba, muda mfupi tu baada ya kuivamia ardhi ya Iran wangeliweza kuuangusha mfumo mchanga wa Kiislamu hapa nchini. Hata hivyo kusimama kidete wananchi na mapambano ya wapiganaji shupavu wa Kiislamu wa Iran yalibatilisha njama zao na jeshi vamizi la Iraq likalazimika kurejea nje ya mipaka ya Iran baada ya kushindwa mtawalia.

Miaka 4 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 15 Agosti 2005 Miladia, utawala wa Kizayuni wa Israel ulilazimika kuondoka katika maeneo ya Ukanda wa Gaza, magharibi mwa Palestina inayokaliwa kwa mabavu. Eneo hilo lilikaliwa kwa mabavu na Wazayuni mwaka 1967, baada ya kutokea vita vya Waarabu na utawala wa Kizayuni wa Israel.
