Aug 20, 2019 22:11 UTC
  • Jumatano tarehe 21 Agosti 2019

Leo ni Jumatano tarehe 19 Dhulhija 1440 Hijria sawa na tarehe 21 Agosti mwaka 2019.

Siku kama ya leo yaani tarehe 30 Mordad katika kalenda ya mwaka wa Kiirani ni siku ya kumuenzi na kumkumbuka Allamah Muhammad Baqir Majlisi, mmoja kati ya maulamaa wakubwa wa Kiislamu. Baba yake Allamah Majlisi alipata elimu kwa msomi mkubwa wa Kiislamu Sheikh Bahai. Umahiri wa Sheikh Majlisi ulianza kuonekana akiwa bado kijana na alipata ijaza au ruhusa ya kunukuu hadithi kutoka kwa msomi na mwanafalsafa mashuhuri wa Kiislamu Mulla Sadra akiwa na umri wa miaka 14 tu. Allamah Majlisi ameandika vitabu vingi wakati wa uhai wake ambavyo hii leo ni marejeo ya Waislamu. Katika kipindi cha uhai wake Allamah Muhammad Baqir Majlisi alifanya hima kubwa kuhakikisha kuwa Swala za Ijumaa na jamaa zinatekelezwa. Vilevile alifanya juhudi za kuasisi shule za masomo ya kidini na kueneza hadithi za Mtume wa Muhammad (saw) na Ahlubaiti zake watoharifu. Idadi ya vitabu vilivyoandika na Allamah Muhammad Baqir Majlisi imetajwa kuwa zaidi ya 600 na umashuhuri zaidi ni kile kinachojulikana kwa jina la Biharul Anwar. Vitabu vingine mashuhuri vya msomi huyo ni Hayatul Quluub, Ainul Hayat na Zadul Maad.

Miaka 505 iliyopita katika siku kama ya leo, kulitokea mapigano ya kihistoria ya Chaldoran kati ya Iran na dola la Othmania katika eneo la bonde lililoko kati ya Tabriz na Khoui, kaskazini magharibi mwa Iran. Mapigano hayo yalikuwa kati ya wapiganaji wa Shah Ismail Safavi na vikosi vya jeshi la Sultan Salim Othmani.

Mapigano ya kihistoria ya Chaldoran

Siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, iliasisiwa The Central Treaty Organization ambayo ilikuwa ikijulikana kwa jina la Cento na kuchukua nafasi ya mkataba wa Baghdad. Taasisi hiyo iliundwa na Iran, Uturuki, Pakistan na Uingereza mjini Ankara Uturuki. Pamoja na kuwa Marekani haikuwa mwanachama rasmi wa Taasisi ya Cento na ilishiriki kwenye vikao vya jumuiya hiyo kama mtazamaji tu, lakini ilikuwa na nafasi kuu katika maamuzi yote ya taasisi hiyo. The Central Treaty Organization ilivunjika baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kujiondoa nchi hiyo katika mkataba huo mwaka 1979.

Makubaliano ya CENTO

Tarehe 21 Agosti mwaka 1965 yaani katika siku kama hii ya leo miaka 54 iliyopita Wamarekani wenye asili ya Afrika katika mji wa Alabama walifanya maandamano wakitaka kutekelezwa sheria ya haki ya kupiga kura. Maandamano hayo yalizidisha harakati ya vuguvugu la kupigania haki za kijamii za Wamarekani weusi. Harakati hiyo ilianza mwaka 1955 kwa lengo la kupigania usawa kati ya Wamarekani weusi na wazungu na ilimalizika mwaka 1968 baada ya kupasishwa sheria ya haki za kiraia.

harakati ya kupigania haki za kijamii za Wamarekani weusi

Siku kama ya leo miaka 50 iliyopita, inayosadifiana na 21 Agosti 1969 Miladia, Masjidul Aqsa Kibla cha Kwanza cha Waislamu, kilichomwa moto na Wazayuni. Katika tukio hilo, eneo hilo takatifu na la kihistoria liliharibika vibaya sana. Utawala wa Kizayuni wa Israel ulidai kuwa, kitendo hicho kilifanywa na mtalii wa Kiaustralia. Utawala huo wa Kizayuni ulitayarisha mahakama ya kimaonyesho tu mjini Tel Aviv na kuchukua uamuzi wa kumuachilia huru mhalifu huyo kwa madai kwamba alikuwa na matatizo ya kiakili. Baada ya kutokea kitendo hicho, nchi za Kiislamu zilikutana na kuamua kuunda Jumuiya ya Nchi za Kiislamu (OIC).

Masjidul Aqsa Kibla cha Kwanza cha Waislamu

Na miaka 28 iliyopita katika siku kama hii ya leo Latvia ambayo ni miongoni mwa nchi za Baltic huko magharibi mwa Urusi ya zamani ilijitangazia uhuru. Latvia ilikuwa chini ya satwa ya Urusi ya zamani kufuatia makubaliano ya siri yaliyofikiwa mwaka 1939 Miladia kati ya Hitler na Stalin. Mwaka 1991, karibu asilimia 80 ya wananchi wa Latvia walishiriki kwenye kura ya maoni na kupelekea kutangazwa uhuru wa nchi hiyo katika siku kama hii.