Aug 21, 2019 20:48 UTC
  • Alkhamisi, 22 Agosti, 2019

Leo ni Alkhamisi tarehe 20 Dhulhija 1440 Hijria sawa na Agosti 22 mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 1313 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa Imam Mussa al-Kadhim (AS) ambaye ni mmoja kati ya wajukuu watukufu wa Bwana wetu Muhammad (SAW). Alilewa na baba yake Imam Ja'afar bin Muhammad Swadiq (as) na kupata elimu na maarifa ya Kiislamu kutoka kwa mtukufu huyo kwa kipindi cha miaka 20. Baada ya kuuawa shahidi baba yake, Imam Kadhim (as) alishika hatamu za Uimamu na uongozi wa Umma wa Kiislamu kwa kipindi cha miaka 35 na kukabiliana na mashaka mengi. Imam Kadhim (as) alipitisha kipindi kikubwa cha umri wake katika kuwazindua na kuwaelimisha Waislamu maarifa asili ya dini. Suala hili liliwatia hofu kubwa watawala wa Bani Abbas ambao walimkamata na kumfunga jela ili kumuweka mbali na Waislamu waliokuwa na kiu ya maarifa halisi ya dini yao. Imam Kadhim (AS) alisifika kwa ukarimu mkubwa, uvumilivu na usamehevu. Tunatoa mkono wa baraka kwa Waislamu wote kwa mnasaba wa kuadhimisha siku hii muhimu ya kuzaliwa mtukufu huyo. 

Miaka 392 iliyopita katika siku kama ya leo, vilijiri vita vya mwisho vya La Rochelle kati ya Wakatoliki na Waprotestanti wa Ufaransa. Vita hivyo vilianza baada ya Waprotestanti kuchochewa na Uingereza. Wakatoliki ambao walikuwa wakiungwa mkono na vikosi vya jeshi la serikali ya Ufaransa chini ya uongozi wa Richelieu, Kansela mashuhuri wa nchi hiyo, walipigana vita na Waprotestanti ambao walikuwa wakipigania maeneo yao katika bandari ya La Rochelle. Vita hivyo vilimalizika baada ya mwaka mmoja kwa kupata ushindi Wakatoliki na kutekwa La Rochelle.

Vita vya mwisho vya La Rochelle

Katika siku kama ya leo miaka 321 iliyopita, mkataba wa pande tatu wa Russia, Poland na Denmark ulitiwa saini dhidi ya Sweden. Wafalme wa nchi hizo tatu walikuwa na lengo la kumuangusha Sharel XII mfalme kijana wa Sweden ili kuikalia kwa mabavu nchi hiyo. Ni kwa msingi huo ndipo miaka miwili baadaye mnamo mwezi Aprili mwaka 1700 Miladia nchi wanachama wa mkataba huo wa pande tatu zikaamua kuishambulia Sweden, hata hivyo jeshi la mfalme Sharel XII likakabiliana vilivyo na kutoa pigo kwa nchi vamizi.  Baada ya kufikia mapatano na Denmark, mwaka 1704 akaishambulia Poland na kuikalia kwa mabau. Hata hivyo mashambulio ya Sharel dhidi ya Russia hayakuzaa matunda. 

Sharel XII mfalme kijana wa Sweden

Siku kama ya leo miaka 159 iliyopita leo Paul Gottlieb Nipkow mmoja wa wavumbuzi wa televisheni alizaliwa huko Ujerumani. Nipkow alikulia katika familia maskini, lakini juhudi na irada kubwa ilimuwezesha kuendeleza masomo yake ya fizikia hadi chuo kikuu. Paul Gottlieb Nipkow alifanya utafiti mkubwa na hatimaye alifanikiwa kuvumbua transimita ya televisheni. Chombo hicho kilichobuniwa na Nipkow kiliweza kurusha mawimbi ya televisheni katika umbali wa mita 30 na baadaye transimita iliyotengenezwa na mvumbuzi huyo wa Kijerumani ilikamilishwa na wabunifu wengine.