Jumatano, Agosti 28, 2019
Leo ni Jumatano tarehe 26 Mfunguo Tatu Dhulhija 1440 Hijria sawa na Agosti 28 mwaka 2019 Milaadia.
Siku kama ya leo miaka 881 iliyopita alizaliwa huko katikati mwa Iraq Abul-Fadhail Amedi fakihi na mwanafasihi wa Kiislamu. Baada ya kusoma elimu za fiqhi, Usul Fiqhi, fasihi na hisabati katika mji wa Baghdad aliondokea kuwa mahiri katika elimu hizo. Abul Fadhail Amedi alikuwa na mashairi yenye kubeba maana kubwa. Amedi aliaga dunia akiwa katika eneo alilozaliwa akiwa na umri wa miaka 49.

Tarehe 28 Agosti 1749 alizaliwa Johann Wolfgang Von Goethe malenga na mwandishi mkubwa wa Kijerumani. Von Goethe alisoma na kujifunza mambo mbalimbali kama uchoraji na kadhalika katika mji aliozaliwa wa Frankfurt nchini Ujerumani, huku akiendelea na masomo yake ya taaluma ya sheria. Von Goethe ambaye anahesabiwa kuwa mmoja kati ya waenezaji wa fasihi ya lugha ya Kifarsi, alivutiwa mno na fasihi ya Kifarsi na hasa mashairi ya Hafidh, malenga na mshairi mashuhuri wa Kiirani. Mwandishi huyo wa Kijerumani alikipenda sana Kitabu Kitakatifu cha Qur'ani pamoja na dini ya Kiislamu. Johann Wolfgang Von Goethe alifariki dunia mwaka 1832.
Siku kama hii ya leo miaka 56 iliyopita yaani Agosti 28, 1963, Martin Luther King mwanaharakati mkubwa wa kutetea haki za Wamarekani weusi nchini Marekani, alihutubia umati mkubwa wa watu waliofanya mgomo wa kutaka wapewe haki ya kijamii nchini humo. Luther King ambaye ni Mmarekani mweusi alihutubia umati huo kwenye uwanja wa kumbukumbu wa Lincoln mjini Washington. Kwenye mkutano huo, Martin Luther King alieleza ndoto yake ya kuwa huru Wamarekani weusi.
Na siku kama ya leo miaka 62 iliyopita kombora la kwanza la kuvuka mabara lilirushwa hewani na wasomi wa Urusi ya zamani. Siku nne baadaye yaani tarehe 4 Oktoba wasomi wa Urusi walirusha angani satalaiti ya kwanza dunia iliyopewa jina la Sputnik 1 kwa kutumia kombora hilo. Hatua hiyo ilipongezwa kote dunia na wasomi hao walitangaza kuwa, watatuma mwanadamu angani katika kipindi cha chini ya miaka mitatu na kwamba watatuma chombo cha anga mwezini miaka mitano baadaye. Wasomi hao wa Urusi walitimiza ahadi zao.