Aug 30, 2019 22:11 UTC
  • Jumamosi, 31 Agosti, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 29 Mfunguo Tatu Dhul-Hija 1440 Hijria mwafaka na tarehe 31 Agosti 2019 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 62 iliyopita, nchi ya Malaysia ilipata uhuru kutoka kwa mkoloni Mwingereza. Wananchi wa Malaysia walianza kuingia taratibu katika dini ya Uislamu katika karne ya 13 Miladia. Ushawishi wa nchi za Ulaya ulianza kuenea nchini humo mwanzoni mwa karne ya 16 sambamba na kuwasili nchini humo baharia wa Kireno, Albuquerque. Uholanzi iliidhibiti nchi hiyo katika karne ya 17 na kuanza kuikoloni. Mwaka 1824 nchi za Uholanzi na Uingereza zilifikia makubaliano ambapo Waingereza waliichukua Malaysia na Waholanzi wakachukua Indonesia. Waingereza waliendelea kuikolonia Malaysia hadi nchi hiyo ilipopata uhuru katika siku kama ya leo. ***

Bendera ya Malaysia

Miaka 52 iliyopita katika siiku kama ya leo, alifariki dunia Ilya Ehrenburg mwandishi wa Umoja wa Kisovieti yaani Urusi ya zamani. Alizaliwa tarehe 17 Januari mwaka 1891 huko Kiev nchini Ukraine. Ilya ambaye anatambuliwa kuwa mkosoaji, mwandishi wa tamthilia, riwaya na hadithi alifanya kazi ya uandishi habari kwa miaka kadhaa huko Ulaya hususan Uhispania. Mwandishi huyo wa Kirusi aliandika vitabu visivyopungua 100 na miongoni mwa vitabu hivyo ni kile cha "tufani" na "kuanguka kwa Paris". ***

Ilya Ehrenburg

Katika siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, Imamu Mussa Sadr, mwanazuoni na msomi mashuhuri wa Lebanon alitoweka katika mazingira ya kutatanisha akiwa safarini nchini Libya. Alizaliwa mnamo mwaka 1928 katika mji mtakatifu wa Qum nchini Iran na baada ya kuhitimu masomo yake alielekea Lebanon. Baada ya kuwasili nchini humo, Imamu Mussa Sadr alichukua hatua kubwa za kuboresha maisha ya Walebanoni waliokuwa katika hali mbaya ya kiuchumi, kijamii na kisiasa. Mwanazuoni huyo pia alikuwa muungaji mkono wa harakati za mapambano ya ukombozi wa Palestina na aliasisi Harakati ya Wanyonge kwa ajili ya kutetea haki za Waislamu wa Lebanon. Hadi sasa juhudi mbalimbali za kutaka kufahamu hatima ya Imamu Mussa Sadr bado hazijazaa matunda. ***

Imamu Mussa Sadr

Siku kama ya leo miaka 28 iliyopita, nchi ya Uzbekistan ambayo kijiografia ipo katikati mwa Asia ilipatia uhuru kutoka kwa Umoja wa Kisovieti. Kuanzia karne ya 6 kabla ya Miladia, nchi hiyo ilikuwa sehemu ya utawala wa Kiirani wa Hakhamanesh. Na baada ya hapo, koo na tawala mbalimbaliza Iran na zisizo za Kiirani ziliitawala nchi hiyo. Baada ya kudhihiri na kuja Uislamu na kukombolewa Uzbekistan na Waislamu katika nusu ya pili ya karne ya 9 Miladia, ukoo wa Kiirani wa Samaniyan ulishika hatamu za uongozi nchini humo na kupelekea utamaduni wa Kiirani na lugha ya Kifarsi kushamiri na kufikia kileleni katika nchi hiyo. ***

Bendera ya Uzbekistan

Na siku kama ya leo miaka 14 iliyopita, karibu Waislamu 1000 wa Iraq waliaga dunia wakati walipokuwa katika hafla ya maombolezo katika mji wa Kadhmein jirani na Baghdad. Inaelezwa kuwa, zaidi ya Waislamu milioni moja wa Iraq walikuwa katika maombolezo ya kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Mussa al-Kadhim (as), ambapo kulishuhudiwa harakati za kutiliwa shaka sambamba na kusikika sauti za milipuko kadhaa. Watu wakiwa na lengo la kutoka katika eneo hilo walisongamana na kupelekea mamia ya wengine kukanyagwa huku wengine wakidondoka kutoka juu ya daraja.***

Kadhmein