Aug 31, 2019 22:07 UTC
  • Jumapili, Septemba Mosi, 2019

Leo ni Jumapili tarehe Mosi Mfunguo Nne Muharram 1441 Hijria sawa na Septemba Mosi 2019Milaadia.

Tarehe Mosi Muharram inasadifiana na kuanza mwaka mpya wa Hijria Qamaria. Mwaka wa Hijria Qamaria unahesabiwa kwa mujibu wa mzunguko wa mwezi na katika nchi nyingi za Kiislamu unatumiwa kwa ajili ya masuala ya kidini au hata kijamii. Mwaka wa Hijria Qamaria pia unatumika katika masuala mengi ya kiibada kama vile kuainisha mwanzo wa funga ya mwezi wa Ramadhani, Hija, kuainisha miezi mitakatifu na kwa ajili ya historia ya matukio mbalimbali. Baadhi ya maulamaa wanasema mwaka wa Hijria ulianzishwa katika zama za utawala wa khalifa Umar bin Khattab kutokana na ushauri uliotolewa na Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as) ambaye aliagiza mwanzo wa hijra ya Mtume kutoka Makka na kwenda Madina uwe mwanzo wa mwaka wa Kiislamu. Kabla ya kalenda ya Miladia kutumika kote duniani, nchi nyingi za Kiislamu zilikuwa zikitumia kalenda ya Hijria Qamaria. 

Miaka 845 iliyopita katika siku kama ya leo, ilianza kazi ya kujenga mnara maarufu wa Pisa huko katika mji wa Pisa nchini Italia. Mnara huo ulijengwa kwa ajili ya kuitundika saa juu yake. Hata hivyo mnara huo uliokuwa na urefu wa mita 55 ulipinda kwa karibu mita tano muda mfupi baada ya kuanza kujengwa. Hitilafu hiyo imeufanya mnara huo ujulikane kwa jina la"Mnara Uliopinda wa Pisa." Hadi kufikia sasa mnara huo umefanyiwa marekebisho ya kiwango fulani kufuatia juhudi za wahandisi na wataalamu wa nchi mbalimbali. 

Mnara wa Pisa

 

Katika siku kama ya leo miaka 96 iliyopita, mtetemeko mkubwa wa ardhi ulioambatana na uharibifu mkubwa na kuua idadi kubwa ya watu, ulitokea nchini Japan. Zilzala hiyo iliyokuwa na ukubwa wa 8.3 kwa kipimo cha Rishta iliua watu zaidi ya laki moja na 40 elfu. Mtetemeko huo uliyakumba hata baadhi ya maeneo ya miji ya Tokyo na Yokohama. Mbali na hasara kubwa zilizosababishwa na mtetemeko huo, idadi kubwa ya Wajapani pia walikosa makazi yao na nyumba nyingi ziliteketea kwa moto.

Kipimo cha Rishta

Siku kama ya leo miaka 80 iliyopita, Vita vya Pili vya Dunia vilianza baada ya jeshi la Ujerumani ya Kinazi kuanzisha mashambulizo dhidi ya Poland. Adolf Hitler alianza kuliandaa jeshi lenye nguvu wakati akiwa madarakani huko Ujerumani kwa kutumia vibaya hadhi yake na hisia za ubaguzi na utaifa wa wananchi wa nchi hiyo, ambao walikuwa wamefedheheka sana kufuatia kushindwa vibaya katika Vita Vikuu vya Kwanza vya Dunia. Katika kipindi kifupi, Hitler alifanikiwa kuikalia kwa mabavu sehemu kubwa ya ardhi za Ulaya na kaskazini mwa Afrika. 

Mwanzo wa Vita Vikuu vya Pili vya Dunia

Na miaka 50 iliyopita katika siku kama ya leo, kulifanyika mapinduzi ya kijeshi nchini Libya yaliyomfikisha madarakani Kanali Muammar Gaddafi. Kabla ya mapinduzi hayo, Libya ilikuwa ikiongozwa na utawala wa Mfalme Idris wa Kwanza. Wakati mfalme Idris alipoelekea nchini Uturuki kwa ajili ya matibabu, kundi moja la wanajeshi ambalo liliongozwa na Kanali Muammar Gaddafi lilifanya mapinduzi ya kijeshi na kumvua madaraka mfalme huyo sambamba na kutangaza utawala wa kisoshalisti nchini Libya. Hata hivyo katika miaka ya kukaribia kupinduliwa na kuuliwa, Muammar Gaddafi alianza kufuata siasa za Wamagharibi na kuwakabidhi viwanda vya mafuta vya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika, hali inayodaiwa kuchangia hasira za wananchi. Muammar Gaddafi aliondolewa madarakani na kuuawa kufuatia mapinduzi ya tarehe 21 mwezi Agosti 2011.

Muammar Gaddafi