Sep 02, 2019 09:51 UTC
  • Mguso wa nyoyo katika maombolezo ya Husain AS

Bismillahir Rahmanir Rahim. Assalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh. Karibuni wasikilizaji wapenzi katika makala hii maalumu tuliyokuandalieni kwa mnasaba wa mwezi mtukufu wa Muharram. Makala yetu imebeba kichwa cha maneno kisemacho, Mguso wa Nyoyo katika Maombolezo ya Imam Husain AS. Ni matumaini yetu mtakuwa nasi hadi mwisho wa makala hii.

Hali maalumu hutanda katika anga ya miji na vijiji vyote vya Iran na katika baadhi ya nchi za dunia wakati unapoingia mwezi mtukufu wa Muharram, kila mwaka. Wadogo kwa wakubwa, wake kwa waume, wazee kwa vijana, wote hujishughulisha kuiandaa misikiti na Husainia na kuzipa sura ya Muhamarram huku nyoyo zao zikiwa zimetanda mapenzi makubwa yasiyoelekezeka kwa Bwana huyo wa Mashahidi, Aba Abdillahil Husain AS. Pamoja na kwamba tukio la Ashura limetokea karne nyingi zilizopita, lakini mndirimo wa shauku ya mapenzi kwa Husain bado unachemka katika nyoyo za wapenzi wa Bwana Mtume Muhammad SAW na Ahlul Bayt wake AS. Bwana Mtume SAW amenukuliwa akisema: Kuuawa shahidi Husain AS kunaleta joto ndani ya nyoyo za waumini, joto ambalo kamwe haliwezi kupozeka. Naam! Mapenzi, shauku na mguso huo mkubwa wa hisia za kumpenda Imam Husain AS hushamiri na kupamba moto katika mwezi wa Muharram kila mwaka, ikiwa ni kama akiba kutoka kwa Mwenyezi Mungu katika nyoyo za waumini.

Kufanyika kwa hamasa kubwa na kwa shauku ya hali ya juu maombolezo ya mwezi wa Muharram kila mwaka, kwa hakika kunathibitisha ushindi wa Mapinduzi ya ‘Ashura. Ijapokuwa Imam Husain AS alimwaga damu yake na ya wafuasi wake waaminifu katika jangwa la Karbala, lakini alifanikiwa kufikia lengo la mapinduzi yake matukufu, la kuipa uhai mpya dini tukufu ya Kiislamu. Watukufu hao walitumia uongofu wao wa kipekee kuwaelimisha walimwengu maana ya kupambana na dhulma, na wenyewe wakafanikiwa kupata daraja tukufu na ya juu ya kuuawa shahidi. Mashahidi wa Karbala wataendelea kuwa na nafasi ya kipekee mbele ya wapigania ukombozi na uadilifu kote ulimwenguni, na wataendelea kuwa vipenzi vya nyoyo za waumini.

Hata hivyo ushindi wa mapambano ya Imam Husain AS katika siku ya ‘Ashura ya mwaka wa 61 Hijria haukupatikana kirahisi, ulipatikana kwa kumwagwa damu takasifu za wajukuu wa Bwana Mtume Muhammad SAW na wafuasi wao waaminifu. Ulipatikana kwenye mazingira ya mateso ya watoto wadogo, kutokuwa na kwa kumbilia akinamama na kwenye anga iliyojaa kudhulumiwa watu hao watukufu. Ni kwa sababu hiyo ndio maana kila yanapokumbushiwa masaibu na dhulma hiyo waliyofanyiwa wajukuu wa Bwana Mtume SAW na wafuasi wao huko Karbala, nyoyo za watu huguswa na huathirika na kuzifanya kumbukumbu za ushindi huo wa damu dhidi ya upanga ziandamane na maombolezo.

 

Waislamu na wapenzi wa Ahlul Bayt AS wanaubakisha hai daima ujumbe wa mapinduzi ya Karbla kwa kukumbuka mapambano ya Imam Husain AS. Wakati watu wanapokutanika kukumbuka na kuomboleza masaibu ya Karbala, hupatikana fursa ya kutajwa sifa, shakhsia na uadhama wa kiroho wa watukufu hao. Hao walikuwa ni watu waliopambika kwa sifa zote nzuri za kibinadamu kama vile subira, uaminifu, istikama, kutotetereka na kujitolea katika njia ya Allah na kila mmoja wao ni kigezo na ruwaza ya sifa bora na njema. Lililo muhimu zaidi ni kuwa, wakati waombolezaji wanapokusanyika kukumbuka dhulma na masaibu yaliyowafika mashahidi wa Karbala, huwa ni fursa ya kuonesha hisia na mapenzi yao makubwa kwa watukufu hao.

Katika upande mwingine, watu wanaoshiriki kwenye maombolezo hayo hupata fursa ya kujua ukatili wa maadui wa Imam Husain AS yaani Yazid na wafuasi wake na kuzidi kutambua ni kiasi gani hawakuwa na chembe ya huruma katika nyoyo zao. Ukweli wa nambo ni kuwa ‘Ashura ni mapambano baina ya makundi mawili. Kundi moja likiwa kwenye kilele cha chuki na uadui na jingine likiwa kwenye kilele cha mapenzi kwa dini na mafundisho ya Mwenyezi Mungu. Karbala ni matukio ya mapambano hayo ya baina ya haki na batili. Katika upande mmoja kuna Imam Husain AS na wafuasi wake ambao katika sira na vitendo vyao vyote kumesheheni mapenzi ya haki na taqwa na katika upande wa pili kuna Yazid na wafuasi wake ambao ni dhihirisho la jinai na uovu.

Kuna hadithi moja maarufu kutoka kwa Imam Muhammad Baqir AS ambaye amenukuliwa akisema: Je dini inaweza kuwa kitu kingine ghairi ya mahaba na mapenzi? Maana ya mahaba na mapenzi inayokusudiwa hapo si ile iliyopotoshwa zama hizi na kupewa sura mbaya. Mapenzi ni kitu kitakasifu na kitukufu zaidi kuliko kitu kingine chochote. Maombolezo ya kukumbuka siku aliyouawa shahidi Imam Husain AS nayo yanafanyika kwa msingi huo huo. Kumbukumbu hizo zina lengo la kueneza mapenzi, na wakati watu wanapolia kwenye ‘majalis’ za maombolezo ya Imam Husain AS nyoyo za watu hao hujaa mapenzi na huruma kwa Ahlul Bayt wa Mtume SAW. Tab’an inabidi tugusie nukta hii kwamba, mbegu ya mapenzi hayo ilipandwa tangu katika kipindi cha Bwana Mtume Muhammad SAW. Qur’ani Tukufu inayataja mapenzi kwa Ahlul Bayt kuwa ni kitu chenye malipo bora na makubwa sana mbele ya Mwenyezi Mungu. Katika sehemu moja ya aya ya 23 ya Surat Shura, tunasoma: “Sema; kwa haya siombi malipo yoyote kwenu isipokuwa mapenzi kwa ndugu.” Wakati iliposhuka aya hiyo, masahaba walimuuliza Bwana Mtume, Ya Rasulallah, ni akina nani hao ndugu zako ambao ni wajibu kwetu kuwapenda? Mtume alijibu kwa kusema ni Ali, Faatima na wana wao. Alirejea mara tatu maneno hayo. Hadhithi hiyo imepokewa kwenye vitabu vingi vikiwemo karibu vitabu 50 vya Waislamu wa Kisunni.

Mwezi wa Muharram, wapenzi wa Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW huuadhimisha kwa namna tofauti

 

Maombolezo ya ‘Ashura kwa upande mmoja ni kudhihirisha mapenzi kwa Imam Husain AS na kwa upande wa pili ni kuonesha hasira kwa uovu na ubaya wote uliofanywa na Yazid na wafuasi wake katika zama na nyakati zote na katika sehemu yoyote ile. Wakati mapenzi na kujibari na waovu kunapofanywa kuwa jambo la msingi, basi jambo hilo huwa halimalizikii kwenye kuonesha hisia tu, bali athari zake huenea pia kwenye matendo ya kila siku ya watu hao na hujenga mfungamano mkubwa na wa kina baina ya mwenye kupenda na mwenye kupendwa na matendo ya wawili hao hufanana na hufuata mkondo mmoja na matokeo yake ni kuambizana wawili hao kuwa mimi nitaishi kwa amani na wanaokupa amani wewe na nitapambana na kumfanyia uadui kila anayekufanyia uadui.

Kulia katika ‘majalis’ za maombolezo ya Imam Husain AS hutokana na nyoyo kuguswa mno na mapenzi ya mtukufu huyo na masaibu aliyoyapata katika jangwa la Karbala. Matukio mengi ya Karbala yanazifanya nyoyo za wanaoyasikia masaibu hayo ziguswe, zisisimke na zipate hamasa. Je, kisa cha usiku wa kuamkia siku ya ‘Ashura mumekisikia? Pale Imam Husain AS alipowakusanya masahaba wake na kuwaambia: Tumieni kiza hiki cha usiku kuokoa maisha yenu kwani maadui hawa wananitaka mimi tu na hawakutakini nyinyi? Wakati huo kimya cha ajabu kilifunika kikao hicho. Baadaye kidogo wafuasi wa Imam Husain AS mmoja baada ya mwingine walikwenda mbele ya Imam AS na kila mmoja akiwa na maneno ya kusisimua na kuvutia mno. Mmoja alisema: Kwa sababu gani unataka tukuache peke yako, yaani unataka sisi tubaki hai baada ya kuuawa kwako? Tunamuomba Mwenyezi Mungu kamwe asitujaalie kufikiwa na siku kama hiyo. Maneno hayo yaliyojaa ushujaa yalitolewa na ndugu yake Imam Husain, yaani Abul Fadhlil Abbas AS akifuatiwa na wafuasi wengine wa Imam ambao kila mmoja alitoa matamshi ya hamasa na yenye mguso wa hali ya juu. Mmoja wa wafuasi wa mtukufu huyo alisema, Ewe mwana wa Mtume wa Mwenyezi Mungu, niko tayari niuawe na kufufuka mara elfu moja kulikoni kuona dini ya Mwenyezi Mungu inapotoshwa na kizazi chako kinauawa. Alimradi kila mmoja kati ya masahaba wa Imam Husain AS katika usiku huo wa kihistoria alionesha ushujaa wa hali ya juu na uaminifu wake usio na kifani kwa Imam wake.  Hii ni kwa sababu mashujaa hao wa Karbala walijua kuwa, kifo ni kitu ambacho kila mwanadamu atakionja. Kifo ni hatua tu ya kutoka katika maisha ya hapa duniani ya mwanadamu na kuingia kwenye maisha ya milele na hakuna mtu yeyote anayeweze kuikwepa hatua hiyo. Lakini kujitolea katika njia ya Imam Husaini ambayo ni njia ya Mwenyezi Mungu, huleta heshima na utukufu wa milele. Hivyo maombolezo ya kumbukumbu ya matukio ya Karbala yanakumbushia watu watukufu kama hao.

Umati mkubwa wa Waislamu katika kumbukumbu za masaibu ya Imam Husain AS

 

Kulia katika majalis za Imam Husain AS huleta mguso wa aina yake katika nyoyo za watu. Mwanadamu hupata maisha yake kupitia upendo na hisia njema za ndani ya moyo wake. Wakati mtu anaposikia masaibu yaliyowafika wajuu wa Bwana Mtume Muhammad SAW na wafuasi wao wakiongozwa na Imam Husain AS katika jangwa la Karba, na moyo wake kuumia, ukaungulika na kuchemsha hisia kali za huzuni ndani ya moyo wake na kuakisiwa na machozi machoni mwake, hali hiyo huwa ni uthibitisho kuwa moyo wa mtu huyo ni mzima. Hilo halina maana ya kuwa moyo wake ni dhaifu au ni wa mtu aliyekata tamaa na maisha. Wakati mtu anaposikia masaibu yaliyotokea kwenye jangwa lenye joto kali, miili iliyokatwa vipande vipande ya mashahidi wa Karbala, vichwa vya vipenzi wa Mtume wa Mwenyezi Mungu vilivyotundikwa juu ya mikuki ya maadui na mahema yaliyochomwa moto ya watu wa nyumba ya Bwana Mtume Muhammad SAW, miili inayochiriza damu kwa kupigwa mijeledi na maadui, furaha na shamrashamra zilizooneshwa na maadui hao wa Ahlul Bayt wa Mtume Muhammad SAW, na masaibu yaliyomkuta Imam Zaynul Abidin AS na Bibi Zaynab SA, lazima moyo wake utaguswa na kuathirika sana. Haiwezekani mtu asikie masaibu yote hayo ya kutisha asiguswe na kuumizwa mno moyoni.

Kumlilia Imam Husain kuna athari kubwa sana pia katika upande wa masuala ya kisiasa na kijamii. Kwani sambamba na vilio hivyo kuleta hisia kali nyoyoni, vinakumbushia pia namna mtu mtukufu kama Imam Husain AS alivyojitolea muhanga yeye na aila yake kwa ajili ya kuifufua na kuilinda dini ya Mwenyezi Mungu. Kaulimbiu maarufu na ya kishujaa ya Imam Husain AS katika mapambano ya Karbla haiwezi kusahaulika nayo ni pale aliposema: Kama dini ya Muhammad haitosimama ila kwa kuuawa mimi, basi enyi panga, chukueni roho yangu! Kwa kweli maombolezo ya masaibu yaliyomfika Imam Husain na wafuasi wake watukufu huko Karbala yanamuunganisha mtu anayefanya maombolezo hayo na shakhsia adhimu na tukufu ya Husain bin Ali AS  na malengo matukufu yaliyopiganiwa na mjukuu huyo wa Mtume Muhammad SAW.

Mtu anapomlilia Imam Husain AS huwa anatangaza uaminifu wake kwa bwana huyo wa vijana wa peponi na malengo matukufu aliyoyapigania. Athari za kuomboleza masaibu ya Imam Husain AS haziwezi kupatikana kama muombolezaji hatojipamba kwa sifa za mtukufu huyo katika maisha yake ya kila siku. Kilichowafanya wananchi Waislamu wa Iran kufanikiwa katika mapambano yao dhidi ya utawala wa kidhulma na wa kitaghuti uliokuwa unalindwa na kuungwa mkono kwa kila namna na madola ya kibeberu hasa Marekani, ni kutokana na Waislamu hao kuchukua funzo la kivitendo kutoka kwa mapambano ya Imam Husain AS katika jangwa la Karbala. Ukweli ni kwamba, kudumisha kumbukumbu za masaibu ya Karbala kunayabakisha hai mapinduzi ya Imam Husain AS na kuidumisha jihadi katika njia ya Mwenyezi Mungu. Maombolezo ya ‘Ashura ni silaha madhubuti sana ya kukabiliana na madhalimu na madola ya kibeberu na kitaghuti ya zama zote. Tunamalizia makala hii kwa maneno ya Imam Khomeini (MA) aliposema, kulia katika maombolezo ya Imam Husain AS kunaweka hai mapinduzi na mwamko wake kwa maana ya kwamba, jamii ya watu wachache wanaweza kusimama imara kukabiliana na dola kubwa lenye nguvu. Maadui wanaogopeshwa na maombolezo hayo kwani maombolezo hayo ni maombolezo ya madhulumina, ni mayowe ya waliodhulumiwa mbele ya dhalimu. Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh.

 

Tags