Jumamosi, 07 Septemba, 2019
Leo ni Jumamosi tarehe 7 Mfunguo Nne Muharram 1441 Hijria ambayo iinasadifiana na tarehe 7 Septemba 2019 Miladia.
Tarehe 7 Mfunguo Nne Muharram mwaka 61 Hijria yaani miaka 1380 iliyopita, kamanda wa jeshi la Yazid bin Muawiya, Umar bin Sa'd aliliamuru jeshi lake kumzuia maji ya mto Furati Imam Hussein na watu waliokuwa katika msafara wake. Baada ya Ubaidullah bin Ziyad kumzingira mjukuu wa Mtume (saw) akiwa na jeshi kubwa katika medani ya Karbala alimwandikia barua Umar bin Sa'd akimtaka amlazimishe Imam Hussein kutangaza utiifu wake kwa mtawala Yazid. Vilevile alimwandikia barua nyingine akimtaka kumzuia Imam Hussein na wafuasi wake wasitumie maji ya mto Furati. Imam Hussein, ndugu, watoto na masahaba zake waliuawa shahidi tarehe 10 Muharram mwaka huo wakiwa na kiu tena kandokando ya mto Furati. ***

Miaka 128 iliyopita katika siku kama ya leo kulingana na kalenda ya Hijria, alizaliwa huko Najaf Iraq Ayatullah al-Udhma Sayyid Muhammad Hadi Milani, Marjaa mkubwa Kishia. Milani alianza kusoma Qur'ani sambamba na masomo ya dini akiwa mdogo. Baadaye alianza kuhudhuria darsa za walimu wa Hawza (Chuo Kikuu cha Kidini) ya Najaf akiwa na lengo la kujiendeleza zaidi kielimu. Bidi na jitihada kubwa katika masomo, zilimfanya Sayyid Muhammad Hadi Milani akwee haraka mno daraja za kielimu na kuwa mahiri katika masomo ya dini pamoja na fasihi za lugha ya Kiarabu na Kifarsi. Baada ya muda akaanza kufundisha sanjari na kuandika vitabu. Darsa zake zilikuwa zikijaa wanafunzi. Ayatullah Milani amefanikiwa kutoa wanafunzi wengi waliokuja kuondokkea kuwa wahakiki na wanafikkra wakuubwa. ***
Katika siku kama ya leo miaka 197 iliyopita, nchi ya Brazil ilipata uhuru wake toka kwa mkoloni Mreno. Ureno ilianza kuikoloni Brazil mwaka 1494, na mbali na kuwatumikisha watu wa jamii ya wekundu wa nchi hiyo, ilichukua mamilioni ya Waafrika kwa ajili ya kuwatumikisha kama watumwa katika shughuli za kilimo nchini humo. ***
Siku kama ya leo miaka 120 iliyopita, kulitokea Harakati ya Wanamasumbwi nchini Uchina. Wanamasumbwi lilikuwa jina walilopewa wanajeshi wa China waliosimama kupambana na ubeberu wa nchi za kigeni hususan za Magharibi ulioambatana na harakati za wamishonari wa Kikristo ndani ya China. Miongoni mwa hatua zilizochukuliwa na wanamasumbwi hao ni kuteka balozi za nchi za Magharibi katika mji wa Beijing na kupambana vikali na shughuli za wahubiri wa Kikristo kutoka Ulaya. Hata hivyo Harakati ya Wanamasumbwi wa Kichina ilikandamizwa na majeshi ya Ulaya, Marekani na Japan na serikali ya China ikalazimika kulipa gharama kubwa kwa nchi hizo. ***

Miaka 35 iliyopita katika siku kama yya leo kulingana na kalenda ya Hijria Shamsia, Ayatullah Mirza Muhammad Baqir Ashtiyani alifariki dunia. Alimu huyo ni mjukuu wa Mirza Muhammad Hassan Ashtiyani mmoja wa viongozi wa Harakati ya Tumbaku nchini Iran. Alizaliwa mjini Tehran na baada ya kukamilisha masomo ya awali alielekea katika mji wa Najaf huko Iraq na kupata elimu kwa maulama mashuhuri wa zama hizo kama Ayatullah Mirza Naini na Sayyid Abul Hassan Isfahani. Ayatullah Muhammad Baqir Ashtiyani ameacha athari nyingi za vitabu zenye thamani kubwa katika nyanja mbalimbali. ***
Na katika siku kama ya leo miaka 22 iliyopita, alifariki dunia dikteta wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo au Zaire ya zamani, Jenerali Mobutu Sese Seko. Mobutu alizaliwa mwaka 1930 nchini Congo na mwaka 1950 alijiunga na harakati ya ukombozi ya Patrice Lumumba. Baada ya uhuru wa Congo, Jenerali Mobutu alishika uongozi wa jeshi la nchi hiyo na mwaka 1960 akawa Waziri Mkuu akiwa na umri wa miaka 30. Tarehe 25 Novemba mwaka 1965 Mobutu alipindua serikali na kushika hatamu za nchi hiyo na kuitawala kidikteta. Tarehe 16 Mei 1997 Mobutu alilazimika kukimbia nchi hiyo na kwenda Morocco ambako alifia na kuacha nyuma faili jeusi la ukatili na mauaji. ***