Alhamisi tarehe 12 Septemba 2019
Leo ni Alkhamisi tarehe 12 Muharram 1441 Hijria sawa na tarehe 12 Septemba 2019.
Siku kama ya leo miaka 1380 iliyopita sawa na tarehe 12 Mfunguo Nne Muharram mwaka 61 Hijria, msafara wa mateka wa Karbala uliojumuisha wanawake na watoto wa mashahidi wa Karbala, uliwasili katika mji wa Kufa, nchini Iraq. Kiongozi wa msafara huo alikuwa Imam Ali bin Hussein Sajjad (as), mtoto wa Imam Hussein (as) na Bibi Zaynab (as) dada wa Imam Hussein bin Ali (as). Licha ya taabu na masaibu waliokutana nayo, wawili hao wakiwa mjini Kufa walifichua kwa ushujaa mkubwa dhulma na jinai za utawala wa wakati huo na kuwalaumu wakazi wa mji huo kumtelekeza Imam Hussein AS na kutomuunga mkono.

Katika siku kama ya leo miaka 1380 iliyopita sawa na tarehe 12 Mfunguo Nne Muharram mwaka 61 Hijria, miili ya mashahidi wa Karbala ukiwemo mwili mtukufu wa mjukuu wa Mtume (saw) Imam Hussein AS ilizikwa ikiwa ni siku mbili baada ya kuuawa shahidi na kuachwa jangwani. Mashahidi wa Karbala walizikwa na watu wa kabila la Bani Asad. Mwili wa Imam Hussein na mashahidi wote wa Karbala ilibakia kwa siku mbili bila ya kuzikwa kwani hakuna mtu aliyekuwa na ujasiri wa kuzika miili hiyo kutokana na hofu ya utawala dhalimu wa Bani Umayyah. Hatimaye katika siku kama hii ya leo wanawake wa kabila la Bani Asad waliwahamasisha wanaume wao kuzika miili hiyo mitakatifu ya wajukuu wa Mtume na masahaba wa Imam Hussein (as).
Miaka 1346 iliyopita katika siku kama ya leo, kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia ya kuaminika, Imam Ali Zainul Abidin maarufu kwa lakabu ya Sajjad mwana wa Imam Hussein (as) na mmoja wa wajukuu wa Mtume Mtukufu S.A.W, aliuawa shahidi. Imam Zainul Abidin alizaliwa mwaka 38 Hijria huko katika mji wa Madina. Mtukufu huyo aliishi katika zama ambapo watu wa Nyumba ya Mtume Mtukufu walikuwa wakikabiliwa na masaibu mengi. Imam Sajjad A.S ambaye alikuwa mgonjwa wakati wa tukio la Karbala, baada ya harakati adhimu ya Imam Hussein, alibeba jukumu kubwa la kueneza ujumbe wa mapambano hayo na kuendeleza njia ya baba yake.

Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, inayosadifiana na 12 Septemba 1897, Irene Joliot- Curie mtaalamu wa Fizikia na Kemia wa Ufaransa, alizaliwa katika mji wa Paris. Baada ya kufanya utafiti wa muda mrefu, Irene Joliot- Curie alifanikiwa kuvumbua mada za radioactive.
Siku kama ya leo miaka 42 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 12 Septemba 1977, alifariki dunia Steve Biko mwanaharakati wa kupigania haki za wazalendo wa Afrika Kusini, akiwa chini ya ulinzi wa polisi. Steve Biko alikuwa kiongozi wa wanafunzi aliyefanya jitihada kubwa za kuwawezesha wazalendo waliokuwa wakibaguliwa wa Afrika Kusini na kuratibu harakati zao. Baada ya kufariki dunia akiwa mikononi mwa polisi, Biko alitambuliwa kuwa shahidi wa mapambano dhidi ya ubaguzi wa rangi. Alikuwa mashuhuri kwa kaulimbiu ya "Weusi ni Uzuri" (black is beautiful) ambayo ililenga kuwapa moyo wazalendo wa Afrika Kusini waliokuwa wakibaguliwa kwa sababu ya rangi ya ngozi yao.