Jumatano tarehe 11 Septemba 2019
Leo ni Jumatano tarehe 11 Mfunguo Nne Muharram 1441 Hijria sawa na Septemba 11 mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka 1380 iliyopita, yaani tarehe 11 Muharram mwaka 61 Hijiria, msafara wa mateka wa familia ya Bwana Mtume Muhammad (saw), baada ya tukio chungu la mauaji ya siku ya Ashura, ulianza safari ya kelekea Sham, yalikokuwa makao makuu ya utawala wa dhalimu wa Yazidi bin Muawiya. Baada ya majeshi ya Yazidi yaliyokuwa yakiongozwa na Omar bin Sa’ad kumuua shahidi Imam Hussein (as) na masahaba wake, majeshi hayo ambayo hayakuwa na chembe ya ubinadamu moyoni, yalianza kupora vitu vya thamani vya msafara wa watu wa familia ya Mtume (saw). Askari hao sanjari na kuchoma moto mahema ya Imam Hussein (as) na watu wake, waliwanyang’anya pia wanawake mapambo yao na kila walichokuwa nacho. Jioni ya siku kama ya leo msafara wa familia ya Imam Hussein uliokuwa ukiongozwa na Imam Sajjad (as) na Bibi Zainab (as), ulielekea Kufa na baadaye Sham.

Miaka 71 iliyopita katika siku kama hii ya leo, aliaga dunia Muhammad Ali Jinnah, mwasisi wa Pakistan. Jinnah alizaliwa mwaka 1876 katika mji wa Karachi kusini mwa Pakistan. Muhammad Ali Jinnah alikuwa miongoni mwa shakhsiya walioasisi chama cha Muslim League mnamo mwaka 1906. Chama cha Muslim League awali kilikuwa kikijishughulisha na masuala ya kitamaduni na kidini, lakini baadaye kikaingia katika uwanja wa siasa na kutaka kuundwa nchi huru kwa ajili ya Waislamu wa India.
Siku kama ya leo miaka 46 iliyopita, Jenerali Agustino Pinoche kamanda wa wakati huo wa vikosi vya majini vya Chile aliipindua serikali halali ya Salvador Alande katika mapinduzi yaliyoungwa mkono na Marekani. Alande ambaye alikuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Kisoshalisti cha Chile, alichaguliwa kuwa Rais wa nchi hiyo mwaka 1970 na kuanza mara moja kutekeleza mpango wa kutaifisha mabenki, sekta ya madini na viwanda, suala ambalo lilikomesha maslahi haramu ya makampuni makubwa ya Kimarekani nchini Chile. Alande pia alikabiliana na ushawishi wa Washington nchini humo na kuifanya Marekani ianzishe vitimbi vya aina mbalimbali dhidi ya kiongozi huyo.
Siku kama ya leo miaka 38 iliyopita inayosadifiana na tarehe 20 Shahrivar 1360 Hijria Shamsia, aliuawa Shahidi Ayatullah Sayyid Asadullah Madani, Imamu wa Swala ya Ijumaa katika mji wa Tabriz, kaskazini magharibi mwa Iran wakati wa kuswalisha Swala ya Ijumaa. Shambulio hilo la kigaidi lilifanywa na kikundi cha kigaidi cha Munafiqin. Ayatullah Madani alipatia elimu kwa maulamaa kadhaa katika mji wa Qum na kisha kuelekea Najaf Iraq, ambako aliweza kujipatia daraja ya juu ya kielimu ya Ijitihad. Msomi huyo alikamatwa na kuteswa mara kadhaa na askari wa utawala wa mfalme wa Iran kutokana na misimamo yake ya kuupinga utawala huo. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Imam Khomeini MA alimteua Ayatullah Madani kuwa Imam wa Swala ya Ijumaa katika mji wa Tabriz.
Miaka 18 iliyopita katika siku kama ya leo ya tarehe 11 Septemba mwaka 2001, ndege mbili kati ya nne za abiria za Marekani zilizotekwa nyara ziligonga minara miwili pacha ya jengo la Biashara la Kimataifa la mjini New York huku ndege moja ikigonga jengo la Wizara ya Ulinzi ya Marekani (Pentagon) huko Washington. Ndege ya nne ililengwa ikiwa katika anga ya Pensylvania na kuangushwa. Baadhi ya ghorofa za jengo la Biashara ya Kimataifa ziliporomoka na sehemu ya jengo la Pentagon pia ikaharibiwa katika mashambulizi hayo ya kigaidi. Karibu watu 3200 waliuawa katika mashambulizi hayo. Marekani ilitangaza kuwa mtandao wa al Qaida uliokuwa ukiongozwa na Usama bin Laden raia wa Saudi Arabia, ndio uliohusika na mashambulizi hayo. Baada ya matukio ya Septemba 11 nchini Marekani, kulianza wimbi la ubaguzi na mashambulizi dhidi ya Waislamu na matukufu ya dini yao katika nchi za Magharibi.