Ijumaa tarehe 13 Septemba 2019
Leo ni Ijumaa tarehe 13 Mfunguo Nne Muharram 1441 Hijria sawa na Septemba 13 mwaka 2019.
Tarehe 13 Muharram mwaka wa 61 Hijria yaani siku kama hii ya leo miaka 1380 iliyopita Abdullah bin Afif aliuawa shahidi na gavana wa Yazid bin Muawiya, Ubaidullah bin Ziad. Afif alikuwa mtu wa kwanza kuanzisha malalamiko na upinzani wa wazi wazi dhidi ya jinai za Ubaidullah bin Ziad za kumuua shahidi mjukuu wa Mtume (saw), Imam Hussein (as). Baada ya Ubaidullah bin Ziyad kuwashambulia kwa maneno makali na kuwavunjia heshima mateka wa Karbala waliokuwa wamepelekwa katika majlisi yake, Abdullah bin Afif ambaye alikuwa miongoni mwa wachamungu wakubwa wa mji wa Kufa huko Iraq na wafuasi wa kweli wa Amirul Muuminin Ali bin Abi Twalib (as), alikerwa mno na mwenendo huo wa gavana wa Yazidi wa kuwavunjia heshima Watu wa Nyumba ya Mtume (saw) na kumjibu mtawala huyo kwa hasira. Ubaidullah ambaye hakutarajia kuona majibu kama hayo baada ya kuua watu wa Nyumba ya Mtume (saw) alitoa amri ya kukamatwa Afif na kupelekwa kwake. Hata hivyo watu wa kabila lake walizuia kitendo hicho. Askari wa utawala wa Bani Umayyah walivamia nyumba ya Abudullah bin Afifi usiku na kumtoa nje kisha wakamuua shahidi kwa kumkata kwa mapanga.

Siku kama ya leo miaka 1392 iliyopita, vilimalizika vita vya miaka 24 baina ya mfalme wa Iran na Roma. Khosrow Parvēz, mfalme wa Kisasani kwa kutekeleza mashambulizi mtawalia, aliweza kudhibiti maeneo ya Mesopotamia, Syria, Palestina, Misri na Asia Ndogo, na hivyo akawa ameweza kupanua wigo wa ushindi wake hadi kufikia Istanbul ya leo. Mwaka 591 Miladia, hatimaye amani ilifikiwa kufuatia kutiwa saini makubaliano baina ya mfalme Khosrow Parvēz na mfalme wa Roma. Hata hivyo tarehe Tano Juni mwaka 603 Miladia, kuliibuka tena vita vilivyodumu kwa muda wa miaka 24 baina ya nchi hizo mbili. Katika vita hivyo, jeshi la Iran lilipata ushindi mtawalia katika ardhi ya Roma kiasi cha kudhibiti karibu eneo zima la Roma ya Mashariki. Baadaye jeshi la mfalme Khosrow lilidhoofika na kumfanya mfalme huyo kukimbilia eneo la Ctesiphon, moja ya tawala za Sasania, huku akikataa pendekezo la usuluhishi. Aidha kutokana na Mfalme Khosrow Parvēz kuchana barua ya Mtukufu Mtume Muhammad (saw) na kulaaniwa na mtukufu huyo, utawala wa mfalame huyo ulidhoofika na hatimaye kushindwa na Waroma. Baadaye raia wa Iran kwa kushirikiana na jeshi la taifa walimuengua Khosrow kwenye utawala na kumtia jela kabla ya kuuawa kwake.
Siku kama ya leo miaka 769 iliyopita, vilianza vita vya Mansuriya katika silsila ya Vita vya Msalaba kati ya Wakristo na Waislamu. Vita hivyo vya kihistoria vilianzishwa katika eneo lililojulikana kwa jina hilo huko Misri na mfalme Saint Louis wa Ufaransa ambaye alikuwa na lengo la kuidhibiti Misri. Katika vita vya Mansuriya Jeshi la Msalaba lilipigwa vibaya na wapiganaji wa Kiislamu wa Misri waliokuwa wakiongozwa na Sallahuddin Ayyubi. Hatimaye Saint Louis alikamatwa mateka na Waislamu na kufungwa jela katika ikulu ya Loken ambayo hii leo inatumika kama jumba la makumbusho.
Miaka 239 iliyopita lifti au elevator kwa kimombo ilivumbuliwa. Mvumbuzi wa lifti hiyo ya kwanza alikuwa raia wa Marekani kwa jina la John Bikbart. Lifti hiyo ilifanyiwa majaribio kwa mara ya kwanza huko katika mji wa Chicago nchini Marekani. Katika majaribio hayo, watu kadhaa waliingia ndani ya lifti hiyo na kwenda juu na chini katika masafa marefu. Lifti ya kwanza ya umeme ilitengenezwa mwaka 1889 na ile ya otomatiki mwaka 1915.
Siku kama ya leo miaka 134 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 13 Septemba 1885, alizaliwa Aquilino Ribeiro mwandishi na mwanamapinduzi wa Ureno. Baada ya kumaliza masomo yake, Ribeiro alitumbukia kwenye uwanja wa kisiasa na kufungwa jela kwa miaka kadhaa. Mnamo mwaka 1961, Aquilino Ribeiro alifanikiwa kupokea tuzo ya Nobel katika taaluma ya fasihi, na miaka miwili baadaye yaani mwaka 1963 akafariki dunia.
Na Siku kama hii ya leo miaka 26 iliyopita, mwafaka na tarehe 13 Septemba 1993 Yasir Arafat, kiongozi wa zamani wa Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na Yitzhak Rabin waziri mkuu wa wakati huo wa utawala haramu wa Israel walisaini mkataba wa mapatano kwa jina la "Makubaliano ya Ghaza-Jericho" huko Washington, Marekani. Harakati ya Ukombozi wa Palestina PLO na utawala wa Kizayuni zilitambuana rasmi katika makubaliano hayo yaliyosainiwa miaka miwili baada ya kuanza mazungumzo eti ya amani kati ya Waarabu na utawala wa Kizayuni.