Sep 13, 2019 22:36 UTC
  • Jumamosi, 14 Septemba, 2019

Leo ni Jumamosi tarehe 14 Mfunguo Nne Muharram 1441 Hijria mwafaka na tarehe 14 Septemba 2019.

Siku kama ya leo miaka 207 iliyopita, moja kati ya ajali kubwa za moto ulimwenguni na uliowashwa kwa makusudi ilitokea katika mji mkuu wa Russia, Moscow. Tukio hilo lilitokea baada ya kupita siku moja tu, tangu mji huo uvamiwe na kukaliwa kwa mabavu na majeshi ya Napoleone Bonaparte, wakati mji huo ulipochomwa moto kwa amri ya mtawala wa wakati huo wa mji huo. Lengo la mtawala huyo lilikuwa ni kuyafanya majeshi ya Bonaparte yashindwe kustafidi na suhula za mji huo. Moto huo mkubwa uliteketeza na kuharibu kabisa robo tatu ya mji mzima wa Moscow. ***

Katika siku kama ya leo miaka 178 iiliyopita kulinga na kalenda ya Hijria, alifariki dunia mjini Isfahan, moja ya miji maarufu ya Iran, Sayyid Sadrud-Din Musawi Amili, msomi na mtaalamu wa hadithi wa Kiislamu. Sayyid Sadrud-Din Musawi Amili alizaliwa katika moja ya viunga vya mji wa Jabal Amil, nchini Lebanon. Akiwa kijana mdogo alisafiri nchini Iraq ambapo baada ya kuhitimu masomo yake ya awali katika Hawza ya elimu ya mjini Najaf, alianza kufanya utafiti katika elimu kadhaa kama vile fiqhi, usulu fiqhi na hadithi na kufikia daraja la juu katika uwanja huo. Sayyid Sadrud-Din Musawi Amili ameandika vitabu mbalimbali katika uga wa elimu ya sheria, nahau na mifano ya aya za Qur’ani Tukufu.***

Sayyid Sadrud-Din Musawi Amili,

Miaka 59 iliyopita katika siku kama ya leo, hati ya Jumuiya ya Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa Wingi Duniani (OPEC) ilitiwa saini na nchi za Iran, Saudi Arabia, Iraq, Kuwait na Venezuela. Jumuiya hiyo ilianzishwa kwa lengo la kukabiliana na makampuni makubwa ya mafuta ya Magharibi ambayo yalikuwa yakisimamia uvumbuzi, uchimbaji na uuzaji wa bidhaa hiyo kimataifa na kuainisha bei ya bidhaa hiyo muhimu kwa maslahi yao binafsi na kwa madhara ya nchi zalishaji. Licha ya kwamba awali jumuiya hiyo haikuwa na nguvu wala ushawishi wowote, lakini ilikuja kupata nguvu zaidi baada ya nchi kadhaa zikiwemo, Algeria, Libya, Nigeria, Qatar, Imarat, Gabon, Indonesia na Ecuador ambazo ni wazalisha wa mafuta kujiunga nayo. ***

Na siku kama ya leo miaka 41 iliyopita yaani tarehe 23 Shahrivar mwaka 1357 Hijria Shamsia kulifanyika maandamano makubwa hapa nchini kuwaenzi mashahidi waliokuwa wameuawa na vibaraka wa Shah siku kadhaa kabla yake. Siku hiyo umati mkubwa wa watu ulimiminika katika makaburi ya Behesht Zahraa mjini Tehran kuwaenzi mashahidi hao. Askari wa utawala wa Shah walikuwa na nia ya kuzuia maandamano hayo lakini umati mkubwa wa wananchi walioshiriki maandamano ulidumisha malalamiko yao dhidi ya utawala wa kidikteta wa Shah huko wakipiga nara za: “Iran ni nchi yetu na Khomeini ni kiongozi wetu.” ***

Maandamano dhidi ya mfalme Shah