Sep 15, 2019 22:09 UTC
  • Jumatatu tarehe 16 Septemba 2019

Leo ni Jumatatu tarehe 16 Muharram 1441 Hijria swa na Septemba 16 mwaka 2019.

Miaka 283 iliyopita katika siku kama ya leo, alifariki dunia Daniel Gabriel Fahrenheit mwanahesabati na mwanafizikia wa Kijerumani aliyevumbua kipimajoto yaani thermometer, akiwa na umri wa miaka 50. Fahrenheit alikuwa na fikra ya kubuni kifaa ambacho kingekuwa na uwezo wa kupima kiwango cha joto na mwaka 1724 mwanafizikia huyo Mjerumani akafanikiwa kutengeneza kipimajoto hicho. Kifaa hicho ambacho kimepewa jina la msomi huyo mwenyewe yaani Fahreinheit, bado kinatumika hadi leo.

Daniel Gabriel Fahrenheit

Miaka 88 iliyopita mwafaka na siku hii ya leo, aliuawa Omar al Mukhtar kiongozi wa taifa la Libya katika mapambano ya ukombozi dhidi ya wakoloni wa Italia. Omar Mukhtar aliyekuwa kiongozi wa kidini alizaliwa mwaka 1859. Mwaka 1895 alielekea Sudan na kushiriki katika harakati za kupambana na ukoloni wa Uingereza. Baada ya kushindwa kwa harakati hizo, Omar Mukhtar alirejea nchini Libya. Mwaka 1911 Wataliano waliivaia Libya kwa lengo la kuitawala nchi hiyo. Kiongozi huyo wa kidini aliwahimiza wapiganaji wa makabila ya Libya kusimama kidete na kupambana dhidi ya wavamizi wa Kitaliano na kuwasababishia hasara kubwa. Hata hivyo kwa kutumia askari wengi zaidi na silaha za kisasa wavamizi hao walimzingira Omar Mukhtar na wenzake na kumkamata na kisha wakamnyonga katika siku kama ya leo.

Omar al Mukhtar

Siku kama ya leo miaka 87 iliyopita Sir Ronald Ross daktari mashuhuri wa Kiingereza na mvumbuzi wa chanzo cha ugonjwa wa Malaria alifariki dunia.  Alizaliwa Mei 13 mwaka 1857 katika mji wa Almora huko India. Alielekea Uingereza akiwa mdogo na kusoka akiwa huko ambapo alifanikiwa kupata shahada ya uzamivu PhD katika taaluma ya tiba. Ufumbuzi wake wa chanzo cha Malaria ulikuwa na nafasi muhimu sana kwani uliandaa uwanja wa namna ya kukabiliana na maradhi hayo. Mwaka 1902 Dakta Ronald Ross alitunukiwa tuzo ya Nobel. Hatimaye Daktari Ronald Ross aliaga dunia katika siku kama ya leo baada ya kuishi kwa muda wa miaka 75.

Sir Ronald Ross

Tarehe 16 Septemba miaka 80 iliyopita Warsaw mji mkuu wa Poland ulizingirwa na Wajerumani, katika mwezi wa kwanza wa Vita vya Pili vya Dunia. Mashambulio ya wanajeshi wa Kinazi wa Ujerumani huko Poland yalianza siku 15 kabla ya kuanza vita hivyo.

Warsaw mji mkuu wa Poland

Siku kama ya leo miaka 78 iliyopita utawala wa kidikteta wa Reza Khan nchini Iran uliangushwa na kukaanza kipindi cha utawala wa mwanawe yaani Muhammad Reza Pahlavi. Baada ya mashambulio ya Jeshi Jekundu la Umoja wa Kisovieti upande wa kaskazini na jeshi la Uingereza upande wa magharibi na kusini mwa Iran na kukaliwa kijeshi Iran wakati wa kujiri Vita vya Pili vya Dunia, Reza Khan alilazimika kujiuzulu katika siku kama ya leo baada ya kutawala kidikteta nchini Iran kwa muda wa miaka 15. Baada ya kubaidishwa Reza Khan, mwanawe yaani Muhammad Reza Pahlavi aliingia madarakani kwa ushirikiano na Waingereza. Baada ya kubaidishwa kwa muda katika kisiwa cha Mauritius hatimaye alipelekwa Johannesburg Afrika Kusini. Aliishi huko hadi alipofariki dunia tarehe 26 Julai 1944.

Kuanza kwa utawalawa Muhammad Reza Pahlavi

Na siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, zilzala iliyokuwa na ukubwa wa 7.7 kwa kipimo cha rishta ililitikisa eneo la kaskazini mashariki mwa Iran na kuuharibu mji wa Tabas na vijiji vya kando kando yake. Watu zaidi ya elfu 25 waliuawa na makumi ya maelfu kujeruhiwa katika mtetemeko huo mkubwa wa ardhi. Zilzala ya Tabas ilitokea sambamba na kupamba moto mapambano ya wananchi wa Iran dhidi ya utawala wa Shah.

Zilzala ya Tabas