Sep 17, 2019 02:36 UTC
  • Jumanne tarehe 17 Septemba 2019

Leo ni Jumanne tarehe 17 Muharram 1441 Hijria sawa na Septemba 17 mwaka 2019

Siku kama hii ya leo miaka 543 iliyopita Nuruddin Abdulrahman Jami, malenga na mwanafasihi mkubwa zaidi wa Kiirani wa karne ya Tisa Hijria alifariki dunia katika mji wa Harat katika Afghanistan ya leo ambao wakati huo ulikuwa sehemu ya ardhi ya Iran. Alielekea huko Samarqand wakati wa ujana wake na akiwa huko alijifunza masomo ya dini, fasihi na historia. Vitabu muhimu vya malenga huyo ni pamoja na "Silsilatu Dh-hahab", Nafahatul Uns, Shawahidu Nubuwah na "Baharistan."

Kaburi la Nuruddin Abdulrahman Jami

Siku kama ya leo miaka 488 iliyopita alizaliwa Bahauddin al Amili maarufu kwa jina la Sheikh Bahai, faqihi na aalim mkubwa wa Kiislamu huko katika mji wa Baalbek nchini Lebaon. Baba yake Sheikh Bahai alikuwa mmoja wa maulamaa wakubwa wa Lebanon ambaye alisafiri naye nchini Iran akiwa mtoto. Sheikh Bahai alitumia kipaji chake kikubwa na kuweza kufikia daraja ya uanazuoni katika kipindi kifupi. Aalim huyo alipewa jina la Sheikhul-Islam kutokana na kipawa cha kielimu cha hali ya juu alichokuwa nacho. Sheikh Bahai ameacha zaidi ya vitabu 88 alivyoviandika kwa lugha za Kifarsi na Kiarabu. Baadhi ya vitabu vyenye thamani vya msomi huyo wa Kiislamu ni kama vile ya Jame Abbasi, Kashkool kilichojumuisha riwaya na hadithi, Tashrih al Aflaq na vingine vingi alivyoviandika kuhusu masuala ya hisabati na kemia. Sheikh Bahai alifariki dunia mwaka 1030 Hijria huko Isfahan Iran.

Kabuli la Sheikh Bahai

Siku kama ya leo miaka 71 iliyopita, aliaga dunia Emil Ludwig mwandika wasifu wa Kijerumani. Alizaliwa 1881 katika mji wa Breslau nchini Ujerumani ambao leo hii ni sehemu ya ardhi ya Poland. Alipata umashuhuri katika nusu ya pili ya karne ya 19 baada ya kuandika wasifu wa Otto Van Bismarck Kansela wa wakati huo wa Ujerumani, kiongozi wa zamani wa Russia Joseph Stalin, Beethoven na rais wa zamani wa Marekani Franklin Roosevelt. Wakati wa Vita vya Pili vya Dunia Ludwig alikuwa mwandishi wa habari aliyepata nafasi ya kufanya mahojiano na watawala waliokuwa na satua na ushawishi mkubwa katika kipindi hicho kama Franklin Delano Roosevelt, Winston Churchil na Joseph Stalin. 

Emil Ludwig

Tarehe 17 Septemba miaka 57 iliyopita aliuawa waziri mkuu wa zamaji wa Uturuki, Adnan Menderes. Alizaliwa mwaka 1899 na kupata elimu katika taaluma ya sheria. Alijiunga na harakati za kisiasa akiwa bado kijana na alishika hatamu za uongozi nchini Uturuki kama waziri mkuu mwaka 1950. Menderes ambaye alikuwa akifuata siasa za sera za kimarekani, alituma vikosi vya jeshi kushambulia Wakurdi wa nchi hiyo, suala ambalo liliwakasirisha sana wasomi na wanafikra wengi nchini Uturuki. Mwaka 1957 alichaguliwa tena kuwa Waziri Mkuu wa Uturuki na kukandamiza maandamano ya wanafunzi wa vyuo vikuu waliokuwa wakipinga utawala wake na kudai marekebisho ya kisiasa. Mwaka 1960 Adnan Menderes aliondolewa madarakani katika mapinduzi ya kijeshi na kufikishwa mahakamani ambapo alihukumiwa kifo kwa kupatikana na hatia ya kuua wanafunzi wa vyuo vikuu, kukiuka katiba ya nchi na kuwa na mahusiano haramu. Usiku wa kutekelezwa hukumu ya kifo, Menderes alifanya jaribio la kujiua lakini madaktari waliwahi kuokoa maisha yake. Hatimaye tarehe 17 Septemba, Adnan Menderes alinyongwa akiwa na umri wa miaka 62.

Adnan Menderes

Tarehe 26 Shahrivar miaka 39 iliyopita kwa mujibu wa kalenda ya Hijria Shamsia, utawala wa zamani wa Iraq ulifuta kwa upande mmoja makubaliano ya mipaka ya mwaka 1975 yaliyojulikana kwa jina la Mkataba wa Algeria kati yake na Iran. Siku hiyo, Saddam Hussein kiongozi wa zamani wa Iraq aliuchana mkataba huo wa Algeria mbele ya kamera za televisheni akiungwa mkono na madola ya kibeberu. Mkataba huo wa mwaka 1975 wa Algeria yalikuwa makubaliano ya mwisho kati ya nchi hizo mbili kwa ajili ya kutatua hitilafu za mipaka. Siku kadhaa baadaye, Saddam Hussein alianzisha uvamizi wa miaka minane dhidi ya ardhi ya Iran kwa uchochezi wa nchi za Magharibi.