Sep 18, 2019 11:26 UTC
  • Ruwaza Njema (20)

Assalaama Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.

Karibuni kusikiliza sehemu nyingine ya kipindi hiki cha Ruwaza Njema ambacho huchambua Hadithi mbalimbali kuhusiana na tabia njema, ya kupigiwa mfano na inayopaswa kuigwa na kufuatwa na Waislamu wote, ya Bwana Mtume (saw) kama tunavyoshauriwa kufanya na kitabu kitakatifu cha Qur'ani. Bila shaka Hadithi hizi ni msaada mkubwa kwetu kwa ajili ya kutuwezesha kutekeleza amri hiyo ya Mwenyezi Mungu Mtukufu.

Katika kipindi cha leo tutakunukulieni Hadithi kadhaa kuhusiana na maisha ya Jihadi ya Bwana wetu Mtume (saw) pamoja na usahilishaji wake wa ibada. Kuweni nasi hadi mwisho wa kipindi, karibuni.

************

Tunaona katika Hadithi zinazofuata dhihirisho kamili na la kuvutia la rehema za Mwenyezi Mungu kupitia nasaha alizozitoa Mtume Mtukufu (saw) kwa mujahideen wakiwa katika medani ya vita na wakikaribia kupata ushindi. Abu Ja'ffar Ahmad bin Muhammad al-Barqi ananukuu katika kitabu chake cha al-Masin Hadithi kutoka kwa mwenezaji wa suna safi za Mtume Muhammad (saw) al-Imam Ja'ffar as-Swadiq (as) kwamba alisema: 'Mtume (saw) alipoazimia kutuma kundi fulani (la wapiganaji) katika vita, alimwita kamanda wa kundi hilo na kumketisha pembeni yake na kisha kuwaita wapiganaji na kuwaketisha mbele yake na kisha kuwaambia: Mwendeeni adui kwa jina la Mwenyezi Mungu, njia ya Mwenyezi Mungu, kwa ajili ya Mwenyezi Mungu, kwa mujibu wa (mafundisho ya) dini ya Mtume wa Mwenyezi Mungu na wala msivunje mkataba. Msimfanyie mabaya (msimdhalilishe) adui, msifanye hiana (katika ugawaji ghanima/ngawira), kuikatakata maiti yake (kuidhalilisha) wala kukata mti wowote isipokuwa mnapolazimika kufanya hivyo. Msiwaue wazee, watoto wala wanawake. Na Mwislamu yeyote, awe ni mtu mashuhuri au la, anapomtazama mtu yeyote katika maadui, awe yuko mbali au katika safu za mbele kwenye jeshi, na kuhisi kuwa kuna kiwango fulani cha heri ndani yake, basi adui huyo mushrik atakuwa katika amani. Ili apate kusikia maneno ya Mwenyezi Mungu. Iwapo atasikia maneno ya Mwenyezi Mungu na kukufuateni basi huyo atakuwa ni ndugu yenu katika dini yenu, na akikataa; ombeni msaada wa Mwenyezi Mungu dhidi yake na kisha muelekezeni pahala pake pa amani.'

Ruwaza Njema

 

Na Hadithi nyingi zinatubainishia wazi jinsi Imam Ali (as) alivyotekeleza vyema na kivitendo mafundisho na ushauri huu muhimu wa Bwana Mtume (saw) katika vita vyake dhidi ya 'Nakitheen' (wasaliti), Qasiteen (wapotofu/wanafiki), Mariqeen (Khawareej/walioritadi) na makundi mengine ya waovu kama hao. Imam Ali (as) aliweza kutekeleza kikamilifu mafundisho hayo ya Mtume (saw), hata kuhusiana na maadui wake sugu. Tunarejea katika maisha ya Jihadi ya Bwana Mtume (saw) na kuona jinsi alivyokuwa akiamiliana kwa wema na wafungwa wa vita. Allama Tabarsi (MA) anasema katika Tafsiri yake ya Majmaul Bayaan kwamba Imam Ali (as) alipoiteka ngome ya al-Qamus ambayo ilikuwa ngome ya Ibn Abu al-Huqayq, Myahudi, Bilal al-Habashi, sahaba wa karibu wa Mtume (saw) alimchukua mateka Swafiyya Bint Huyayy bin Akhtab na mwanamke mwingine wa Kiyahudi na kuwapeleka mbele ya Mtume (saw). Alipokuwa anawapeleka kwa Mtume (saw), Bilal aliwapitishia sehemu ambayo maiti za Mayahudi waliokuwa wameuawa zilikuwa zimelala. Swafiyya alipoziona maiti hizo, aliangua kilio, kuukwaruzakwaruza uso wake na kujimwagia mchanga kichwani huku akiwa analia kwa sauti kubwa. Walipofika mbele ya Mtume (saw), alimuuliza Swafiyya: 'Ni kwa nini uso wake umekwaruzika hivi, kichwa kujaa mchanga hali ya kuwa unaonekana kuwa mwenye huzuni nyingi? Swafiyya, akamuelezea kisa cha kupita mbele ya maiti kilivyokuwa. Mtume alikasirishwa na kitendo cha Bilal kuwapitisha wanawake wafungwa mbele ya maiti na kumuuliza. Ewe Bilal! Je, uliondokewa na huruma na upendo kiasi cha kukufanya uwapitishe wanawake hawa mbele ya maiti za watu wao? Ni kwa nini ulifanya kitendo hiki kisicho cha huruma?'

Licha ya kuwa Bilal alikuwa na nafasi muhimu, maalumu na ya kuheshimika sana mbele ya Mtume (as) lakini alikemewa na Mtume na kusisitiziwa kwamba wafungwa wanapasa kuonyeshwa huruma na mapenzi kwa msingi wa mafundisho ya Kiislamu.

*********

Ama kuhusu suala la kusahilisha ibada, Imepokelewa katika kitabu cha al-Kafi kutoka kwa Abu Ja'ffar al-Imam Muhammad Baqir (as) kwamba alisema: 'Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: 'Hakika kila ibada ina nishati na uchangamfu wake ambao hatimaye hutulia na kupungua. Hivyo kila mtu ambaye uchangamfu na nishati ya ibada yake hupungua kwa mujibu wa suna yangu, huwa ameongoka la sivyo, kila anayepinga suna yangu hupotea njia na amali zake kuwa kazi bure isiyokuwa na maana. Jueni kwamba mimi huswali, hulala, hufunga swaumu, hufuturu, hucheka na kulia. Hivyo, kila anayepinga mwenendo na suna yangu, si katika mimi.'

 

Wapenzi wasikilizaji, na katika suna za Mtume Mtukufu (saw) ni kusahilisha mambo katika ibada kama anavyowatakia waja wake Mwenyezi Mungu Subhanahu wa Taala. Hivi ndivyo zinavyotuelekeza Hadithi nyingi za Kiislamu ambapo tutaashiria baadhi hapa. Badhi ya Hadithi hizo ni zile zilizoashiriwa na Sheikh Swadouq katika kitabu chake cha Man La Yahdhuruhu al-Faqih akimnukuu Imam Swadiq (as) aliyesema: 'Mtume (saw) alikuwa akiswali faradhi juu ya ngamia wake siku ya mvua.'

Na Hadithi ya pili imepokelewa kutola kwa Ibrahim al-Karkhi ambaye anasema: 'Nilimwambia Aba Abdillah al-Imam as-Swadiq (as): Hakika mimi ninaweza kuelekea upande wa Kibla hata nikiwa juu ya kipandio. Imam (as) akamwambia: Huu ni usumbufu, kwani hamna ruwaza njema (mfano mwema wa kuiga) kwa Mtume (saw)?'

Tunasoma Riwaya nyingine ambayo imepokelewa na Hurr al-Amili katika juzuu ya nne ya kitabu chake cha Wasail as-Shia akimnukuu Hammad bin Isa ambaye anasema: 'Nilimsikia Aba Abdillah as-Swadiq (as) akisema: Mtume (saw) alitoka kuelekea Tabuk na kuswali Swalat al-Leil (swala ya usiku) huku akiwa juu ya kipandio chake (ngamia) na kuendelea na swala bila kujali upande kilioelekea, na kufanya 'imaa' (kutoa ishara katika rukuu na sijda).'

***************

Na katika kitabu cha Kashf al-Ghumat fi Ma'rifat al-Aimma cha Allama Ali bin Isah kuna Hadithi ambayo imepokelewa kupitia Faidh bin Matar anayesema: 'Nilienda kwa baba yake Ja'ffar al-Imam Baqir (as) huku nikiwa na nia ya kumuuliza swali kuhusiana na swala ya usiku juu ya kipandio ( mara nyingine chumba kinachowekwa kwenye kipandio) naye akawa ameniwahi kwa kusema: Mtume (saw) alikuwa akiswali akiwa juu ya kipandio na kuendelea na swala bila kujali kilikoelekea.'

**********

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu hiki cha Ruwaza Njema kwa juma hili, kipindi ambacho kimekujieni kupitia Idhaa y kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni matumaini yetu kwamba mmenufaika vya kutosha na yale tuliyokuandalieni. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

 

Tags