Sep 29, 2019 06:04 UTC
  • Ruwaza Njema (27)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Tuna furaha kukutana nanyi tena katika makala nyingine ya kipindi hiki cha Ruwaza Njema, hii ikiwa ni sehemu ya 27 ya kipindi hiki.

Kwa leo tatazungumzia kwa ufupi moja ya hutuba za Imam Ali (as) ambayo ndani yake mna maneno mazito kuhusiana na udharura wa kuiga na kumfuata Mtume Mtukufu (saw) katika kuepuka anasa na matamanio ya kidunia, na vilevile kuonyesha upole, huruma na kuwatakia heri wanadamu.

Hivyo tunakuombeni muwe nasi hadi mwisho wa kipindi, karibuni.

*********

Imam Ali (as) anasema katika hotuba  ya 160 kati ya hutuba zake ambazo zimenukuliwa katika kitabu cha Nahjul Balagha kama inavyofuata:

'Hali ni kama hivyo kwa yule ambaye dunia imemuia kubwa machoni pake, na nafasi yake (dunia) kuwa na umuhimu moyoni mwake, huichagua dunia na kumuacha Mwenyezi Mungu. Hivyo huachana na kila kitu, kujiunga na dunia na hatimaye kuwa mtumwa wake. Na hakika Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) anatosha kuwa mfano bora kwako na ni dalili ya kukuwezesha kuipuuza dunia na kuibeza, kwa sababu ya wingi wa aibu na mabaya yake, kwa kuzingatia kwamba pande zake zilibanwa mbali naye (Mtume Mtukufu) hali ya kuwa wengine waliachiwa fursa ya kunufaika nazo.  Alikatishwa kunyonya kwake na kukatazwa mapambo yake. Bali muige Nabii wako mzuri aliye safi (saw) kwani kwake yeye kuna mifano kwa anayefuata mfano, na ni ushauri kwa kwa anayefuata ushauri, na mja mpendwa mno kwa Mwenyezi Mungu ni yule mwenye kuiga mfano wa Nabii wake, na anayefuata nyayo zake. Alichukua kutoka katika dunia hii kiasi kidogo (cha haja) wala hakuitupia jicho kwa kiwango kikubwa. Ni mwenye tumbo tupu mno katika watu wa dunia hii, na aliyekuwa na tumbo lililo boba mno. Alipewa dunia na akakataa kuikubali. Alipojua kwamba Mwenyezi Mungu anakichukia kitu fulani, naye alikichukia, akikidunisha naye alikidunisha na akikidogesha naye alikidogesha. Lau hakungekuwa katika sisi ila kupenda kwetu alichokichukia Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, na kuadhimisha kwetu alichokidogesha Mwenyezi Mungu na Mtume Wake, hilo lingetosha kuwa ni kujiweka mbali na Mwenyezi Mungu na kukiuka amri yake. Hakika Mtume (saw) alikuwa akilia chini (sakafuni) na akikaa kwa unyenyekevu kama anavyokaa mtumwa na akivitengeneza viatu vyake kwa mkono wake. Alikuwa akitia kiraka nguo yake yeye mweneyewe, akipanda punda asiye na tandiko na kumpakia mtu nyuma yake. Ikiwa kulikuwa na pazia lenye picha kwenye mlango wa nyumba yake alikuwa akimwambia mmoja wa wake zake: Ewe funali! Iondoe mbali na mimi kwa kuwa nikiiangalia nitakumbuka dunia na mapambo yake. Akawa anaipa kisogo dunia moyo wake na akaifisha kumbukumbu yake nafsini mwake. Alipenda mapambo yake yatokomee mbali na macho yake ili asichukue humo vazi na pambo, hivyo basi akaitoa nje ya mazingatio yake, akaifanya itoweke moyoni mwake na kuifanya ifichike mbali na macho. Na kadhalika mwenye kuchukia kitu huchukia kukiangalia na kutajwa mbele yake.

 

Wapenzi wasikilizaji, tunaendelea kubakia na Bwana wa Wanaomuiga Mtume (saw) ambaye si mwingine bali ni Amir al-Mu'mineen Ali (as) ambaye anamalizia hutuba hii kwa kusema:

Kwa Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) kulikuwa na kila liwezalo kukujulisha (kukuonya dhidi ya) maovu ya dunia na aibu zake pale aliposhikwa na njaa licha ya nafasi yake (mbele ya Mola wake) pamoja na umahususi wake. Na yamewekwa mbali na yeye mapambo yake, hali akiwa na utukufu mno wa ukaribu. Hivyo basi mwangaliaji na aangaliye kwa akili yake: Je, Mwenyezi Mungu amempa heshima Muhammad kwa hilo au amemdhalilisha?!

Ikiwa atasema: Amemdhalilisha, kwa kweli atakuwa amesema uongo na akisema amempa heshima, basi ujue kwamba Mwenyezi Mungu amemtweza mwingine, kwa kumkunjulia dunia na kuikunja mbali na mtu aliye karibu sana na Yeye. Na amfuate mfuataji Nabii wake, akanyage alipokanyaga na aingine alipoingia, vinginevyo hatonusurika dhidi ya maangamizi. Kwa hakika Mwenyezi Mungu amemfanya Muhammad (saw) kuwa ni alama ya Kiayama (kwa kuwa hakuna mtume mwingine baada yake), na ni mbashiriaji wa Pepo na muonyaji dhidi ya adhabu. Ameiaga dunia hali akiwa tumbo tupu, na kuwasili Akhera akiwa salama. Hakuweka jiwe juu ya jiwe jingine mpaka alipoenda njia yake (alipofariki), aliitikia wito wa muitaji wa Mola wake. Utukufu ulioje wa Baraka za Mwenyezi Mungu kwetu pindi alipotuneemesha kupitia yeye (Mtume saw) akiwa mtangulizi tunayemfuata na kiongozi ambaye tunakanyaga kisigino chake (kufuata mwenendo wake). Naapa kwa Mwenyezi Mungu! Nimeweka viraka kanzu yangu hii hadi nikamuonea haya muweka viraka. Mtu mmoja aliniambia: 'Je, huitupi?!' Nikasema: Niondokee, wakati wa asubuhi watu watausifu mwendo.'

 

Allama Sayyid Hashim al-Bahrani amenukuu Hadithi ifuatayo katika juzuu ya kwanza ya kitabu chake kinachoitwa Hulyatul Abrar: 'Walimpoleta mtoto mchanga mbele ya Mtume Mtukufu (saw) kwa ajili ya kumuombea dua au kumpa jina, Mtukufu huyo alikuwa akimpakata mtoto huyo ili kuonyesha heshima kwa familia yake ambapo mara nyingine mtoto huyo alikuwa akimkojolea Mtume (saw), na hali hiyo kupelekea mmoja wa waliokuwa karibu naye kupiga mayowe akimkemea. Mtume (saw) alikuwa akiwaambia: Msimzuie mtoto kukujoa. Alikuwa akimwacha mtoto amalize kukojoa na kisha kumuombea dua au kumpa jina. Kwa kitendo hicho familia ya mtoto yule ilikuwa ikifurahi na kutambua kuwa Mtume hakukasirishwa na kitendo cha mtoto wao kumkojolea. Mtume (saw) alikuwa akiosha na kutwahirisha nguo yake baada ya wao kuondoka.'

Katika Riwaya nyingine inayofanana na hii, Mtume (saw) amesema: 'Nguo yangu itatahirika kwa maji, ama je, ni kitu gani kinachoweza kufuta vumbi ambalo mnaliweka kwenye moyo wa mtoto?!'

**********

Ndugu wasikilizaji, na tunasoma katika juzuu ya 16 ya kitabu cha Bihar al-Anwar Riwaya ambayo imenukuliwa na Allama al-Majlisi (MA) inayosema: 'Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) alikuwa ameketi kwenye msikiti ambapo mtu mmoja aliingia msikitini naye Mtume (saw) akawa amemuinukia kama ishara ya heshima kwake. Mtu yule akasema: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Kuna nafasi kubwa na pana tu. Mtume akasema: Ni haki ya Mwislamu kwa Mwislamu mwenzake anapomwona amemkaribia kuketi chini, amuinukie na kusonga kando kidogo ili kumpa nafasi ya kuketi (alama ya heshima).'

Jurair bin Abdallah amenukuliwa katika kitabu cha Makarim al-Akhlaaq akisema: Mtume (saw) alipobaathiwa, nilifika mbele yake naye akaniuliza: Ewe Jurair! Je, umekuja kufanya nini? Nikasema: Nimekuja ili nisilimu kupitia kwako ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Hapo akanitupia shuka na kisha kuwaambia masahaba zake: anapokujieni kiongozi wa kaumu fulani, mkirimuni.'

 

Na hatimaye wapenzi wasikilizaji tunazingatia kwa pamoja Hadithi ifuatayo ya Mtume wetu Mtukufu (saw) akiwatakia heri, Baraka na fanaka wasafiri. Sheikh Swadouq (MA) amenukuu katika kitabu chake cha Man La Yahdhuruhu al-Faqih kwamba Imam Baqir (as) alisema: 'Mtume (saw) alipokuwa akimuaga msafiri alikuwa akiushika mkono wake na kumuombea dua kama inavyofuata: Mwenyezi Mungu akupe mwenza mwema safarini, ukusaidie kikamilifu na kukusahilishia misukosuko. Akukaribishie yaliyo mbali, akukidhie haja zako, akulindie dini na amana yako na kufanya mwisho wako uwe mzuri. Akuongoze kwenye kila la heri na zingatia takwa ya Mwenyezi Mungu. Mtegemee Mwenyezi Mungu na anza safari yako huku ukiwa unamtumainia Mwenyezi Mungu Mtukufu.'

**********

Na hadi hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Ruwaza Njema ambacho kimekujieni moja kwa moja kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Ni matumaini yetu kuwa mmenufaika vya kutosha na yale tuliyokuandalieni kwa juma hili. Basi hadi tutakapokutana tena katika kinpindi kingine cha Ruwaza Njema, tunakuageni nyote kwa kusema, Wassalaam Aleikum Warahmatullahi Wabarakatuh.

Tags