Rais wa Iran: Kupunguza mvutano katika eneo kunahitaji kutounga mkono wavamizi
https://parstoday.ir/sw/news/iran-i137258-rais_wa_iran_kupunguza_mvutano_katika_eneo_kunahitaji_kutounga_mkono_wavamizi
Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kwamba juhudi za wale walioanzisha uchokozi dhidi ya Iran zimekuwa zikilenga kupandikiza mifarakano kati ya mataifa jirani. Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imeonyesha utayari wake wa kupunguza mvutano katika eneo hili, mradi tu anga, ardhi na maji ya mataifa jirani yasitumike kama njia ya kushambulia watu wa Iran.
(last modified 2026-03-10T03:59:55+00:00 )
Mar 10, 2026 03:59 UTC
  • Rais wa Iran: Kupunguza mvutano katika eneo kunahitaji kutounga mkono wavamizi

Rais wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema kwamba juhudi za wale walioanzisha uchokozi dhidi ya Iran zimekuwa zikilenga kupandikiza mifarakano kati ya mataifa jirani. Amesisitiza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imeonyesha utayari wake wa kupunguza mvutano katika eneo hili, mradi tu anga, ardhi na maji ya mataifa jirani yasitumike kama njia ya kushambulia watu wa Iran.

Kwa mujibu wa Shirika la Habari la IRIB, Rais Masoud Pezeshkian wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na Rais Recep Tayyip Erdoğan wa Uturuki walifanya mazungumzo kwa njia ya simu jioni ya Jumatatu,  wakijadiliana kuhusu mwenendo wa matukio katika eneo hili kufuatia uchokozi wa kijeshi wa Marekani na utawala wa Kizayuni dhidi ya Iran, pamoja na athari na matokeo yake katika ngazi ya kikanda na kimataifa.

Katika mazungumzo hayo, Pezeshkian ameashiria juhudi za utawala wa Kizayuni na serikali ya Marekani za kujaribu kuleta mifarakano kati ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na majirani zake, pamoja na tuhuma zilizotolewa na vyombo vya habari vinavyohusishwa nao zikidai kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanya mashambulizi ya makombora dhidi ya nchi rafiki na ndugu, Uturuki. Amesema: Jamhuri ya Kiislamu ya Iran daima imekuwa tayari kupunguza mvutano katika eneo hili, kwa sharti kwamba nchi hizo zisitumike kama njia ya kushambulia wananchi wa Iran.

Rais pia alitoa shukrani kwa misimamo ya nchi rafiki na ndugu ya Uturuki, pamoja na juhudi zake za kuchangia upatikanaji wa amani na utulivu katika eneo hili. Aidha, ameishukuru serikali ya Uturuki  kwa kutuma salamu za rambirambi kufuatia kuuawa shahidi kwa Kiongozi Muadhamu mwenye heshima kubwa pamoja na idadi ya raia wasio na hatia.

Ameongeza kuwa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran iko tayari kuondoa sintofahamu kuhusu madai ya mashambulizi ya makombora dhidi ya Uturuki, kuunda timu ya pamoja ya uchunguzi itakayopitia madai yanayotolewa na nchi na tawala zilizo na uhasama na Iran, ili kuhakikisha kuwa daima uhusiano wa nchi hizi mbili rafiki na ndugu hauathiriwi na propaganda za vyombo vya habari.

Rais wa Uturuki, Recep Tayyip Erdoğan, katika mazungumzo hayo ya simu ametoa tena salamu za pole kufuatia kuuawa shahidi kwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi. Aidha amebainisha  masikitiko na rambirambi zake kwa kuuawa kwa idadi kubwa ya raia wasio na hatia, hususan watoto wasio na ulinzi wa Shule ya Minab.

Rais wa Uturuki pia alimtakia mafanikio Ayatullah Mojtaba Khamenei kama Kiongozi mpya wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran.

Akiashiria kuendelea kwa juhudi za serikali ya Uturuki za kupunguza mvutano katika eneo hili, Erdoğan amesisitiza: Tumekuwa tukitangaza katika kila fursa kwamba kuingilia mambo ya ndani ya Iran hakukubaliki, na kuongezeka kwa mvutano kati ya nchi za eneo hili hakunufaishi maslahi ya majirani wala maslahi ya muda mrefu ya Iran.

Rais wa Uturuki ameongeza kuwa: Hatufikirii kamwe kukabiliana na Iran kwa namna yoyote ile. Tunaelewa hali ngumu inayokabili Iran, na tuko tayari, kadiri inavyowezekana kwa uwezo wa serikali ya Uturuki, kushiriki katika juhudi za kupunguza mvutano katika eneo hili.

Erdogan amemaliza kwa kusema: Katika wakati huu nyeti, kuna haja zaidi kuliko wakati mwingine wowote wa kufungua milango ya diplomasia.