Sep 29, 2019 06:08 UTC
  • Ruwaza Njema (28)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikiliza na karibuni kusikiliza kipindi kingine cha Ruwaza Njema ambacho kinakujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutanagazieni kutoka mjini Tehran.

Leo tutaendelea kama kawaida kuzungumzia Hadithi kadhaa tukufu zinazotunasihi tuige na kumfuata Mtume Mtukufu (saw) katika matendo na tabia zake zote. Kipindi chetu cha leo kitazungumzia tabia na ushauri wa Mtume (saw) katika kuwapa watoto wetu majina mazuri na ya kupendeza bali kuyabadilisha yaliyo mabaya na mazuri, na vilevile udharura wa kulinda heshima ya watu na kuepuka mambo yanayowaudhi, karibuni.

*********

Tunaanza wapenzi wasikilizaji kwa kunukuu Hadithi kutoka kitabu cha Qurb al-Isnaad ambayo imepokelewa kutoka kwa Imam Swadiq (as) ambaye anasema: 'Daima Mtume (saw) alikuwa akiyabadilisha majina mabaya ya wanaume na miji.'

Na Sheikh Swadouq ananukuu katika kitabu chake cha Uyun Akhbar ar-Ridha (as) Hadithi kutoka kwa mtukufu huyo kwamba alisema: 'Mtume (saw) alimpa jina Hassan siku ya saba - yaani tokea azaliwe – na kutoa (kunyambua) katika jina hilo jina la Hussein.'

Na Sheikh Swadouq (MA) pia amenukuu katika kitabu cha Ilal as-Sharai'

Kutoka kwa mtukufu huyo (as) kwamba Mtume (saw) alisema: 'Msiwaite watoto wenu 'al-Hakam' wala 'Abul Hakam' kwa kuwa Mwenyezi Mungu ndiye 'al-Hakam.'

Pia Mtume (saw) amenukuliwa katika kitabu cha al-Aamali cha Sheikh at-Tousi akisema: 'Hakuna familia yoyote iliyo na mtu aliyetajwa jina la Nabii ila Mwenyezi Mungu hutuma katika familia hiyo Malaika ambaye huwatakasa – yaani huwalinda na kuwaombea dua - asubuhi na usiku.'

 

Wapenzi wasikilizaji, na tunasoma katika kitabu cha al-Muntakhab cha Allama at-Turaihi (MA) ambaye amenukuu Hadithi ndefu inayosema kwamba Mkristo mmoja alifika mbele ya Mtume Mtukufu (saw) naye akamuuliza: 'Unaitwa nani? Akamjibu: Ninaitwa 'Abdushams'. Mtume (saw) akamwambia: Badilisha jina lako; mimi nitakuita 'Abdulwahhab.'

Na imenukuliwa katika kitabu cha Mizan al-Hikma kwamba mtu mmoja alifika mbele ya Mtume (saw) naye akamuuliza: 'Unaitwa nani? Akajibu: Ninaitwa 'Bughaidh' (linalotokana na chuki) ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu!..... Mtume (saw) akamwambia bali wewe ni Hubaib, (linalotokana na upendo)  na hapo akawa amemwita jina hilo la Hubaib'.

Na tunasoma katika juzuu ya 21 ya kitabu cha Jamiu al-Ahadith as-Shia Hadithi inayohusiana na sahaba mwema Salman al-Muhammadi (Salman al-Farisi) (MA) na ambayo imepokelewa kutoka kwa Imam Musa al-Kadhim (as) kwamba: 'Hakika Salman alikuwa akiitwa 'Ruzbeh' na Mtume (saw) akamnunua kutoka kwa mwanamke mmoja wa Kiyahudi kwa mitende mia nne (400). Salman akasema: Mtume (saw) akaniacha huru na kuniita 'Salman'.'

Na hatimaye tunasoma Hadithi iliyonukuliwa na Sheikh Ibn Fahd al-Hilli katika kitabu cha Uddat ad-Daai' kwamba mtu mmoja alifika kwa Mtume (saw) akiwa ameandamana na mwanaye na kumuuliza: 'Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Mwanangu huyu ana haki gani (kwangu)? Mtume (saw) akamjibu: Umpe jina zuri, umfunze tabia njema na kumuweka mahala pema!'

********

Na Allama Tabarsi (MA) anasema katika kitabu chake mashuhuri cha Makarim al-Akhlaaq: 'Imepokelewa kwamba Mtume (saw) hakuwa akimruhusu mtu yeyote kutembea kwa miguu pembeni yake hali ya kuwa yeye amepanda kipandio bali alikuwa akimuomba apande pamoja naye na alipokataa, alikuwa akimwambia: Basi wewe tangulia na ukifika mahala fulani nisubiri hapo ili ukiwa na jambo tupate kulizungumzia hapo. Na Mtume (saw) alialikwa na watu fulani wa mji wa Madina kwa chakula alichokuwa ametayarishiwa yeye na masahaba wake watano. Walipokuwa njiani sahaba wa sita alijiunga nao na wakawa wanaelekea kwenye mwaliko pamoja. Walipokaribia nyumba ya watu hao, Mtume (saw) alimwambia sahaba huyo wa sita: watu hawa hawakukualika wewe hivyo keti hapa ili tuwajulishe na tupate kukuombea idhini.'

Mtume (saw) alikuwa akiwaheshimu watu wote hata katika kuwatazama usoni ambapo daima alikuwa ni mwingi wa kutabasamu alipokutana nao na kuwakaribisha katika vikao tofauti. Kuhusiana na hilo Jurair bin Abdallah anasema kwamba hakuna wakati wowote ambao alikutana na mtukufu huyo bila yeye Mtume (saw) kumtabasamia.  Ni kweli inaposemekana kwamba Mtume (saw) alikuwa ni mwingi wa kutabasamu kumliko mtu mwingine yeyote.

 

Tunasoma katika kitabu cha al-Mahasin cha Sheikh al-Barqi (MA) ambapo ananukuu Hadithi iliyopokelewa na Naufali kuhusiana na tabia njema na ya kupigiwa mfano ya Bwana Mtume (saw) ya kuwaombea dua watu waliomwalika kwa chakula kwa kusema: 'Mtume (saw) alipokula chakula katika nyumba yoyote ile, alikuwa akiwaombea dua watu wa nyumba hiyo kwa kusema: 'Wanaofunga saumu wapate kula kwenu, wakule pamoja nanyi watu wema na wakuswalieni Malaika wateule.'

Na tunasoma katika kitabu hicho hicho mfano mwema wa Maimamu Watoharifu (as) ambao wanafuata mfano mwema wa Bwana wao Mtume (saw) katika jambo hilo. Abu Abdallah as-Samman amenukuliwa katika kitabu hicho akisema kwamba alimpelekea chakula Imam Swadiq (as) na wakawa wanakula pamoja chakula hicho. Alipomaliza kula, Imam (as) alisema: Alhamdulillah, na kumwambia: 'Watu wema wapate kula chakula chako na wakuswalie Malaika wateule.'

Na hatimaye tunasoma katika kitabu hicho hicho Hadithi ambayo imepokelewa kutoka kwa Imam Muhammad Baqir (as) kwamba alisema: 'Mtume (saw) alipokula chakula na watu, alikuwa wa kwanza kuanza kula na wa mwisho kumaliza kula ili watu wapate kula.'

************

Na kufiki ahapa wapezi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Ruwaza Njema kilichokujieni kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapojaliwa kukutana tena katika kipindi kingine, tunakuageni nyote kwa kusema, kwaherini.

 

Tags