Sep 29, 2019 05:55 UTC
  • Ruwaza Njema (25)

Assalaama Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu inayokutangazieni kutoka mjini Tehran.

Karibuni kusikiliza sehemu hii ya 25 ya mfululizo wa vipindi hivi vya Ruwaza Njema ambavyo hujadili tabia njema na mienendo ya kuvutia ya Bwana Mtume (saw) ambapo sote Waislamu tunatakiwa na maandiko matakatifu kuifuata mienendo hiyo. Katika kipindi cha leo tutazungumzia sifa ya Mtume ya kutowakatisha tamaa watu wanaoomba kukidhiwa haja zao na kufanya urafiki na kuwakirimu wenzetu, karibuni. Tunaanza na Hadithi iliyonukuliwa na mtaalamu wa maarifa ya Qur'ani, al-Allama Tabarsi katika kitabu chake cha Makarim al-Akhlaaq. Hadithi hiyo imepokelewa na Ibn Abbas kutoka kwa Mtume Mtukufu (saw) kwamba alisema: 'Mimi nimefundishwa adabu na Mwenyezi Mungu naye Ali akajifunza adabu kutoka kwangu mimi. Mola wangu ameniamuru kuwa mkarimu na kutenda mema na kunikataza kufanya ubakhili na kuwa mkali (dhalimu). Hakuna jambo linalomchukiza Mwemnyezi Mungu kama kuwa bakhili na mwenye tabia mbaya, kwa sababu mawili haya huharibu mambo mema ya mwanadamu kama inavyoharibu siki asali.'

***********

Wapenzi wasikilizaji na tazameni hapa jinsi Mtume Mtukufu (saw) alivyokuwa mkarimu hata mbele ya shekhe na kiongozi wa watu waliosamehewa na kuachwa huru baada ya kutekwa mji mtakatifu wa Makka kutoka mikononi mwa makafiri wa mji huo, makafiri na mushrikina waliotesa na kumuudhi Mtume (saw) kwa kila njia waliyoweza. Kiongozi huyo si mwingine bali ni Abu Sufyan. Imepokelewa katika kitabu cha Makarim al-Akhlaaq kutoka kwa Ibn Abbas kwamba alisema: 'Waislamu hawakuwa wakimtazama wala kuketi na Abu Sufyan. Akafika mbele ya Mtume (saw) na kumwambia: Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Ninakuomba mambo matatu, je utanikubalia? Mtume (saw) akasema: Nam. Akasema (Abu Sufyan) Nina binti mwema na mrembo zaidi wa Kiarabu kwa jina la Umu Habiba bint Abu Sufyan. Ninataka kukuoza, je, utamkubali? Mtume akajibu: Nam. Akasema: Umfanye Muawiyya kuwa mmoja wa waandishi wa Wahyi; Mtume (saw) akajibu: Nam. Akasema (Abu Sufya): Unifanye kuwa kamanda ili nipate kupigana na makafiri kama nilivyopigana na Waislamu. Mtume (saw) akakubali. Abu Zumail akasema, kama Abu Sufyan asingelimwomba Mtume (saw) mambo hayo, asingempa, kwa sababu hakuombwa jambo lolote ila alikuwa akilikubali.'

 

Ndugu wasikilizaji, tunaashiria Hadithi hii nyingine ambayo imenukuliwa na mtaalamu wa Hadithi al-Hussein bin Said al-Kufi katika kitabu cha az-Zuhd kutoka kwa Abu Abdallah al-Imam as-Swadiq (as) kwamba alisema: 'Siku moja Mtume (saw) alipita karibu na mtu mmoja kutoka ukoo wa Bani Fahd ambaye alikuwa akimuadhibu na kumpiga mtumwa wake ambaye kutokana na makali ya mateso alikuwa akipaza sauti kwa kusema: Ninajikinga na Mwenyezi Mungu. Pamoja na hayo lakini bwana wake huyo hakumuacha bali aliendelea kumpiga. Mtumwa yule alipomwona Mtume (saw) akawa anapaza sauti kwa kusema: Ninajikinga na Muhammad (saw). Alipoyasikia maneno hayo bwana yule akawa ameacha kumpiga mtumwa huyo. Hapo Mtume akasema: Je, anajikinga na Mwenyezi Mungu huku anaendelea kumpiga na kumwacha anapojikinga na Muhammad?!! Mwenyezi Mungu ndiye kimbilio bora zaidi kumliko Muhammad. Hapo mtu huyo akasema: Nimemwachilia huru kwa ajili ya Mwenyezi Mungu. Hapo Mtume (saw) akasema: Ninaapa kwa jila la Yule aliyeniteua kwa haki kuwa Nabii, kama usingefanya hivyo uso wako ungekumbwa na joto kali la moto wa Jahannam.'

****************

Ama kuhusiana na suala la kuwa na miamala mizuri pamoja na kuwakirimu wenzetu, Allama Tabarsi ananukuu katika kitabu chake cha Makarim al-Aklaaq Hadithi kadhaa zinazozungumza na kubainisha vyema suala hilo linalotokana na mafundisho ya Bwana Mtume (swa) ambaye tunatakiwa kumuiga kama ruwaza njema. Ibn Abbas amenukuliwa akisema katika kitabu hicho: 'Mtume (saw) alipozungumzia au kuuliza suala fulani, alikuwa akilikariri mara tatu ili lifahamike vyema na kutokuwa na hali yoyote ya kutofahamika vizuri'

Na mtu mmoja amenukuliwa akimwambia Mtume (saw): 'Ewe Mtume wa Mwenyezi Mungu! Naye Mtume (saw) akamjibu kwa kusema: 'Labbaika'. Naye Zaid bin Thabit anasema: 'Kila mara tulipokaa na Mtume (saw) na kuamua kuzungumzia suala la Akhera, yeye pia alikuwa akiamua kulizungumzia suala hilo hilo, na tulipozungumzia dunia yeye pia alizungumzia suala hilo hilo na tulipozungumzia chakula na kinywaji naye pia lifanya hivyo hivyo.'

Image Caption

 

Tunazingatia kwa pamoja wapenzi wasikilizaji njia bora aliyoitumia Mtume (saw) katika kukosoa na kulaumu mtu ilipobidi kufanya hivyo kwa kutumia sifa nzuri ya 'kijana' kwa yule aliyemkosoa. Abdullah bin Abu al-Humaisaa amenukuliwa katika kitabu tulichotangulia kukitaja cha Makarim al-Akhlaaq kwamba alisema: 'Nilimfuata Mtume (saw) kabla ya kubaathiwa kwake na kuahidiana naye tukutane sehemu fulani, lakini mimi nikawa nimesahau ahadi hiyo. Siku tatu zikawa zimepita nami nikaharakisha kwenda sehemu ile. Nilimkuta Mtume hapo naye akasema: Ewe kijana! Umenitia kwenye tabu. Nimekusubiri hapa kwa muda wa siku tatu.'

Hatupasi kusahau kuashiria hapa umuhimu mkubwa aliokuwa akilipa Mtume (saw) suala la kutekeleza ahadi kama tulivyoona katika Riwaya hii tukufu. Riwaya hii inabainisha wazi subira na ukarimu mkubwa aliouonyesha Mtume kwa watu wengine.

Imepokelewa kutoka kwa Salman al-Farisi kuwa alisema: 'Niliingia kwa Mtume (saw) hali ya kuwa ameegemea kwenye takia.  Alinipa takia hilo na kusema: 'Ewe Salman! Haingii Mwislamu yoyote kwa ndugu yake Mwislamu naye akampa takia kwa kumkirimu ila Mwenyezi Mungu humsamehe dhambi zake.'

**********

Na kwa Hadithi hiyo wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi chetu hiki cha Ruwaza Njema kwa juma hili. Tunatumai mmepata kunufaika vya kutosha na yale tuliyokuandalieni kwenye kipindi hiki. Basi hadi tutakapojaaliwa kukutana tena wiki ijayo tunakuageni nyote kwa kusema, kwaherini.

 

Tags