Sep 18, 2019 11:29 UTC
  • Ruwaza Njema (21)

Assalaam Aleikum wapenzi wasikilizaji wa Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na karibuni kusikiliza sehemu ya 21 ya kipindi hiki cha Ruwaza Njema ambacho kinakujieni kutoka mjini Tehran.

Leo tutaangazia Hadithi nyingine ambazo zinatuasa na kutushauri tufuate mfano mwema wa Mtume Mtukufu (sw) katika kuwa wapole (kuwa na huruma) na kukijali kila kiumbe ambacho kimeumbwa na Mwenyezi Mungu na hasa wanyama na vilevile kuwa shujaa mbele ya maadui na wakati huohuo kuonyesha unyenyekevu wa hali ya juu mbele ya Mwenyezi Mungu Muumba. Tunaanza na Hadithi ambayo imenukuliwa na Sheikh Barqi (MA) katika kitabu chake cha al-Mahasin kutoka kwa Imam Ali (as) ambaye anasema: 'Mtume wa Mwenyezi Mungu (saw) amesema: Hakika Mwenyezi Mungu anapenda upole na husaidia katika upole huo. Hivyo basi mnapowapanda wanyama waliokonda, waacheni wapumzike kwenye vituo maalumu vya mapumziko. Iwapo ardhi ya karibu itakuwa kavu isiyokuwa na malisho, basi piteni hapo kwa haraka na iwapo itakuwa na kijani kibichi na malisho ya kutosha waacheni wapumzike hapo (yaani ili wapete fursa ya kula malisho hayo).'

Na imepokelewa Hadithi katika kitabu cha Mustadrak al-Wasail cha Muhaddith Ayatullah an-Nuri (MA) kutoka kwa Imam Ali bin Abi Talib (as) ambaye anasema: 'Mtume Mtukufu (saw) alisema: Niliingia peponi na kuona huko mtu aliyevunja kiu cha mmbwa wake kwa maji.' Imam Ali (as) pia amepokelewa katika sehemu nyingine akisema: 'Mtume (saw) alipokuwa akitawadha, paka alifika mbele yake na Mtume (saw) akafahamu kuwa mnyama huyo alikuwa na kiu. Alichukua chombo kilichokuwa na maji na kukiweka mbele ya paka huyo. Baada ya paka kuvunja kiu chake, Mtume (saw) alichukua maji yaliyobaki na kuyachukulia udhu.'

Hakika nyinyi mnayo ruwaza njema kwa Mtume wa Allah kwa anayemtaraji Mwenyezi Mungu na Siku ya Mwisho, na akamkumbuka Allah sana. (Surat al Ahzab, 33:21)

 

Ndugu wasikilizaji, tunasoma katika kiyabu cha Makarim al-Akhlaq cha Sheikh Tousi Hadithi ambayo imepokelewa kutoka kwa as-Sakwini kwamba: 'Mtume (saw) alimwona ngamia mmoja wa kike akiwa amefungwa miguu hali ya kuwa mizigo ingali mgongoni kwake. Mtume akauliza, je, mwenye ngamia huyu yuko wapi? (Aambiwe) ajitayarishe kesho (Siku ya Kiama) kwa ajili ya kushtakiwa na ngamia huyu.' Kisha mpokezi wa Hadithi anasema: 'Ali bin al-Hussein (as) alikwenda Hija mara arubaini kwa kutumia ngamia wake lakini hakuwahi kumpiga (kwa kutumia mjeledi au fimbo) hata mara moja.'

Na hatimaye tunasoma katika kitabu cha al-Ikhtisaas cha Sheikh al-Mufid (MA) kisa cha kuvutia kifuatacho mbacho kinadhihirisha wazi tabia ya Maimamu Watoharifu ya kufuata kila jambo kutoka kwa Bwana wao, Muhammad al-Mustafa (saw). Imepokelewa kutoka kwa Imam Ja'ffar as-Swadiq (as) kwamba alisema:  'Siku moja Ali bin Hussein (as) alikuwa njiani na masahaba zake wakielekea Makka kuhiji. Walipokuwa wameketi kwa ajili ya kula chakula cha mchana mbweha mmoja alipita karibu nao naye Imam Ali bin Hussein (as) akawauliza, je, mnaahidi kwamba hamtaudhi wala kumpigia kelele mbweha huyo iwapo nitamwita aje tulipo? Wakaahidi na kuapa kuwa hawangemuudhi wala kumpigia kilele. Imam alimwita yule mbweha kwa kumwambia: Ewe Mbweha, njoo kwetu! Mbweha yule alikaribia na kuketi pembeni ya Imam Ali bin Hussein (as). Hapo Imam akachukua mfupa na kuuweka mbele ya mbweha, naye akawa anashughulika kuula. Kisha akasogea mbali kidogo. Imam (as) akawaambia masahaba: Ikiwa mtaniahidi na kumfanya Mwenyezi Mungu kuwa shahidi wa hilo, nitamwita tena mbweha huyu arejee hapa. Masahaba wakakubali jambo hilo. Baada ya Imam Sajjad kumwita tena, mbweha yule alirejea alipokuwa mbeleni yaani kando ya kundi hilo la masahaba. Ghafla mtu mmoja kwenye kundi hilo akawa anamtazama yule mbweha kwa chukukia huku akiwa amemkunjia uso. Mbweha alipoona hivyo alikimbia kutoka mahala pale. Imam Sajjad akauliza: Je, ni nani kati yenu amevunja ahadi yetu? Mhusika akajibu: Ewe mwana wa Mtume! Mimi nilimkunjia uso mbweha huyo bila kujua, na ninaomba msamaha kwa Mwenyezi Mungu. Hapo Imam (as) akanyamaza.'

********

Allama Tabarsi (MA) amenukuliwa katika kitabu cha Makarim al-Akhlaq akisema: 'Imam Ali (as) amepokelewa akisema: Kama ungetuona siku ya vita vya Badr, tulikuwa tukimkimbilia Mtume Mtukufu wa Mwenyezi Mungu (saw) katika kipindi kigumu zaidi cha vita, ambapo alikuwa mtu wa karibu zaidi na adui kutuliko sisi huku akionyesha ushujaa na ujasiri mkubwa kutuliko sote.'

Pia Imam (as) amenukuliwa akisema katika sehemu nyingine: 'Vita vilipokuwa vikipamba moto na kufikia kilele, tulikuwa tukimkimbilia Mtume wa Mwenyezi Mungu na hakuna yeyote kati yetu sisi Waislamu aliyekuwa karibu zaidi na adui kumliko mtukufu huyo.'

Na Anas bin Malik amepokelewa akisema: 'Mtume Mtukufu (saw) alikuwa shujaa, mwema na mwenye kusamehe zaidi kuliko watu wote. Usiku mmoja wakazi wa mji wa Madina waliingiwa na hofu kubwa kutokana na sauti ya kutisha waliyoisikia. Baadhi ya watu waliamua kuelekea upande sauti ilikokuwa ikitokea. Njiani walikutana na Mtume ambaye tayari alikuwa amewatangulia kufika huko huku akiwa amepanda farasi wa Abu Talha na akiwa amebeba upanga wake begani. Aliwaona watu hao na kuwaambia: Msiogope! Msiogope!

 

Na Mtume Muhammad (saw) alikuwa mbora wa watu waliomnyenyekea zaidi Mwenyezi Mungu kama ambavyo alikuwa shujaa wa mashujaa wote. Tunasoma katika kitabu cha Sunan an-Nabi cha Allama Tabatabai, akinukuu kitabu cha Maj'maul Bayaan kwamba kila mara Mtume (saw) aliposikia sauti ya radi alikuwa akisema: 'Umetukuka Ewe ambaye radi inakutukuza kwa kukuhimidi!'

Kitabu hicho hicho kinaendelea kusema: 'Mtume (saw) alipokuwa akisikia sauti ya radi alikuwa akisema: 'Allahumma! Usituue kwa ghadhabu yako na wala usituhilikishe kwa ghadhabu yako na tusamehe kabla ya hapo.' Pia kinasema: 'Watu wa al-Ukhdud walipotajwa mbele yake Mtume (saw), alikuwa akijikinga na Mwenyezi Mungu kutokana na balaa.

*************

Na kufikia hapa wapenzi wasikilizaji ndio tunafikia mwisho wa kipindi hiki cha Ruwaza Njema ambacho mmekitegea sikio kupitia Idhaa ya Kiswahili, Sauti ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran inayokutangazieni kutoka mjini Tehran. Basi hadi tutakapokutana tena juma lijalo, siku na wakati mwingine kama huu panapo majaaliwa, tunakuageni nyote kwa kusema, kwaherini.

 

Tags