Ijumaa tarehe 20 Septemba 2019
Leo ni Ijumaa tarehe 20 Muharram mwaka 1441 Hijria inayosadifiana na tarehe 20 Septemba 2019.
Siku kama ya leo miaka 188 iliyopita, lilitengenezwa basi la kwanza lililokuwa likitumia nishati ya mvuke. Basi hilo lilikuwa na uwezo wa kubeba abiria 30 na kwenda kwa kasi ndogo na lilitengenezwa na Gordon Branz, raia wa Uingereza. Hii leo mabasi bora na ya kisasa ni miongoni mwa vyombo muhimu vya usafiri kote duniani.
Siku kama ya leo miaka 152 iliyopita, nchi ya Hungary iliungana na ardhi ya Austria na Francois Joseph akawa mtawala wa kifalme wa nchini mbili hizo. Hungary ambayo kwa mara kadhaa katika historia ilivamiwa na kukaliwa kwa mabavu na nchi zenye nguvu za Ulaya kama vile Austria na utawala wa Othmania, baadaye ilijipatia uhuru wake mnamo mwaka 1918 mwishoni mwa Vita vya Kwanza vya Dunia.
Siku kama ya leo miaka 40 iliyopita, Jean-Bedel Bokasa, dikteta wa Jamhuri ya Afrika ya Kati aliondolewa madarakani kupitia mapinduzi ya kijeshi. Bokasa alizaliwa mwaka 1922 na kusomea nchini Ufaransa. Alikuwa shabiki mkubwa wa Napoleon Bonaparte na Charles de Gaulle, viongozi wawili wa zamani wa Ufaransa. Alichukua madaraka ya Jamhuri ya Afrika ya Kati mwaka 1966 baada ya kufanya mapinduzi dhidi ya binamu yake, David Dacko, wakati Bokasa alipokuwa mkuu wa majeshi ya nchi hiyo. Jean-Bedel Bokasa alitawala nchi hiyo kwa mfumo wa kiimla na kwa kipindi cha miaka 13 na kusimamia moja kwa moja wizara 14 kati ya wizara 16 za nchi hiyo ya katikati mwa Afrika.
Na siku kama ya leo, miaka 8 iliyopita, aliuawa , Mkuu wa Baraza Kuu la Usalama nchini Afghanistan. Burhanuddin Rabbani alizaliwa tarehe 20 Septemba mwaka 1940. Alikuwa kiongozi wa chama cha Jumuiya ya Kiislamu nchini humo na rais rasmi wa kwanza wa utawala wa Mujahidina huko Afghanistan. Hadi mwisho wa maisha yake, Burhanuddin Rabbani, alikuwa mkuu wa Baraza Kuu la Usalama lililoundwa na rais wa zamani wa nchi hiyo, Hamid Karzay. Baraza hilo lilikuwa na wadhifa wa kufanya mazungumzo na kundi la Taleban kwa lengo la kufikiwa suluhu na kumaliza mgogoro wa taifa hilo kwa njia ya amani. Rabani aliuawa katika siku kama ya leo na gaidi aliyekuwa ameficha bomu katika kilemba chake, wakati alipoingia ofisini kwa mwanasiasa huyo kwa madai ya kufanya mazungumzo.