Alkhamisi tarehe 26 Septemba 2019
Leo ni Alkhamisi tarehe 26 Muharram mwaka 1441 Hijria sawa na tarehe 26 Septemba mwaka 2019.
Siku kama ya leo miaka 1377 iliyopita mji mtakatifu wa Makka ulishambuliwa baada ya kuzingirwa na jeshi la mtawala mal'uni wa kizazi cha Banii Umayyah, Yazid bin Muawiyya. Baada ya kumuua shahidi Imam Hussein na wafuasi wake katika medani ya Karbala na Watu wa Nyumba ya Mtume wakachukuliwa mateka, Yazid alidharaulika sana na kukosa heshima katika Umma wa Kiislamu. Waislamu katika maeneo mbalimbali walianzisha uasi dhidi ya utawala wake. Harakati hizo za uasi zilifika hadi Hijaz hapo mwaka 63 Hijria ambapo watu wa Makka walimfukuza gavana wa Yazid na kuchukua madaraka ya mji huo. Mtawala huyo alituma jeshi ambalo liliuzingira mji huo mtukufu na kushambulia Msikiti wa Makka na al Kaaba kwa mawe.
Miaka 418 iliyopita aliaga dunia Sheikh Abdullah Tostari faqihi na msomi wa Kiislamu wa Kiirani. Sheikh Tostari alifikia daraja ya ijtihad baada ya kuhitimu masomo ya kidini chini ya maustadhi wakubwa wa zama hizo. Sheikh Abdullah Tostari baadaye alielekea katika hauza ya kielimu ya mji wa Isfahan nchini Iran na kuanza kufundisha masomo ya dini. Darsa ya mujtahidi huyo ilikuwa ikihudhuriwa na wanafunzi wengi ambao walinufaika na bahari kubwa ya elimu yake. Allamah Majlisi na Mirza Muhammad Naini ni miongoni mwa wanafunzi wa Sheikh Abdullah Tostari.

Katika siku kama ya leo miaka 131 iliyopita alizaliwa Thomas Stearns Eliot mshairi na mwanafasihi mashuhuri wa Uingereza. Malenga huyo ambaye ni mashuhuri kwa jina la S. T. Eliot alitoa nudhumu yake ya kwanza ya mashairi mwaka 1922 iliyokuwa na jina la "The Waste Land" na kupata umashuhuri mkubwa. Mwanafasihi huyo wa Kiingereza aliaga dunia mwaka 1965.
Siku kama ya leo miaka 112 iliyopita, inayosadifiana na 26 Septemba 1907, nchi ya New Zealand iliyoko mashariki mwa Australia ilipata uhuru. Visiwa vya New Zealand vilikoloniwa na Uingereza mwaka 1769 na karne ya 19 Miladia, ilishuhudia ukoloni dhidi ya nchi hiyo ukishadidi sambamba na wimbi kubwa la wahajiri wa Kiingereza waliokuwa wakielekea katika nchi hiyo.
Siku kama ya leo miaka 59 iliyopita, inayosadifiana na 26 Septemba 1960, Makamu wa Rais wa Marekani Richard Nixon na Seneta John F. Kennedy wa Massachusetts walikabiliana katika mdahalo wa kwanza wa televisheni wakati wakiwania tiketi ya kuingia ikulu ya White House. John Kennedy aliibuka na ushindi katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwaka huo.
Na siku kama hii ya leo miaka 7 iliyopita Maya Nasri mwandishi habari wa Kikristo wa kanali ya televisheni ya Press ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliuawa mjini Damascus nchini Syria wakati alipokuwa akitayarisha ripoti kwa ajili ya kanali hiyo. Maya Nasr alizaliwa tarehe 30 Julai mwaka 1979 nchini Syria na kuhitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Kaplan kilichoko New York huko Marekani. Nasr akiwa pamoja na Mkurugenzi wa kanali ya televisheni ya Press nchini Syria, Hussein Murtadha, alishambuliwa kwa kupigwa risasi mbili kichwani na mlenga shabaha wa wapinzani wa serikali ya Damascus wakitayarisha ripoti ya matukio ya Syria. Mwenzake Maya, Hussein Murtadhaa alijeruhiwa katika shambulizi hilo.