Oct 30, 2019 04:12 UTC
  • Jumatano, tarehe 30 Oktoba, 2019

Leo ni Jumatano tarehe Mosi Rabiul Awwal 1441 Hijria sawa na Oktoba 30 mwaka 2019

Siku kama ya leo miaka 1441 iliyopita, Mtume Muhammad SAW alianza Hijra yake ya kuhama Makka na kuelekea Madina, ikiwa imepita miaka 13 tokea alipobaathiwa na kupewa Utume. Mtume wa Allah alihama Makka kutokana na kushadidi vitimbi vya washirikina wa mji huo ambao walikusudia kumdhuru na kumuua wakati wa usiku akiwa amelala nyumbani kwake. Imam Ali AS alijitolea mhanga, kwa kuamua kulala kwenye kitanda cha Mtume, ili maadui wasitambue kwamba Mtume wa Allah ameondoka mjini Makka. Hijra ya Mtume SAW na matukio ya baada yake yalikuwa na umuhimu mkubwa katika ustawi na maendeleo ya Uislamu kiasi kwamba lilitambuliwa kuwa mwanzo wa kalenda ya Kiislamu. Ni vyema kukumbusha hapa kuwa Mtume (saw) ndiye aliyekuwa wa kwanza kutumia hijra yake kama mwanzo wa kalenda ya Kiislamu kwani barua zote zilizoandikwa na mtukufu huyo kwa wakuu wa makabila na shakhsia maarufu alizisajili kwa kalenda hiyo.

Tarehe Mosi Rabiul Awwal miaka 1376 iliyopita, ilianza harakati ya Tawwabin kwa lengo la kulipiza kisasi cha kuuawa shahidi Imam Hussein AS pamoja na wafuasi wake watiifu. Awali, watu wa Kufa walimuomba Imam Hussein AS aelekee mjini humo kwa lengo la kuongoza harakati dhidi ya utawala wa kidhalimu wa Yazid bin Muawiya lakini alizingirwa njiani na jeshi la mtawala dhalimu, Yazid bin Muawiya, na kuuawa shahidi. Tawwabin ni kundi la watu wa Kufa ambalo lilijuta kwa kushindwa kutekeleza ahadi yake na kumuacha Imam Hussein na wafuasi wake wachache peke yao wapambane na majeshi ya Yazid. Kwa minajili hiyo watu hao walitubia makosa yao na kuamua kuanzisha harakati ya kulipiza kisasi wakiongozwa na Sulaiman bin Sorad dhidi ya jeshi la Yazid. Kundi hilo lilipigana kishujaa na jeshi la Yazid na wengi kati ya wapiganaji wake wakauawa shahidi.

Siku kama ya leo miaka 109 iliyopita yaani tarehe 30 Oktoba 1910 alifariki dunia Henri Dunant, mwasisi wa Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu. Dunant alizaliwa Geneva na mwaka 1828, aliamua kuanzisha Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu kwa shabaha ya kuokoa maisha ya majeruhi wa vita. Kutokana na hatua yake hiyo ya kibinadamu, Henri Dunant alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel mwaka 1901, na alifariki dunia akiwa na umri wa miaka 82.

Henri Dunant

Na Siku kama ya leo miaka 39 iliyopita, inayosadifiana na tarehe 8 Aban 1359 Hijria Shamsia, aliuawa shahidi Muhammad Hussein Fahmideh, kijana shujaa wa Kiirani kwenye vita vya kichokozi vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran. Shahidi Fahmideh alielekea kwenye medani ya vita akiwa na umri wa miaka 13 tu, ikiwa imepita miezi michache tu baada ya kuanza kwa vita hivyo. Shahidi Fahmideh alijitolea mhanga kwa kujifunga kiunoni maguruneti na kujilaza mahala kilipokuwa kikipita kifaru cha adui na kuwatia kiwewe na hatimaye kuwalazimisha wavamizi kukimbia. Hatua hiyo ilipongezwa na Imam Khomeini ambaye alimtaja kijana huyo kuwa ni kiongozi na kigezo cha kuigwa.

Muhammad Hussein Fahmideh

 

Tags