Nov 14, 2019 02:41 UTC
  • Alkhamisi tarehe 14 Novemba 2019

Leo ni Alkhamisi tarehe 16 Mfunguo Sita Rabiul Awwal 1441 Hijria sawa na Novemba 14 mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 1440 kwa mujibu wa baadhi ya mapokezi ya historia, Swala ya kwanza ya Ijumaa iliswaliwa na Mtume Muhammad (saw) baada ya mtukufu huyo kuhama mji wa Makka. Baada ya kuwasili katika eneo la Bani Salim bin Auf kwa jina la Quba karibu na Madina wakati wa adhuhuri, Mtume (saw) alitoa hotuba na kusimamisha Swala ya Ijumaa mahala hapo. Wanahistoria wanasema hiyo ilikuwa Swala ya kwanza ya Ijumaa katika Uislamu. Hatua hiyo pia inaonesha umuhimu wa ibada hiyo ya kiroho na kisiasa ambayo Bwana Mtume aliamua kuitekeleza mara tu baada ya kuwasili karibu na mji wa Madina. Baadaye Waislamu walijenga msikiti katika eneo hilo palipofanyika Swala ya Ijumaa ya kwanza katika Uislamu.

Katika siku kama ya leo miaka 486 iliyopita, Ecuador inayopatikana huko Amerika ya Kusini iligunduliwa na wavumbuzi wa Kihispania na kuunganishwa na ardhi zilizokuwa zikidhibitiwa na Uhispania. Ecuador ilikoloniwa na Uhispania kwa karne tatu.Hata hivyo mwaka 1822 wananchi wapigania ukombozi wa nchi hiyo chini ya uongozi wa Simon Bolivar walifanikiwa kurejesha uhuru wa nchi hiyo na Ecuador ikajiunga na Shirikisho la Colombia Kubwa.

Bendera ya Ecuador

Siku kama ya leo miaka 303 iliyopita, Gottfried Wilhelm Leibnitz mwanahisabati na mwanafalsafa wa Kijerumani aliaga dunia mjini Hanover Ujerumani akiwa na umri wa miaka 70. Wilhelm Leibnitz alianza kuzisoma kwa bidii na juhudi elimu za falsafa na hisabati akiwa na umri wa miaka 15 alifanikiwa kupata shahada za juu kabisa katika masomo hayo. Elimu na ufahamu mkubwa na mchango aliotoa katika elimu ya hisabati pamoja na vitabu alivyoandika kuhusiana na elimu hizo, ni mambo yaliyomfanya Gottfried Wilhelm Leibnitz awekwe katika faharasa ya wasomi maarufu wa falsafa na hisabati nchini Ujerumani. 

Gottfried Wilhelm Leibnitz

Siku kama ya leo miaka 222 iliyopita inayosadifiana na tarehe 14 Novemba mwaka 1897, alizaliwa Charles Lyell mtaalamu wa masuala ya ardhi na mwanasayansi wa Scottland. Lyell alikuwa mtu wa kwanza kuweka misingi na kanuni sahihi za kielimu katika masuala ya geolojia.

Charles Lyell

Siku kama ya leo miaka 130 iliyopita, Jawaharlal Nehru mmoja kati ya viongozi wakubwa wa harakati ya mapambano ya India dhidi ya mkoloni Mwingereza alizaliwa huko Allahabad kaskazini mwa India. Nehru alianza mapambano dhidi ya mkoloni Mwingereza baada ya kujiunga na harakati ya kitaifa ya ukombozi wa India. Jawaharlal Nehru alitiwa mbaroni mara kadhaa na kufungwa jela kutokana na mchango na nafasi yake kubwa katika mapambano hayo. Baada ya Mahatma Ghandi kujiunga na harakati ya kitaifa ya India, wanaharakati hao wakiongoza mapambano ya kupigania uhuru ya wananchi wa India walitoa pigo kubwa kwa mkoloni Mwingereza. Hatimaye India ilipata uhuru Agosti 15 mwaka 1947.

Jawaharlal Nehru

Miaka 130 iliyopita katika siku kama ya leo, Dakta Taha Hussein mwandishi na mwanafasihi mtajika wa Misri alizaliwa. Msomi huyo mashuhuri alipofuka macho akiwa mtoto. Hata hivyo kipaji chake cha hali ya juu kilimuwezesha kuendelea na masomo na hadi kufikia mwaka 1918 alikuwa amekamilisha masomo yake ya shahada ya uzamivu katika vyuo vikuu vya Misri na Ufaransa. Dakta Taha Hussein mbali na kuwa kipofu, aliweza pia kushika nyadhifa za juu ndani na nje ya Misri na kipindi fulani alikuwa Waziri wa Utamaduni wa Misri.

Dakta Taha Hussein

Siku kama ya leo miaka 54 iliyopita mwafaka na tarehe 23 Aban mwaka 1344 Hijria Shamsia, alifariki dunia mwandishi na mhakiki mkubwa wa Kiirani, Said Nafisi akiwa na umri wa miaka 71. Baada ya kupata elimu ya upili, Nafisi alielekea Ufaransa kwa ajili ya elimu ya juu. Baada ya kumaliza masomo yake huko Ufaransa alirejea Iran na kufunza katika vyuo vikuu hapa nchini. Said Nafisi ameandika na kutarjumu vitabu zaidi ya 180 ikiwemo kamusi ya lugha ya Kifaransa na Kifarsi.

Said Nafisi

 

Tags