Dec 05, 2019 01:21 UTC
  • Alkhamisi tarehe 5 Disemba 2019

Leo ni Alkhamisi tarehe 8 Rabiuthani 1441 Hijria sawa na Disemba 5 mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 1209 iliyopita alizaliwa Imam Hassan Askari (as) ambaye ni miongoni mwa wajukuu wa Mtume Muhammad (saw), katika mji mtakatifu wa Madina. Imam Askari alilazimishwa na watawala wa Bani Abbas kwenda uhamishoni huko Samarra akiwa pamoja na baba yake na kufaidika na elimu ya Imam Hadi kwa kipindi cha miaka 13. Alishika hatamu za kuongoza Umma wa Kiislamu kwa kipindi cha karibu miaka sita baada ya kuuawa shahidi baba yake. Sehemu ya umri wake wa miaka 28 uliishia katika jela za watawala madhalimu wa Bani Abbas au akiwa uhamishoni na chini ya udhibiti wa watawala hao. Hata hivyo mtukufu huyo hakuacha kueneza maarifa sahihi ya Uislamu na kulea kizazi cha wanazuoni hodari.

Katika siku kama ya leo miaka 1084 iliyopita yaani mwaka 357 Hijria, aliaga dunia Abu Firas al-Hamdani malenga na mwandishi mahiri wa Kiarabu. Mbali na kuandika mashairi, Abu Firas al-Hamdani alikuwa mpiganaji na miongoni mwa watu wa karibu kwa Seiful Dawlah mtawala wa Halab, Vilevile alikuwa miongoni mwa makamanda wake. Wakati washairi wengi walipokuwa wakitunga mashairi kusifu watawala wa Banii Abbas, mshairi huyo mashuhuri alitunga na kusoma mashairi yanayokashifu na kulaani dhulma za watawala hao. Katika kipindi cha vita baina ya Seiful Daulah na Warumi, Abu Firas al-Hamdani alitekwa nyara na maadui na alichiwa huru baada miaka 4. Alijeruhiwa katika vita nyingine na kufariki dunia baadaye.

ابو فراس حمدانی

Katika siku kama ya leo miaka 149 iliyopita, aliaga dunia Alexander Dumas mwandishi mtajika wa Kifaransa. Mwandishi huyo ambaye ni mashuhuri pia kwa jina la Dumas Baba baada ya kumaliza masomo yake aliajiriwa katika ofisi moja ya kiwanda kama katibu kutokana na kuwa na hati nzuri.

Alexander Dumas

Siku kama ya leo miaka 145 iliyopita, Iran ilijiunga na Shirika la Kimataifa la Msalaba Mwekundu. Jitihada za awali za Iran kutaka kujiunga na shirika hilo zinarejea nyuma katika kipindi cha utawala wa Mfalme Nassereddin Shah Qajar. Katika kipindi cha utawala wake, Disemba 1874 Iran iliukubali mkataba uliopasishwa Geneva Uswisi, lakini licha ya kupita miaka kumi tangu isaini mkataba huo, utawala wake haukuchukua hatua yoyote ile ya kuasisi taasisi au jumuiya ambayo itatekeleza hati ya mkataba huo hapa Iran.

Tarehe 5 Disemba miaka 118 iliyopita alizaliwa Walt Disney shakhsiya mashuhuri wa sekta ya filamu za watoto. Disney alizaliwa katika mji wa Chicago huko Marekani. Walt Disney alihitimu masomo katika Chuo Kikuu cha Havard na kutunukiwa shahada ya udaktari katika sayansi ya uchoraji na uchongaji (Fine Art). Disney alitoa mchango mkubwa katika kuimarisha sanaa ya filamu za katuni. Mara kadhaa alitunukiwa tuzo za Oscar katika uwanja huo wa kutengeneza filamu za katuni. Miongoni mwa kazi muhimu za Walt Disney ni Snow White, The Seven Dwarfs, Polar Bears.

Siku kama ya leo miaka 102 iliyopita aliaga dunia alimu na mwanazuoni Mulla Fathullah Gharawi Isfahani aliyejulikana kwa jina la Sheikhu Shari'a Isfahani. Alizaliwa mwaka 1228 Hijria Shamsia huko Isfahan katikati mwa Iran na kupata elimu ya dini katika mji huo. Baadaye kidogo alielekea katika mji mtakatifu wa Mash'had na mwaka 1257 alikwenda Najaf nchini Iraq kwa ajili ya kutafuta elimu na kusoma kwa walimu wakubwa na mashuhuri wa zama hizo. Ameandika vitabu kadhaa katika masuala ya sheria na fiqhi ya Kiislamu. Sheikhu Shari'a pia alikuwa mstari wa mbele katika mapambano ya kiutamaduni, kisiasa na kijeshi dhidi ya wakoloni wa Kiingereza na aliongoza harakati za wananchi wa Iraq dhidi ya wakoloni hao.

Sheikhu Shari'a Isfahani

Siku kama ya leo miaka 6 iliyopita alifariki dunia shujaa wa mapambano ya ukombozi na kupinga ubaguzi wa rangi nchini Afrika Kusini Mzee Nelson Mandela akiwa na umri wa miaka 95. Mandela alizaliwa mwaka 1918 na alitumia zaidi ya nusu ya umri wake akipambana na utawala wa kibaguzi nchini kwake. Utawala wa wazungu wabaguzi ulimfunga jela kwa kipindi cha miaka 27 hadi mfumo wa ubaguzi wa rangi ulipofutwa mwaka 1990. Mwaka 1994 wananchi wa Afrika Kusini walimchagua Nelson Mandela kuwa Rais wa kwanza mzalendo wa nchi hiyo. Baada ya kushika hatamu za uongozi, Mandela aliamiliana vyema na watala wa zamani wa mfumo wa ubaguzi wa rangi na hata wale waliomfunga jela na kumtesa. Mwenendo huo wa kusamehe ulizidisha umashuhuri na kupendwa shujaa huyo, na mwaka 1993 alitunukiwa tuzo ya amani ya Nobel. Kitabu mashuhuri zaidi cha shujaa huyo wa Afrika ni kile chenye kumbukumbu zake alichokipa jina la: "Njia Ndefu ya Kuelekea kwenye Uhuru".

نلسون ماندلا

Na Leo Disemba 5 ni Siku ya Kimataifa ya Wahisani ambao hujitolea kwa hali na mali kwa ajili ya kuokoa maisha ya watu wengine. Kutenda wema na kufanya hisani ni suala ambalo halihusu, dini, taifa, wala kaumu makhsusi. Hata hivyo Uislamu ambayo ni dini ya mwisho ya Mwenyezi Mungu, umehimiza zaidi kutenda wema na hisani na kuwataja wahisani na watenda wema kwamba ni vipenzi vya Mwenyezi Mungu. Sehemu ya Aya ya 195 ya Suratul Baqara inasema: Na fanyeni wema. Hakika Mwenyezi Mungu huwapenda wahisani.  

Siku ya Kimataifa ya Wahisani

 

Tags