Dec 26, 2019 01:09 UTC
  • Alkhamisi tarehe 26 Disemba 2019

Leo ni Alkhamisi tarehe 29 Mfunguo Nane Rabiuthani 1441 Hijria inayosadifiana na Disemba 26 mwaka 2019.

Siku kama ya leo miaka 15 iliyopita mtetemeko mkubwa wa ardhi uliokuwa na daraja 9 kwa kipimo cha Rishta ulitokea katika Bahari ya Hindi na kusababisha mawimbi makubwa ya Tsunami. Mawimbi hayo yalisambaa na kuenea kwa kasi kubwa katika nchi kadhaa za kandokando ya bahari hiyo na kusababisha maafa makubwa. Kitovu cha mtetemeko huo kilikuwa maji ya kusini mashariki mwa Asia na kwa msingi huo nchi za India, Indonesia, Sri Lanka na Thailand ndizo zilizoathiriwa zaidi na mtetemeko huo. Mawimbi ya Tsunami yaliyosababishwa na mtetemeko huo yalisababisha vifo vya watu wasiopungua laki mbili na elfu 20 na kuharibu nyumba za watu milioni mbili. Nchi hizo pia zilipata hasara ya mamilioni ya dola.

Tarehe 5 Dei mwaka 1382 Hijria Shamsia yaani siku kama hii la leo miaka 16 iliyopita, mtetemeko wa ardhi uliokuwa na nguvu ya 6.8 kwa kipimo cha Rishta ulitokea katika mji wa Bam kusini mwa Iran na maeneo ya kandokando yake. Mtetemeko huo wa ardhi uliharibu sehemu kubwa ya mji huo na kusababisha vifo vya watu elfu 41. Makumi ya maelfu ya watu wengine pia walijeruhiwa. Maafa ya mtetetemo huo wa ardhi yalikuwa makubwa mno kwa kadiri kwamba baadhi ya jumuiya na taasisi za kimataifa zilijiunga na wananchi na serikali ya Iran katika kutoa misaada ya dharura kwa waathiriwa. Mbali na hasara za nafsi na vifo vya maelfu ya watu, mtetemeko wa ardhi wa Bam ulisababisha pia hasara kubwa za kiuchumi na kuharibu jengo la kale la Arge Bam.

Miaka 40 iliyopita katika siku kama ya leo Jeshi Jekundu la Urusi ya zamani liliivamia ardhi ya Afghanistan. Uvamizi huo wa Russia unatambuliwa na kizazi kipya cha viongozi wa nchi hiyo kuwa ni miongoni mwa makosa makubwa ya ikulu ya Kremlin katika siasa zake za nje. Uvamizi huo wa Urusi ulifanyika kutokana na ombi la Babrak Karmal mmoja wa viongozi wa Afghanistan. Tangu wakati huo Mujahidina wa Afghanistan walianza mapambano dhidi ya jeshi la askari laki moja na 30 elfu la Jeshi Jekundu (Red Army). Katika upande mwingine Marekani ambayo ilitambua kuwepo kwa Urusi ya zamani huko Afghanistan kuwa ni hatari kwa maslahi yake ilianza kuunda makundi ya wapiganaji na kuyasaidia kwa mali na silaha kwa ajili ya kukabiliana na Urusi. Makumi ya maelfu ya watu waliuawa na wengine kufanywa vilema katika kipindi cha miaka 10 ya uvamizi wa Urusi huko Afghanistan.

Uvamizi wa Red Army huko Afghanistan

Katika siku kama ya leo miaka 121 iliyopita, Ayatullah Sayyid Ali Husseini Mar’ashi mashuhuri kwa lakabu ya Sayyid al-At’baa mmoja wa matabibu mahiri wa Iran alifariki dunia. Alizaliwa katika mji wa Tabriz nchini Iran na baada ya kumaliza masomo ya awali ya kidini alisafiri na kuelekea Najaf Iraq kwa shabaha ya kujiendeleza zaidi kielimu. Sayyid Ali Mar’ashi alisoma kwa kwa walimu mahiri wa zama hizo mjini Najaf na kurejea katika mji aliozaliwa akiwa na shahada ya Ijtihadi. Kutokana na mapenzi yake makubwa na elimu ya tiba alielekea katika mji wa Isfahan na kusoma taaluma hiyo kwa muda wa miaka 15. Alimu huyo amevirithisha vizazi vilivyokuja baada yake vitabu vingi na vyenye thamani kubwa ambapo Tarikh Tabriz na Sharh Tib al-Nabbi ni baadhi tu ya vitabu vyake muhimu.

Ayatullah Sayyid Ali Husseini Mar’ashi

Miaka 768 iliyopita katika siku kama hii ya leo alizaliwa Muhammad bin Ahmad Dhahabi, anayejulikana kwa lakabu la Shamsuddin, mpokeaji wa hadithi na mwanahistoria mashuhuri wa zama hizo. Dhahabi alikuwa akipenda sana kukusanya hadithi na alifanya safari nyingi katika pembe mbalimbali duniani ili kukamilisha elimu hiyo. Muhammad bin Ahmad Dhahabi alisimuliwa hadithi nyingi sana kutoka kwa wazee na maulamaa katika safari zake hizo. Dhahabi alifuatilia matukio ya historia ya Uislamu na watu mashuhuri ya kuanzia wakati wa kudhihiri Uislamu hadi mwaka 704 na kuandika habari na matukuio ya wataalamu wa hadithi wa zama hizo. Matukio hayo aliyakusanya katika kitabu alichokipa jina la Historia ya Uislamu. Vitabu vingine vya msomi huyo ni pamoja na Tabaqatul Qurraa, al Muujamul Saghiir na al Muujamul Kabiir.