Feb 13, 2020 06:21 UTC
  • Nuru ya Imani katika Mwamko wa Imam Khomeini MA

Hamjambo wapenzi wasikilizake na karibuni kujiunga nami katika makala hii tuliyokutayarishieni kwa mnasaba wa maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ambapo leo tutaangazia namna fikra za Imam Khomeini MA, zilivyoweza kuenea na kuwavutia wasomi wengi duniani.

Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran mnamo February 1979 si tu kuwa ulipelekea kuanguka utawala wa kifalme, kiimla na kifisadi wa Pahlavi, bali pia ushindi huo ulikuwa na taathira kubwa nje ya mipaka ya Iran. Moja ya taathiri muhimu zaidi za ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ni kuenea umaanawi, kuhuishwa Uislamu na idadi kubwa ya watu kuanza kuzingatia tena dini hii tukufu ya mbinguni. Imam Khomeini MA kama kiongozi wa kidini na msomi wa Kiislamu alikuwa na nafasi ya kimsingi katika kuongoza Mpainduzi ya Kiislamu katika mkondo wa Kiislamu. Aidha alichangia pakubwa katika kuhakikisha kuwa fikra ya Mapinduzi ya Kiislamu inaenea kote duniani na kuwafaidi Waislamu na wasio kuwa Waislamu na kupelekea wengi kusilimu au kuuchagua Uislamu kama muongozo wa maisha. Idadi kubwa ya Waislamu pia walivutiwa na shakhsia ya kimaanawi na mkondo wa kimapainduzi wa Imam Khomeini na hivyo wakaamua kusilimu ili kufuata itikadi yake. Ahmad Huber nwanafikra na mwandishi habari kutoka Sweden anasema: "Imam Khomeini MA aliweza kuleta muamko miongoni mwa wale wote wenye Imani ya Mungu Mmoja katika zama zetu. Kwa hakika dunia ina deni kubwa kwa Imam Khomeini MA na wafuasi wake katika Mapinduzi ya Kiislamu kutokana uhuishaji wa dini na umaanawi katika zama za dunia iliyokuwa imezama katika kuabudu fedha na iliyokuwa imejaa fikra zilizo dhidi ya umaanawi."

Kuangazia namna watu kama hawa walivyoweza kuvutiwa na thamani za Mapinduzi ya Kiislamu na muasisi wa mapinduzi hayo ni jambo linaloweza kuweka wazi taathira ya kimaanawi ya harakati hiyo ya mapinduzi.

Imam Khomeini MA akiwa Neauphle-le-Château Uaransa

Katika zama za harakati zake, Imam Khomeini aliishi uhamishoni nchini Iraq kwa muda mrefu lakini utawala wa Baath wa nchi hiyo ulimlazimisha kuondoka na Oktoba 6 1978 aliwasili mjini Paris Ufaransa na kuelekea katika kijiji cha Neauphle-le-Château karibu na mji huo na alikaa hapo kwa muda wa takribani miezi minne. Katika kipindi hicho alifanya mahojiano, kutoa taarifa na pia kukutana na  watu wengi kwa lengo la kubainisha utambulisho na malengo ya mapinduzi ya Kiislamu kwa wote na hivyo harakati ya kuelekea ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ikashika kasi zaidi. Katika kipindi hicho wakaazi wengi wa Neauphle-le-Château na watu wengine wa Ufaransa walivutiwa sana na shakhsia ya Imam na harakati zake.

Mmoja kati ya waliovutiwa na Imam Khomeini ni Bi. Moharraz Laab. Mkutano wake mfupi na Imam Khomeini MA na mvuto pamoja na nuru yake ya kimaanawi ni jambo ambalo lilimvutia sana mwanamke huyu Mfaransa. Kutokana na baraka hizo, mwanamke huyo alishuhudia mabadiliko ya kiroho na akaanza kufanya utafiti kuhusu Uislamu ambao  Imam Khomeini alikuwa ameuarifisha na baada ya muda usiokuwa mrefu alipata taufikI na kufuata itikadi ya Kiislamu ambayo aliipata kutoka kwa Imam. Itikadi ya mwanamke huyo ambaye alikuwa tajiri iliwavutia wanawe na mume wake nao pia wakaamua kufuata mafundisho yenye thamani ya Qur'ani Tukufu na Ahul Bayt wa Mtume SAW. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu alifanikiwa kuonana mara mbili na Imam Khomeini MA na katika moja ya mikutano hiyo Imam alimtunuku nakala ya Qur'ani ambayo alikuwa ameitia saini. Nafisa, mjukuu wa Bi. Moharraz Laab anazungumza kuhusu maadili ya nyanya yake na kusema: "Nyanya yangu alikuwa na maadili na akhlaqi njema kiasi kwamba aliweza kuwavutia wale wote aliozungumza nao. Alikuwa na uwezo mkubwa wa kubainisha na kufafanua mambo ya kidini na hivyo aliwafanya wengi wavutiwe na Uislamu. Mapenzi na mahaba ambayo nyanya yangu alikuwa nayo kwa Maimamu Watoharifu AS ni jambo ambalo lilipelekea wote katika familia na jamaa kuwa Waislamu wafuasi wa madhehebu ya Shia na kwa hakika mafanikio hayo yote yametokana na ukarimu wa Ahul Bayt AS."

Bi. Laab

Bi. Laab ambaye alikuwa Muislamu mwanamapinduzi na mwenye hima kubwa, alijipa jukumu la kuhakikisha kuwa anaeneza mafundisho halisi ya Kiislamu kwa wengine. Ni kwa sababu hii ndio, kwa kutawakali au kumtegemea Mwenyezi Mungu na kwa himaya ya mume wake na marafiki zake, alitumia utajiri wake mkubwa kuutangaza Uislamu na kuwafahamisha Wafaransa kuhusu Ahul Bayt wa Mtume SAW na Mapinduzi ya Kiislamu. Mahrez Laib aliweza kupata mafanikio makubwa katika kazi yake hiyo na aliweza pia kujenga misikiti na vituo vya Kiislamu katika maeneo mbali mbali ya Ufaransa. Harakati zake za kuutangaza Uislamu zilipelekea serikali ya Ufaransa iingiwe na wasi wasi mkubwa na hivyo hatimaye  alikamatwa na kufungwa jela kwa tuhuma zisizo na msingi. Lakini akiwa gerezani pia aliendeleza harakati zake za kuutangaza Uislamu halisi na kuwaongoza  wafungwa katika njia ya Qur'ani Tukufu na maarifa ya Ahul Bay AS. Aidha katika ukuta wa seli yake aliweka picha ya Imam Khomeini MA na aliwatangazia wafungwa malengo ya kiongozi huyo na kuhusu mfumo wa Kiislamu nchini Iran. Kutokana na harakati hizo, maafisa wa usalama wa Ufaransa waliamua kuwa alikuwa hatari zaidi ndani ya gereza kuliko nje ya gereza na hivyo waliamua kumuachilia huru. Bi. Moharraz Laab aliendeleza harakati zake na hatimaye akaaga dunia na kurejea kwa Mola wake mwaka 2015 akiwa ameshatumia aghalabu ya utajiri wake kuutangaza Uislamu.

Harakati ya Kiislamu na ya wananchi ya Imam Khomeini MA pia ilimvutia kijana Mtaliano, Roberto Arcadi,  ambaye aliusoma Uilamu na kupata jibu baada ya utafiti wake kumhusu Mungu na maumbile ya dunia. Maisha ya kijana huyo Mtaliano yalipata muongozo zaidi alipovutiwa na shakhsia ya Imam Khomeini MA. Anafafanua hivi kuhusu nukta hiyo: "Siku moja nilimuona Imam Khomeini MA katika televisheni na kwa kweli nilivutiwa sana na haiba pamoja na adhama yake iliyojaa nuru na hapo nikaanza kuwaza na kujiuliza huyu bwana ni nani na ametoka wapi? Ni vipi amepata ushujaa wa aina hii kukabiliana na madola makubwa duniani. Alinivutia sana na kunishangaza na kwa msingi huo nikaanza kufanya utafiti kuhusu Uislamu na Mapiunduzi ya Kiislamu. Baadaye niliweza kuwa na marafiki ambao walikuwa ni wafuasi wa Ahul Bayt AS na kisha nikawa na uhusiano na Wairani wanaoishi Milan. Hatimaye katika sherehe za kukumbuka kuzaliwa Imam wa Zama, Imam Mahdi ATF, rafiki yangu alinialika katika Kituo cha Kiislamu cha Wairani na hapo nikatamka  Shahada Mbili na nikawa Muislamu wa Madhehebu ya Shia." Roberto Arcadi aliathiriwa sana na shakhsia ya Imam Ruhullah Mousawi Khomeini kiasi kwamba alibadilisha jina lake likawa ni Ruhullah. Kuhusu shakhsia ya Imam Khomeini Arcadi anasema: "Kwa hakika Imam Khomeini alikuwa shakhsia mwenye sifa kadhaa za kipekee na alikuwa na ufahamu wa masuala yote ya maisha na alikuwa na uhusiano wenye nguvu na watu wote kwa sababu alikuwa na mapenzi yaliyojaa Ikhlasi kutoka kwa Mwenyezi Mungu."

Mahojiano kadhaa ambayo Imam Khomeini aliyafanya na vyombo vya habari kabla ya kurejea Iran yalikuwa na nafasi muhimu katika kuarifisha utambulisho na malengo ya Mapinduzi ya Kiislamu. Sheikh Ibrahim Zakzaky wa Nigeria alipata fursa ya kusikiliza mmoja kati ya mahojiano hayo wakati akiwa mwanafunzi wa chuo kikuu katika taaluma ya kiuchumi nchini Nigeria.

Sheikh Zakzaky

Katika zama hizo, tumaini lake kuu lilikuwa ni kuanzishwa mfumo wa utawala wa Kiislamu katika nchi yake na hivyo wakati aliposikia kuwa Imam Khomeini ameweza kuanzisha mfumo wa Kiislamu nchini Iran alivutiwa sana na kiongozi huyo.  Ili kumfahamu zaidi Imam Khomeini, Sheikh Zakzaky alisikiliza mahojiano yake. Hatimaye aliweza kualikwa kuja Iran katika maadhimisho ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika mwanzo wa muongo wa 80 ambapo aliweza kukutana na Imam Khomeini. Baada ya kumalizika kikao hicho, Zakzaky alimuomba Imam ampe ujumbe wa kuwafikishia watu wa Nigeria na hapo Imam akamkabidhi nakala ya Qur'ani Tukufu na kumpa nasaha ifuatayo: "Wafikishe salamu zetu watu wa Nigeria na uwafahamishe kuwa maneno yote ya Khomeini yamo kwenye hii Qur'ani Tukufu." Shakhsia ya busara na kimaanawi ya Imam Khomeini ilikuwa na taathira kubwa kwa Sheikh Zakzaky kiasi kwamba anasema aliporejea Nigeria alitokwa na machozi akiwa ameishika nakala hiyo ya Qur'ani mkononi. Anafafanua zaidi kwa kusema: "Katika uso wa Imam nilimuona Musa, Issa, Ibrahim Khalilullah na Muhammad Rasulullah." Sheikh Zakzaky anasema alifika Nigeria na kuwafahamisha watu wa nchi hiyo kuhusu mafundisho ya Qur'ani. Kutokana na jitihada za Sheikh Zakzaky za kueneza fikra za Imam Khomeini MA katika nchi yake, hivi sasa zaidi ya Wanigeria milioni 15 ni wafuasi wa Uislamu asili na Madhehebu ya Ahul Bayt AS.  Kutokana na jitihada zake hizo serikali ya nchi hiyo imeingiwa na kiwewe na hivyo Sheikh Zakzaky amefungwa jela mara kadhaa na watoto wake sita wameuawa shahidi. Aidha hivi sasa akiwa na mke wake wanaendelea kushikiliwa gerezani nchini Nigeria.

Profesa Roger Garaudy

Msomi mwingine ambaye tunaweza kumtaja hapa ni Profesa Roger Garaudy, mwanafalsafa Mfaransa ambaye naye pia aliweza kuvutia na shakhsia iliyojaa nuru ya Imam Khomeini, muasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran. Wakati alipokuwa mwanafikra wa chama cha kikomunisti katika nchi yake, aliweza kupata taufiki ya kusoma fikra za Imam Khomeini na hatimaye akaamua kusilimu.

Profesa Garaudy alisema hivi kuhusu fikra za Mapinduzi ya Kiislamu na Imam Khomeini: "Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran chini ya uongozi wa Imam Khomeini MA yameweza kuweka wazi ustaarabu asili wa Kiislamu na kuleta matumaini katika nyoyo za mamilioni ya Waislamu kote duniani na jambo hili limeweza kuleta uhai mpya katika Uislamu na kuhuisha adhama ya jadi ya Uislamu duniani."

 

Tags