Feb 04, 2019 05:48 UTC
  • Miaka 40 ya kuwa bega kwa bega wanawake na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran

Tukichunguza kwa makini mapinduzi na mabadiliko mbalimbali ambayo yametokea duniani hadi sasa tutabaini kuwa wanawake wameshiriki na wametoa mchango athirifu katika akthari ya mapinduzi hayo. Katika moja ya sifa maalumu za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni kushiriki kwa wingi wanawake na mchango mkubwa waliotoa katika mapinduzi hayo.

Wanawake, ambao ni nusu moja ya jamii ya Wairani, si tu hawakubaki nyuma wakati wa vuguvugu na harakati za mapinduzi, lakini pia walikuwa na nafasi na mchango muhimu katika mapinduzi hayo. Kushiriki kwao katika maandamano na mapambano kulikuwa kwa kiwango kikubwa kiasi cha kuwafanya moja ya vielezo muhimu vya mapinduzi. Wakati vuguvugu la mapinduzi lilipopamba moto, wanawake Waislamu wa Iran, ambao kabla ya hapo walikuwa wakishiriki kwenye harakati za chini kwa chini za mapambano, wakiwa ni ama mama wa mashahidi wa mapinduzi au wake wa wanamapambano walioko kwenye magereza ya Shah, walianza kujitokeza barabarani, wakiwa wamejisitiri kikamilifu kwa vazi la staha la Hijabu ya Chador na wakiwa wamewabeba pia watoto wao huku wamekunja ngumi na kupaza sauti juu kwa kutoa nara za "Mauti kwa Shah, mauti kwa Shah". Imam Ruhullah Khomeini (MA), kiongozi mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu na mwasisi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliizungumzia hali hiyo kwa kuhoji: "Ni katika historia gani mumewahi kuona hali kama hii? Leo wanawake wamewabeba watoto wao wanaonyonya na kuingia kwenye medani za kukabiliana na bunduki na vifaru; ni katika historia gani umeshuhudiwa ushujaa na kujitolea mhanga wanawake kwa namna hii."

Wanawake Waislamu wa Iran wakishiriki katika maandamano ya kufanikisha ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu

Wanawake waelewa na wenye adhama wa Kiirani walifungamanisha mapenzi yao ya umama na mapenzi ya Mwenyezi Mungu. Waliziandaa roho na nafsi za watoto wao na kizazi walichokilea kwa huruma na upendo mkubwa na kukikuza kwa tabu na mashaka, na kukiweka tayari kujitoa mhanga na kuuawa shahidi. Ni kwa sababu hiyo, Imam Khomeini, alikuwa akiwataja wanawake katika hotuba zake mbalimbali kuwa ni watu walio mstari wa mbele katika Mapinduzi na kuwaelezea kuwa ni wanawake ambao: "walikuwa safu ya mbele katika maandamano; ambao kwa harakati zao, waliwahamasisha wanaume kuingia kwenye mapambano; wanawake ambao waliwapa watoto wao malezi ya kuwafanya wawe tayari kufa shahidi; wanawake ambao wameyafanya mapinduzi yadumu kwa kuilinda damu ya mashahidi…" Na katika sentensi moja wadhiha na inayojitosheleza, Imam Khomeini (MA) alisema: "Mafanikio ya harakati yetu, yametokana na wanawake." Na kwa hakika kauli hii, kuliko maelezo mengine yoyote yale, inatosha kubainisha nafasi na mchango wa wanawake katika ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu.

Katika hekaheka za Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, baadhi ya wanawake waliokuwa wakihudhuria mikutano ya kisiasa, walikuwa baada ya mikutano hiyo, wakifanya vikao na wanawake wenzao ili kuwajuvya mambo muhimu na tarehe za maandamano. Baadhi yao wakishirikiana na jamaa wa familia zingine kuwapa hifadhi wanamapambano waliokuwa wakisakwa na askari wa utawala, na vilevile kuwauguza wanampambano waliojeruhiwa, ambao haikuwezekana kuwapeleka hospitalini. Moja ya harakati kubwa zilizokuwa zikifanywa na wanawake ilikuwa ni kushiriki kwenye maandamano wakiwa wamejisitiri na kuchunga thamani za Kiislamu. Mbali na kushiriki wao wenyewe kwenye maandamano, wanawake walikuwa na mchango mkubwa pia katika kuwashajiisha na kuwahamasisha waume na watoto wao kujiunga na vuguvugu la Mapinduzi ya Kiislamu. Katika kila pembe ya Iran, kuna wanawake wengi ambao waliuawa shahidi wakati wa vuguvugu hilo. Miongoni mwa mashahidi wa jamii za jadi za Iran, moja ya majina yanayong'aa ni la mwanamke aitwaye Bakhtar Biglari. Bi Bakhtar alikuwa na umri wa miaka 30 na mama wa watoto wawili wadogo. Alipopata habari za mapambano ya Imam Khomeini dhidi ya utawala wa Shah, kwa kufuata sira ya Bibi Zainab (as), simba wa mapambano ya Karbala, yeye pamoja na mumewe na watoto wake wawili walijiunga na mapambano dhidi ya utawala wa Shah yaliyoendeshwa na jamii za jadi za Lor na Nafar katika eneo la Lorestan. Wakati askari katili wa utawala huo walipowamiminia risasi waandamanaji, mume wa Bakhtar na mwanawe wa kiume mwenye umri wa miaka mitatu waliuawa shahidi. Mwanamke huyo alipambana kiume na kukabiliana kishujaa na askari hao; na yeye mwenyewe pia akauliwa shahidi. Jina la Bakhtar limesajiliwa kwa anuani ya shahidi wa kwanza mwanamke wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Kwa kuelewa mchango mkubwa mno wa wanawake katika Mapinduzi, Imam Khomeini anasema: "Akina mama wetu wapenzi, wamekuwa sababu ya wanaume pia kuwa na uthubutu na ushujaa. Sisi tunapaswa kuwashukuru wanawake kwa tabu walizopata."

Bakhtar Biglari, shahidi wa mwanzo mwanamke wa Mapinduzi ya Kiislamu

Mchango athirifu wa wanawake wa Kiirani katika Mapinduzi ya Kiislamu, ulipanuka na kuwa mkubwa zaidi baada ya ushindi wa mapinduzi hayo. Wanawake hao wamejitokeza na kushiriki kikamilifu katika nyuga mbali mbali za kisiasa, kijamii na kiutamaduni; na viongozi wa Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu, nao pia wameupokea kwa mikono miwili ushiriki na uwajibikaji huo wa wanawake Waislamu wa Iran. Ushiriki athirifu wa wanawake wanamapinduzi wa Iran katika nyuga zote muhimu nchini kunatoa ujumbe kwa walimwengu kwamba, kinyume na baadhi ya tawala na makundi yanayojionyesha kidhahiri kuwa ya Kiislamu katika eneo hili, ambayo yamewabana mno wanawake; katika Uislamu, wanawake wanaweza kushiriki bega kwa bega na wanaume katika shughuli za kijamii watakapokuwa tu wamechunga mipaka ya Kiislamu.

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wakati wa vita vya kulazimishwa vya miaka minane, vilivyoanzishwa na Iraq dhidi ya Iran, wanawake wa Kiirani walisimama imara mithili ya jabali, wakashika nafasi za waume zao waliokufa shahidi kwa kushughulikia malezi na matunzo ya watoto wao. Baadhi ya akina mama waliwatoa watoto wao watatu hadi wanne katika njia ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuihami dini na nchi yao; na kwa njia hiyo wakayalinda malengo matukufu yaliyopiganiwa na Uislamu. Kwa hakika subira na uvumilivu ulioonyeshwa na wanawake hao ni kitu kisichoweza kutasawarika ndani ya akili za watu wengi.

Moja ya nyuga zenye ushiriki mkubwa wa wanawake nchini Iran ni za elimu na taaluma. Imam Khomeini alikuwa akisema: "Mwanamke inapasa ajihusishe na masuala yanayouhusu Uislamu nchini. Nyinyi kama ambavyo mlikuwa na mchango mkuu katika harakati na mlikuwa na nafasi, hivi sasa pia inapasa muwe na nafasi katika ushindi; na msisahau kuwa kila itapohitajika, endesheni harakati na mapambano." Umuhimu ambao uongozi wa Mapinduzi umetoa kwa suala la kuwajenga na kuwaendeleza wanawake katika Mfumo wa Kiislamu umewafanya wanawake wanawake washiriki katika nyuga mbalimbali na kuongeza kiwango cha ushiriki wao katika uga wa elimu na mafunzo. Hivi sasa, mbali na ongezeko kubwa la idadi ya wanawake wa Kiirani wanaojua kusoma na kuandika, hamu na shauku ya kupenda elimu na kiwango cha mafanikio wanayopata wasichana katika mitihani mbalimbali ya kielimu kimeongezeka kwa kiwango kikubwa. Kwa sasa, zaidi ya asilimia 68 ya nafasi za elimu ya juu nchini Iran zinashikiliwa na wanafunzi wa kike. Kiwango cha asilimia 34 cha wanawake waliokuwa wakijua kusoma na kuandika katika miaka ya kabla ya Mapinduzi, kimepanda na kufikia asilimia 80 katika miaka ya baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu. Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka 2012 ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (UNESCO), Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni moja ya nchi sita duniani zinazoongoza katika uwezeshaji wa kupata elimu kwa msingi wa usawa wa kijinsia. Aidha katika miaka ya karibuni na kutokana na sisitizo la Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei, la kuanzishwa harakati ya kuzalisha sayansi nchini Iran, tumekuwa tukishuhudia kuchanua kwa vipawa vya wasichana wabunifu na ushiriki wao katika mashindano ya kielimu ya Olympiad duniani. Kuongezeka na kustawi ushiriki wa wanawake wa Kiirani katika nyanja tofauti za sayansi na teknolojia zikiwemo za kuanzisha ubunifu na utaalamu katika uga wa teknolojia ya Nano, nishati ya nyuklia, anga za mbali, sayansi msingi n.k, ni sehemu ya maendeleo waliyopata wanawake wa Kiirani katika miaka ya baada ya Mapinduzi ya Kiislamu. Leo hii wanawake nchini Iran wananufaika na kuzitumia bila ya tabu yoyote haki zao mbali mbali zikiwemo za kupiga kura katika uchaguzi, kuajiriwa serikalini na hata kushika baadhi ya nyadhifa na nafasi za uongozi, ilhali katika baadhi ya nchi zingine za Kiislamu, wanawake wangali wameshindwa kupata hata baadhi ya haki zao za msingi kabisa.

Wanafunzi wa Iran walioshinda mashindano ya kimataifa ya masomo ya Sayansi ya Olympiad

Hamu na shauku waliyonayo wanawake ya kuinua kiwango chao cha elimu kwa kushiriki kikamilifu katika taasisi za kielimu na vyuo vikuu, imewapatia fursa mpya za kudhihirisha vipawa na uwezo wao. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, wanawake wamepata fursa ya kutoa mchango katika nyuga za kisayansi na utafiti. Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatullah Khamenei, anasema, kujaaliwa Iran ya Kiislamu kuwa na idadi kubwa ya wanawake wenye vipaji, wasomi, wanafikra na wenye uwezo mkubwa ni miongoni mwa neema za Mwenyezi Mungu na moja ya fahari kubwa zaidi za Jamhuri ya Kiislamu na analifafanua hilo kwa kusema: “Leo bendera ya kujitegemea kiutambulisho na kiutamaduni wanawake, imebebwa na wanawake wa Kiirani; leo akina mama wa Kiirani wanaitangazia dunia kujitawala kwao kiutambulisho na kujitawala kwao kiutamaduni huku wakiwa wamechunga hijabu; yaani dunia inasikia kitu kipya. Mwanamke anaweza kushiriki kikamilifu katika nyuga za kijamii na kuwa na taathira kubwa kijamii. Leo wanawake wa nchi yetu wanatoa mchango wenye taathira chanya katika sekta mbali mbali; lakini wakati huo huo kuchunga hijabu na staha, kulinda mipaka baina ya mwanamke na mwanamme, kutokubali kutumiwa vibaya na wanaume, kutojiona kuwa ni bidhaa ya kustarehesha wanaume wasio maharimu na wenye uchu na kutojishusha hadhi na kutojidunisha ni miongoni mwa sifa maalumu alizonazo leo hii mwanamke wa Kiirani na mwanamke Muislamu.”

Ni kwa namna hii wanawake wa Kiirani wametambulika kama washiriki imara na wenye taathira kubwa katika Mapinduzi ya Kiislamu; na kwa upande mwingine Mapinduzi ya Kiislamu yameleta mageuzi na mabadiliko kadhaa katika utamaduni na muundo wa kifikra wa jamii hususan miongoni mwa wanawake wa kiwango kisichotasawarika kuhusiana na hali zao.  Kuongezeka idadi ya wahitimu wa vyuo vikuu, wanafunzi na wanavyuo, wahadhiri wa vyuo vikuu, wasanii, waajiriwa na wadau amilifu wa kiuchumi na kijamii, kupewa umuhimu maalumu hali ya haki za wanawake na kupitishwa sheria zinazoendana na hali zao kwa sasa, kama sheria ya “kuainisha mahari kulingana na thamani ya fedha”, kuzingatia hali ya ajira ya wanawake, kupitisha sheria zinazoendana na hadhi ya wanawake ambao ni mama na mama wa nyumbani, ikiwemo kutumia likizo ya uzazi, kufanya kazi nusu ya muda rasmi, kustaafu kabla ya wakati n.k …. ni miongoni mwa matunda ya miaka 40 ya Mapinduzi kwa ajili ya wanawake, japokuwa kungali kuna safari ndefu kabla ya kufikia malengo kamili yaliyokusudiwa.../

 

 

 

Tags