Feb 10, 2019 08:10 UTC
  • Taathira za Kimataifa za Mapinduzi ya Kislamu ya Iran

Ni wasaa na wakati mwingine mpenzi msikilizaji unapokutana nami Salum Bendera katika mfululizo huu wa vipindi hivi maalumu vya Alfajiri Kumi vinavyokujieni kwa manasaba wa maadhimisho ya miaka 40 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu yaliyotokea mwaka 1979 kwa uongozi wa Imam Ruhullah Khomeini.

 

Kipindi chetu cha leo kitatupia jicho Taathira za Kimataifa za Mapinduzi haya ya Kiislamu  ambayo yamefikia muongo wake wa nne.

Karibuni.

Wananchi wa Iran wanaadhimisha kutimia miaka 40 ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu katika hali ambayo, mwangwi mzuri wenye risala na ujumbe wa Mapinduzi yao unasikika kuanzia mashariki hadi magharibi mwa Ulimwengu wa Kiislamu. Katika siku za awali za ushindi wa harakati ya Mapinduzi ya Kiislamu wakati Imam Khomeini MA alipokuwa akiwataka wananchi wa Iran kuufikisha wito wa Mapinduzi haya nje ya mipaka ya nchi, baadhi hawakuweza kudiriki kina cha maneno haya; lakini hivi sasa ambapo imepita miaka 40 tangu Mapinduzi haya yapate ushindi, wapinzani na waungaji mkono wake wanashuhudia kwamba,  misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu imepata nafasi yake katika fikra za Waislamu ulimwenguni bila ya vita au kutumia mabavu. Mafanikio haya bila shaka hayatokani na kitu kingine bighairi ya kuwa, risala ya Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran ni ujumbe unaoendana na fitra na maumbile salama ya mwanadamu. Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu anasema kuhusiana na hili:

Mafahimu ya Mapinduzi na Uislamu ni mithili ya harufu nzuri ya maua katika msimu wa machipuo; hakuna anaeweza kuzuia kuenea kwa harufu hiyo nzuri. Husambaa kila mahala na ni upepo mwanana wenye kuleta utulivu wa kiroho  ambao hufika kila mahala.

 

Ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ulizifanya jamii za Kiislamu kuondoka katika hali ya kulegalega na kujiona kuwa haziwezi kufanya kitu, na kuzisukuma zifanye hima na bidii kwa minajili ya kurejea katika utambulisho wao wa Kiislamu. Hatua ya Mapinduzi ya Kiislamu ya kuzalisha tena maarifa aali na yenye thamani ya Kiislamu, iliwafanya Waislamu kupata tena utambulisho na shakhsia yao ya Kiislamu na kwa mara nyingine tena, mafundisho hai ya Uislamu yakarejea na kuwa kiigizo.

Hii ni katika hali ambayo, Umma wa Kiislamu kutokana na kukumbwa na mghafala, kwa muda mrefu ulikuwa umesahau kabisa ukweli huu. Harakati ya Kiislamu ya wananchi wa Iran ilipata ushindi ikiwa mikono mitupu mbele ya utawala wa Kifalme wa Kiphalavi uliokuwa na silaha na ambao ulikuwa ukiungwa mkono na madola makubwa na yanayotumia mabavu. Bila shaka, risala muhimu ya ushindi huu kwa Ulimwengu wa Kiislamu ilikuwa hii kwamba, Umma wa Kiislamu unaweza kuwa huru, unaweza kupata maendeleo, ukiwa na uelewa, wenye nguvu na uwezo na yote haya yanawezekana kwa baraka za mafundisho ya Kiislamu.

Miongoni mwa mataifa mbalimbali, Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalikuwa na taathira kubwa mno na ya kuzingatiwa kwa Waislamu wa Kishia nchini Lebanon. Hima, juhudi na harakati za mwamko za Imam Mussa Sadr katika kipindi chote cha kabla ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran pamoja na hali maalumu iliyokuwa likikabiliwa nayo eneo la kusini mwa Lebanon yaani kukaliwa kwa mabavu eneo hilo na utawala vamizi wa Israel na kudhulumiwa Mashia ambako hakukuwahi kushuhudiwa, ni mambo ambayo katika kipindi hicho yaliifanya Lebanon iwe na utayari zaidi ikilinganishwa na maeneo mengine ya ardhi za Kiislamu wa kuupokea ujumbe na risala ya Mapinduzi. Kushindwa mtawalia Waarabu na utawala bandia wa Israel, kuhisi kuwa duni na kuigopa Israel miongoni mwa wananchi wa Lebanon, kutofanikiwa makundi amilifu katika medani ya kimapambano na kisiasa ya Lebanon katika kukabiliana na wavamizi na kushindwa jeshi la taifa ni mambo ambayo yalipelekea kuongezeka hisia za chuki dhidi ya adui na kukajitokeza mwamko wa matumaini ya kuwa kifua mbele Uislamu katika nyoyo za Waislamu wa Lebanon.

Imam Mussa Sadr

Katika mazingira kama haya, tajiriba ya mafanikio ya wananchi wa Iran katika kupambana na dhulma na Uistikbari ilipelekea muda mfupi tu baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu kukaasiwa Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Hizbullah ya Lebanon mnano mwaka 1980 kwa miongozo ya Imam Mussa Sadr. Katika mapambano yake na Israel, Harakati ya Hizbullah ya Lebanon ilipata ushindi na mafanikio muhimu na hata ikaweza kuzikomboa ardhi za kusini mwa nchi hiyo zilizokuwa zikikaliwa kwa mabavu na utawala dhalimu wa Israel. Baada ya Hizbullah kuwa na nafasi muhimu katika vita na mapambano dhidi ya Israel, ikaondokea pia kuwa na nafasi isiyo na kifani katika uga wa kisiasa na kijamii na kadhalika kuwa na nafasi athirifu katika uchaguzi wa Bunge, Mabaraza ya Miji na Vijiji. Hii ni katika hali ambayo, kabla ya hapo, Waislamu wa Kishia nchini Lebanon hawakuwa na mahudhurio katika muundo wa nguvu na madaraka katika nchi hiyo.

Aidha moja ya mifano ya wazi ya kukubaliwa na kupokelewa risala na ujumbe wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran na kuenea kwake katika kona mbalimbali za dunia licha ya kuweko masafa makubwa ni Waislamu wa Nigeria. Nchi ya Kiafrika ya Nigeria ambayo inajulikana na The Giant of Afrika, inahesabiwa kuwa nchi yenye idadi kubwa zaidi ya watu barani Afrika ambapo kwa mujibu wa takwimu za mwaka 2017 ilikuwa na watu milioni 190 na laki tisa.  Asilimia 50 ya wananchi wa Nigeria ni Waislamu na akthari yao ni Waislamu wa madhehebu ya Sunni wanaofuata fikihi ya Imam Maliki. Asilimia 40 ya wananchi wa Nigeria ni Wakristo na asilimia kumi iliyobakia ni wafuasi wa dini za kijadi. Uislamu uliingia nchini Nigeria mwanzoni mwa karne ya Pili Hijria kupitia wahubiri na wafanyabiashara.

Kwa hakika, ushindi wa Mapinduzi ya Kislamu ulikuwa adia na zawadi kwa maisha na kuleta matumaini miongoni mwa Waislamu nchini Nigeria. Sheikh Ibrahim Zakzaky akiwa kijana mwenye nishati, hamasa na shauku na aliyekuwa na harakati za Kihawza na Chuo Kikuu alifanya safari nchini Iran mwanzoni mwa Mapinduzi ya Kiislamu. Baada ya kukutana na Imam Khomeini, Sheikh Ibrahim Zakzaky aliyakumbatia na kuyakubali madhehebu ya Kishia. Baada ya kurejea nchini Nigeria, alianzisha harakati kubwa kwa ajili ya kuwaamsha Waislamu na kufanikiwa kuasisi harakati kubwa ya Kiislamu. Harakati zake katika kipindi cha miongo mitatu iliyopita, zilipelekea idadi ya Mashia wa Nigeria kuongezeka na kufikia milioni kumi.

Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria

Kuitegemea dini pamoja na uwezo wake katika kuiongoza na kuisimamia kwa njia sahihi jamii na kuwa na imani na nguvu ya umoja ilikuwa zawadi yenye thamani ya Mapinduzi ya Kiislamu kwa ajili ya Waislamu wa Nigeria. Wananchi hao ambao walikuwa na kigugumizi mkabala na vitendo na hatua zilizo dhidi ya dini wakabadilika na kuwa miongoni mwa makundi ya harakati amilifu na zenye kupigania haki zao ambao wako tayari kujitolea uhai na maisha yao kwa ajili ya malengo yao ya kidini. Moja ya mifano ya wazi katika kadhia hii ni ni suala la vazi tukufu la Hijabu ambapo kwa miaka mingi mabinti wa Kiislamu walikuwa wamepigwa marufuku kuvaa vazi hilo mashuleni na katika Vyuo Vikuu.

Waislamu wa kaskazini mwa Nigeria baada ya miaka mingi ya kusimama kidete hatimaye walifanikiwa kuwakinaisha viongozi wa majimbo yenye wakazi Waislamu kwamba, mabinti wa Kiislamu wanapaswa kuruhusiwa kuvaa hijabu wakiwa shuleni. Maandamano ya Waislamu wa Nigeria yenye lengo la kutaka kuweko Sharia za Kiislamu yanaweza kutajwa kuwa yameathirika na Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran. Hatimaye serikali ya Nigeria ikalazimika  kusalimu amri mbele ya matakwa ya Waislamu kwa kukubali kuweko Sharia za Kiislamu katika majimbo ambayo wakazi wake ni Waislamu.

Hii leo Mashia wa Nigeria ni miongoni mwa makundi amilifu ya Kishia ulimwenguni ambapo si tu kwamba, hawanyamazii kimya matukio ya ndani ya nchi hiyo bali wamekuwa wakifuatilia na kukemea siasa za kidhulma na ukandamizaji katika maeneo mbalimbali ya Ulimwengu wa Kiislamu. Harakati hiyo ambayo ilianza baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran, imekuwa na msukumo maradufu kwa wahakiki na watafiki wa Uislamu kutaka kuufahamu zaidi Ushia.

Wakati Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalipopata ushindi mwaka 1979 ilikuwa imepita miaka 20 tangu Imam Khomeini MA aanze kueleza na kusema kwamba, Israel ni utawala haramu na usio na uhalali wowote huko Palestina. Kupambana na utawala ghasibu wa Israel ambao ni donda la saratani linalotishia uhai wa Umma wa Kiislamu, tangu awali ulikuwa msingi miongoni mwa misingi ya Mapinduzi ya Kiislamu.

Imam Ruhullah Khomeini MA aliitangaza Ijumaa ya mwisho ya mwezi Mtukufu wa Ramadhani kila mwaka kuwa Siku ya Kimataifa ya Quds na kuwafanya Waislamu ulimwenguni waizingatie na kuipa umuhimu kadhia ya Palestina. Kwa hatua yake hiyo, Imam Khomeini akalifanya suala la Palestina kuwa kadhia ya kwanza na muhimu katika Ulimwengu wa Kiislamu na kukaibuka matumaini mapya ya kukombolewa Palestina.

Kwa hakika Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yalihuisha masuala kama ya Hijabu, vita na mapambano dhidi ya dhulma na ubeberu, yakaleta mfungamano wa dini na siasa sambamba na hamu, shauku na muelekeo wa kutaka utawala wa Kiislamu katika Ulimwengu wa Kiislamu. Aidha Mapinduzi ya Kiislamu ya Iran yamekuwa na taathira muhimu mno kwa harakati ya mwamko wa Kiislamu. Kabla ya hapo na katika anga ya Uliberali na Ukomonisti ni watu wachache waliokuwa na imani ya uwezo dini kuweza kufanya mapinduzi. Mwamko wa Kiislamu unaoshuhudiwa leo katika nchi kama Yemen, Bahrain, Misri, Tunisia, Libya na kwingineko bila shaka ni taathira iliyotokana na Mapinduzi ya Kiislamu.

Wapenzi wasikilizaji muda wa kipindi hiki maalumu umefikia tamati.

Wassalaamu Alaykum Warahmatullahi Wabarakaatuh….

Tags