Feb 02, 2019 04:35 UTC
  • Miaka 40 na juhudi za kuunganisha madhehebu za Kiislamu

Katika mada ya 11 ya Katiba ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran na kwa msingi wa Aya ya Qur'ani Tukufu inayosema: Hakika umma wenu huu ni umma mmoja, na Mimi ni Mola wenu, kwa hivyo niabuduni Mimi, serikali ya Jamhuri ya Kiislamu inawajibika kuratibu siasa zake kuu kwa msingi wa kuleta umoja na mshikamano wa kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni kati ya mataifa yote ya Kiislamu.

Kupitia Aya nyingi za kitabu kitakatifu cha Qur'ani, Mwenyezi Mungu amewataka Waislamu kuungana na kuwa kitu kimoja. Katika maneno na matendo yake yote, Mtume Mtukufu (saw) kwa kufuata mfano huo wa Qur'ani alitetea sana umoja wa Umma wa Kiislamu. Kwa mfano, Mwenyezi Mungu anasema mwanzoni mwa aya ya 103 ya Surat Aal Imran: Na shikamaneni na Kamba ya Mwenyezi Mungu nyote pamoja, wala msifarikiane. Na kumbukeni neema ya Mwenyezi Mungu juu yenu mlipokuwa maadui nyinyi kwa nyinyi naye akaziunganisha nyoyo zenu; kwa neema yake mkawa ndugu.


Kama mnavyojua madola ya kiistikbari na kitaghuti katika kipindi chote cha historia daima yamekuwa yakifanya juhudi za kueneza fitina na mifarakano kati ya mataifa tofauti ili yaweze kufikia kirahisi malengo yao ya kikoloni. Yamekuwa yakitumia kila aina ya mbinu za kisasa kwa madhumuni ya kuudhibiti ulimwengu wa Kiislamu na kuwazuia Waislamu kuhuisha utamaduni wao mkubwa. Hivyo, wameanzisha na kupandikiza madhehebu bandia za Kiislamu kama Uwahabi ili waweze kuwakufurisha Waislamu wengine na kuhalalisha damu zao.

Tokea mwanzoni mwa kubuniwa kwake, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imekuwa ikizingatia sana umuhimu na udharura wa kuwepo umoja wa Kiislamu katika ulimwengu wa Kiislamu. Imam Khomeini (MA) Kiongozi na mwanzilishi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran aliuchukulia umoja wa Waislamu kuwa moja ya malengo makuu ya mfumo wa Kiislamu na akisema miaka 15 kabla ya kufikiwa ushindi Mapinduzi ya Kiislamu nchini: 'Mpango wetu ambao ni mpango wa Kiislamu ni kuwaunganisha Waislamu, mataifa ya Kiislamu, kuleta udugu kati ya madhehebu yote ya Kiislamu na maelewano kati ya serikali za Kiislamu.' Sisistizo hilo la mwanzilishi wa Mapinduzi ya Kiislamu juu ya kuwepo umoja na mshikamano katika ulimwengu wa Kiislamu na kufanya juhudi za kufikiwa malengo matukufu ya Umma wa Kiislamu kuliyakurubisha pamoja mataifa ya Kiislamu na hivyo kuyawezesha kwa kiwango fulani kuimarisha umoja miongoni mwao. Imam Khomeini alikuwa akiamini sana umuhimu wa umoja wa Umma wa Kiislamu katika kubuniwa serikali ya Kiislamu. Katika hutuba aliyotoa mwaka 1969 huko katika mji mtakataifu wa Najf nchini Iraq, Imam Khomeini (MA) alisema: Ili tupate kudhamini umoja wa Umma wa Kiislamu na kuzikomboa nchi za Kiislamu kutokana na ukoloni wa wakoloni na serikali zao za kibaraka, hatuna chaguo jingine ila kuunda serikali. Hii ni kwa sababu ili kuleta umoja na uhuru katika mataifa ya Kiislamu tunapasa kuziangusha serikali zote za kidhalimu na kibaraka na kisha kuasisi serikali adilifu za Kiislamu ambazo zitawahudumia wananchi. Kubuniwa serikali ni kwa ajili ya kulinda mfumo na umoja wa Waislamu.'

Imam Khomeini (MA) daima alikuwa akisisitiza umoja wa mataifa ya Kiislamu

Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, umoja wa Kiislamu ilichukuliwa kuwa moja ya nguzo muhimu za siasa za ndani na nje ya nchi. Ni kwa msingi huo ndipo tangu kuasisiwa kwake, Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ambayo imebuniwa katika msingi wa kuyaunganisha makundi, madhehebu na makabila yote chini ya bendera ya Uislamu, ikawa inasisitiza na kuandaa kila mwaka Wiki ya Umoja wa Kiislamu kwa shabaha ya kuwaunganisha wafuasi wa madhehebu ya Shia na Suni. Ubunifu wa kuanzisha Wiki ya Umoja wa Kiislamu ulianzishwa na Imam Khomeini (MA) kwa lengo la kuhuisha thamani za kidini kati ya Umma wa Kiislamu na kuzingatia nukta za pamoja miongoni mwa jamii za Kiislamu. Kwa msingi huo, Wiki hii huadhimishwa tokea tarehe  12 hadi 17 Rabiul Awwal kutokana na kuwa kwa mujibu wa Riwaya ya Ahlu Suna, Mtume Mtukufu (saw) alizaliwa tarehe 12 na kwa mujibu wa Mashia mtukufu huo alizaliwa tarehe 17 Rabiul Awwal. Hivyo Imam Khomeini alianzisha fikra ya kuadhimisha Wiki ya Umoja wa Kiislamu kati ya tarehe mbili hizo ili kupunguza mvutano na kuimarisha umoja na udugu kati ya Waislamu wa madhehebu mbili hizo. Katika siku za wiki hii muhimu, makongamano, sherehe na mikusanyoko ya Waislamu hufanyika nchini Iran na nchi nyingine za dunia ambapo Waislamu huzungumzia umuhimu wa kuimarisha umoja na udugu muiongoni mwao kwa ajili ya kuhuisha utamaduni na ustaarabu mkongwe wa Umma wa Kiislamu.

Baada ya kuaga dunia Imam Khomeini (MA) na kuchukua mahala pake Ayatullah Ali Khamenei, Muadhamu huyo pia amekuwa akisisitiza mara kwa mara na kwa namna maalumu udharura wa kuwepo umoja na mshikamanao kati ya mataifa ya Kiislamu. Katika siku za kwanza za jukumu lake zito la kuhudumia nchi kama Kiongozi Muadhamu, Ayatullah Khamenei alisisitiza umuhimu wa kuondolewa hitilafu kwa kusema: 'Wakati tunapopiga nara ya 'umoja' tunapasa kuzingatia nukta mbili; ya kwanza ni kuondoa hitilafu na migongano, ghasia na hiana ambazo zimekuwepo kati ya makundi tofauti ya  Waislamu tokea karne nyingi zilizopita hadi leo, hiana ambazo daima zimekuwa na madhara kwa Waislamu. Nukta ya pili ni kwamba umoja unapasa kuwa kwa maslahi ya serikali ya Kiislamu. Wanazuoni wa Kiislamu wanakubali kwamba Aya ya 64 ya Surat an-Nisaa inayosema: Na hatukumpeleka Mtume ila atiiwe kwa amri ya Mwenyezi Mungu, haikuteremka kwa ajili ya Mtume kutoa nasaha, atamke maneno na watu waendelee kufanya mambo yao ya kawaida huku wakimtii kidhahiri tu, bali alitumwa kwa ajili ya kutiiwa, aongoze jamii aunde mfumo wa uongozi na kuwaongoza wanadamu kuelelekea malengo maalumu ya maisha sahihi. Hivyo harakati inapaswa kufanywa kwa madhumuni ya kuasisi utawala wa Kiislamu, na utawala wa Kiislamu katika nchi na jamii za Kiislamu ni jambo linalowezekana (hotuba ya tarehe 8/10/1990).

Katika hotuba zake, Ayatullah Khamenei daima amekuwa akisisitiza kwa njia maalumu umuhimu wa Umoja wa Kiislamu

Katika hotuba zake, Ayatullah Khamenei daima amekuwa akisisitiza kwa njia maalumu umuhimu wa Umoja wa Kiislamu. Amethibitisha kivitendo suala hilo kwa kuanzisha Jumuiya ya Kukurubisha pamoja Madhehebu za Kiislamu na vilevile kuunga mkono kwa hali na mali vikao vya Kongamano la Umoja wa Kiislamu. Jukumu la jumuiya hiyo ni kunyanyua kiwango cha uelewa na kuimarisha maelewano baina ya wafuasia wa madhehebu ya Kiislamu, heshima ya pande mbili na udugu wa Kiislamu baina ya Waislamu kwa ajili ya kufikiwa Umma mmoja wa Kiislamu. Jumuiya ya Kimataifa ya Ahlul Beit ikiwa ni shirika lisilo la kiserikali na la kimataifa iliasisiwa mwaka 1990 katika mtazamo mpana wa kuimarisha umoja wa Kiislamu duniani. Tasisi hiyo muhimu ina jukumu la kuimarisha umoja katika Umma wa Kiislamu na hasa miongoni mwa wafuasi wa Madhehebu ya Ahlul Beit (as), pamoja na kuwatetea Waislamu katika pembe mbalimbali za dunia.

Bila shaka fatwa za wanazuoni wa Kiislamu zina nafasi muhimu katika kuunganisha au kuugawa ulimwengu wa Kiislamu. Iwapo Mujtahid na wanazuoni hao watatoa fatwa ya kuruhusu Waislamu wa madhebu moja kushiriki katika marasimu na sherehe za madhehebu nyingine ya Kiislamu bila shaka jambo hilo litakuwa na nafasi muhimu katika kuimarisha umoja na udugu kati ya Waislamu. Fatwa ya Ayatullah Khamenei akiwa Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu na marja' wa Mashia, kuhusu kuruhusiwa kwao kushiriki katika swala za jamaa za Masuni na vilevile kuharamishwa kutusiwa matukufu ya ndugu wa Kisuni, kukiwemo kutuhumiwa wake za Mtume (saw) ilikaribishwa na kuungwa mkono pakubwa katika ulimwengu wa Kiislamu, na hasa wanazuoni wa Kisuni. Jambo hilo bila shaka liliimarisha pakubwa umoja na mshikamano kati ya wafuasi wa madhehebu mbili hizi za Kiislamu.

Ni wazi kuwa suala lililo na umuhimu mkubwa hivi sasa katika ulimwengu wa Kiislamu ni suala la Palestina na Quds Tukufu. Quds bila shaka ndiyo nembo iliyo na uwezo mkubwa zaidi wa kuwaunganisha Waislamu bila kujali madhehebu zao. Kama mnavyojua, baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu, Iran iliweza kuwa nguvu kubwa ya eneo na kubadilika kuwa adui mkubwa wa utawala ghasibu wa Israel, utawala ambao ulikuwa ikiona mipaka yake ikianzia Mto Nile hadi Mto Furati katika Mashariki ya Kati. Baada ya ushindi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran utawala huo ulilazimika kujizingira kwa ukuta na kusahau kabisa ndoto yake hiyo ya kubuni Israel Kubwa katika eneo. Ni wazi kuwa mafanikio hayo makubwa hayangeweza kufikiwa kama usingekuwepo umoja na mshikamano wa vijana wa Iran, Lebanon, Syria, Iraq, Afghanistan na nchi nyingine za eneo. Muhimu zaidi kuliko masuala mengine yote ni kudhoofika na kusambaratika kwa ndani utawala huo haramu, ambapo hata mashirika ya kijasusi ya Marekani yenyewe yanakiri jambo hilo na kutabiri kuwa utawala huo utadumu kwa karibu miaka 20 tu ijayo.

Tukimalizia, tunaweza kusema kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran imefanya juhudi kubwa katika kipindi cha miaka 40 iliyopita kwa ajili ya kuimarisha umoja miongoni mwa madhehebu za Kiislamu na daima imekuwa ikilichukulia suala hilo kuwa moja ya nguzo kuu za stratejia zake. Sawa kabisa kama anavyosema Ludwig Hagemann, mhadhiri wa taaluma ya masuala ya kidini katika chuo kikuu cha Würzburg nchini Ujerumani: 'Viongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu nchini Iran licha ya kuwa ni Mashia na Mashia wanaunda asilimia ndogo tu ya Waislamu wote duniani, lakini hawajaacha shaka yoyote kuwa mapinduzi yao si ya Mashia wala Wairani pekee bali ni ya kuunganisha Umma mzima wa Kiislamu.'

Tags