Apr 06, 2020 06:29 UTC
  • Jumamosi, 4 Aprili, 2020

Leo ni Jumamosi tarehe 10 Shaaban 1441 Hijria, ambayo inasadifiana na tarehe 4 Aprili 2020 Miladia.

Siku kama ya leo miaka 1019 iliyopita, alifariki dunia mjini Baghdad, Iraq Abu Abdillah Abdul-Baqi, mmoja wa malenga mashuhuri wa karne ya tano Hijiria. Mbali na kusoma kwa maulama wakubwa wa fasihi, pia alipata fursa ya kushiriki masomo ya kidini kwa maulama wakubwa wa mji huo na kuweza kustafidi  na elimu tofauti, hususan elimu ya hadithi na kadhalika. Mashairi ya Abu Abdillah Abdul-Baqi yalikuwa ya kipekee kiusomaji mashairi na ameacha athari nyingi katika uwanja huo. ***

Abu Abdillah Abdul-Baqi

 

Katika siku kama ya leo miaka 687 iliyopita,  alifariki dunia Majdud-Din Abul-Fawaaris, mmoja wa maulama wakubwa wa Kiislamu. Alizaliwa nchini Iraq na baada ya kuhitimu elimu ya msingi, alianza kusoma kwa maulama wakubwa na kufanikiwa kufikia daraja ya juu kielimu na kutokea kuwa mwalimu. Majdud-Din Abul-Fawaaris, alitabahari sana katika elimu za fiqhi, usulu fiqhi, hadithi, theolojia, tafsiri ya Qur'ani na fasihi ya lugha ya Kiarabu. Kuna athari nyingi kutoka kwa msomi huyo mkubwa wa Kiislamu na mojawapo ni kitabu kinachoitwa 'Kanzul-Fawaaidi.'***

Majdud-Din Abul-Fawaaris

 

Miaka 95 iliyopita katika siku kama ya leo,  aliaga dunia Muhammad Ali Shah, mfalme dhalimu wa ukoo wa Qajar nchini Iran. Muhammad Ali Shah alizaliwa 1249 Hijria Shamsia katika mji wa Tabriz na baada ya kusoma kidogo, akiwa na umri wa miaka 17 alianza kufanya kazi yake ya kwanza serikalini. Baada ya Mozaffar ad-Din Shah Qajar kuingia madarakani, Muhammad Ali Shah aliteuliwa kuwa mrithi wa kiti cha ufalme.  ***

Muhammad Ali Shah,

 

Katika siku kama ya leo miaka 60 iliyopita, Senegal inayopatikana magharibi mwa Afrika ilipata uhuru. Senegal ilikuwa chini ya ushawishi na ukoloni wa Wareno kuanzia karne ya 15 Miladia na kuanzia karne ya 17 pia Wafaransa nao walianza kuiba maliasili na utajiri wa nchi hiyo. Senegal iko katika pwani ya bahari ya Atlantic huku ikipakana na Mauritania, Mali na Guinea Bissau.***

Bendera ya Senegal

 

Siku kama ya leo miaka 52 iliyopita, Martin Luther King kiongoziwa mapambano ya raia weusi wa Marekani aliuawa kwa kupigwa risasi na mtu mmoja au watu kadhaa wasiojulikana. Martin Luther alizaliwa mwaka 1929 katika mji wa Atlanta huko Marekani. Alipata mafunzo katika Chuo Kikuu cha Boston na baadae akaanza kuongoza harakati ya ukombozi ya Wamarekani weusi dhidi ya ubaguzi wa rangi waliokuwa wakifanyiwa raia weusi nchini Marekani. Katika kipindi hicho raia weusi wa Marekani waliasisi harakati ya nchi nzima ya kupinga ubaguzi wa rangi na vilevile katika kulalamikia sheria iliyokuwa ikiwatambua wazungu kama watu wa daraja ya juu huko Marekani. Kwa mujibu wa baadhi ya ushahidi ni kuwa shirika la ujasusi la Marekani CIA lilihusika katika mauaji hayo.***

Martin Luther King

 

Na katika siku kama ya leo miaka 41 iliyopita, Zulfiqar Ali Bhutto, Waziri Mkuu wa zamani wa Pakistan alinyongwa. Bhutto ambaye alikuwa mwasisi wa Chama cha Wananchi alikuwa Rais wa Pakistan mwaka 1971. Mwaka 1977 Jenerali Muhammad Dhiaul Haq alifanya mapinduzi na kumuondoa madarakani Bhutto akimtuhumu kwa kufanya mauaji na kuisaliti Pakistan. Hatimaye tarehe 4 Aprili mwaka 1979 Zulfiqar Ali Bhutto alinyongwa, licha ya viongozi wa baadhi ya nchi duniani kutaka asamehewe. ***

Zulfiqar Ali Bhutto,

 

Tags